October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais ‘Kiduku’ aibipu UN

Spread the love

RAIS wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un maarufu kama ‘Kiduku’ kutokana na staili yake ya nywele, amesimamia urushwaji wa kombora la masafa mafupi kuelekea pwani ya Bahari ya Mashariki licha ya Umoja wa Mataifa kumuonya kuhusu harakati zake. Anaripoti Glory Massamu – TUDARCo… (endelea)

Jaribio hilo limefanyika mapema leo tarehe 28 Septemba 2021 ikiwa ni siku chache zimepita tangu Balozi wa taifa hilo, Kim Song kuhutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kupima ubora wa silaha zake.

Akizungumza katika mkutano huo jijini New York unaofanyika kila mwaka, Balozi huyo wa Korea alisema hakuna mtu anayeweza kukataa haki ya nchi yake kujilinda na kujaribu silaha zake.

Awali Korea Kaskazini ilirusha makombora mapema mwezi huu jambo ambalo lililalamikiwa na majirani zao Japan ambao kupitia wizara ya ulinzi ilisema makombora yaliyorushwa yalikuwa ya masafa marefu wakati yamepigwa marufuku na UN.

Hata hivyo, Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in ameliagiza Baraza la Usalama la Taifa la nchi hiyo kuchambua na kufutilia malengo ya kurushwa kwa makombora hayo na kauli za hivi karibuni zilizotolewa na dada yake Rais wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un.

Dada huyo anayefahamika kwa jina la Kim Yo-jong alisema nia ya taifa lao ni kumaliza uhasama kati ya nchi hizo mbili yaani Korea Kusini na Kaskazini.

Korea Kaskazini mara kwa mara imekuwa ikiishutumu Korea Kusini kuhusu ya shughuli zake za kijeshi zinazofanywa na taifa hilo na kusema kua wanahitaji kujilinda na kujenga usalama na amani ya nchi.

Aidha, Marekani ilisema inafahamu kuhusu kombora hilo lakini pia imesema kitendo hicho kinaonyesha athari mbaya ya mpango wa silaha haramu wa Korea Kaskazini.

error: Content is protected !!