April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Kenyatta amfunda Mama Samia

Uhuru Kenyata, Rais wa Kenya

Spread the love

 

RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemzungumzia aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Pombe Magufuli, akisema katika muda mfupi wa uongozi wake, ameonesha njia ya Bara la Afrika kujitegemea kiuchumi na kijamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Kiongozi huyo wa Kenya, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu tarehe 22 Machi 2021, katika shughuli ya kitaifa ya kuuaga mwili wa Hayati Rais Magufuli, kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

“Kwa muda wa miaka michache (miaka mitano na ushehe), ameonesha ya kwamba sisi Afrika tuko na uwezo wa kujitoa katika utegemezi wa watu na nchi za nje na tuko na uwezo kama Waafrika kusimamia uchumi wetu na kuhakikisha wananchi wetu wanatendewa haki,” amesema Rais Kenya.

Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), amesema Hayati Rais Magufuli alikuwa rafiki yake wa karibu, enzi za uhai wake.

“Niko hapa pia kumuombeleza rafiki wa karibu, ambaye alikuwa ni mtu tulikuwa tunaogea mara kwa mara, mchana na jioni tukibadilishana mawazo kuhusu nchi zetu mbili, na kuhusu jumuiya yetu ya EAC,” amesema Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta amemzungumzia Hayati Magufuli akisema “Kwa muda mfupi tumeona kazi ya barabara, kazi ya umeme, tumeona kazi ya ujenzi wa uwanja wa ndege na mengine mengi ambayo yatakuwa na manufaa kwa Watanzania na kutusaidia sisi sote wa Afrika Mashariki, kufanya biashara pamoja kutuletea sote tuwe kitu kimoja.”

Kiongozi huyo wa Kenya amesema, kifo cha Hayati Rais Magufuli, kilichotokea tarehe 17 Machi 2021 “ni pigo kwake.”

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

“Kwangu mimi ni pigo sababu alikuwa mtu wa heshima, na ndipo tukasema sisi kama Wakenya na mimi binafsi ya kwamba iwe liwalo na liwe lazima nije tuungane pamoja nanyi kumsindikiza rais wetu,” amesema Rais Kenyatta.

Mbali na kuomboleza kifo cha Hayati Rais Magufuli, Rais Kenyatta amemhakikishia Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

“Nataka kuwahakikishia ya kwamba, tutaendelea kufanya kazi pamoja, kushirikiana na tutaendelea kuhakikisha ya kwamba tumeleta jumuiya yetu ya EAC pamoja na Bara la Afrika.”

“Sina shaka nikisema hapa siku ya leo ya kwamba dada yangu Samia Suluhu Hassan na sasa rais mwenzangu, barabara umeoneshwa na ndugu yetu Rais Magufuli, barabara imefunguliwa ,” ameahidi Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta amemshauri Rais Samia kumtanguliza Mungu katika kipindi hiki kigumu anachopitia cha Taifa kuondokewa na Hayati Rais Magufuli.

Kiongozi huyo wa Kenya amemuomba Rais Samia asifadhahishwe na msiba huo, bali awe hodari na shujaa, kwani Mungu yu pamoja naye.

“Dada yangu najua wakati huu ni mgumu sana kwako, kwa sababu umechukua usukani wakati mgumu na wakati wa majonzi. Lakini mimi neno pekee ningependa nikuachie siku ya leo, ni lile neno Mungu alipatia Joshua wakati Musa aliaga,” amesema Rais Kenyatta na kuongeza:

“Na Joshua alikua anajiuliza kama ana uwezo wa kuendelea ama kujaza viatu vya Mussa naye Mungu akamuambia uwe hodari, uwe na moyo wa ushujaa usiogope, wala wa usifadhaike kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe kila uendapo.”

Rais Samia anakuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi Tanzania, tangu taifa hilo lipate uhuru.

Kabla ya kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha Hayati Rais Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi 2021, Rais Samia alikuwa Makamu wa Rais.

Rais Samia aliapishwa kuwa Rais wa Tanzania tarehe 19 Machi 2021. Ikulu ndogo jijini Dar es Salaam.

Mwili wa Hayati Rais Magufuli unatarajiwa kuzikwa tarehe 26 Machi mwaka huu, kijijini kwao Chato mkoani Kagera

error: Content is protected !!