Wednesday , 8 February 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Karume, azungumzia muungano wa Maalim Seif na Dk. Mwinyi
Habari za SiasaTangulizi

Rais Karume, azungumzia muungano wa Maalim Seif na Dk. Mwinyi

Aman Abeid Karume, Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
Spread the love

RAIS mstaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, amesifu hatua ya Maalim Seif Sharif Hamad, kukubali kujiunga katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani humo (SUKI). Anaripoti Erasto Masalu, Zanzibar … (endelea).

Akizungumza katika mahojiano yake na MwanaHALISI Online, wiki iliyopita, ofisini kwake, mjini Unguja, Karume alisema, kitendo hicho, kitaiponya nchi na majeraha ya uchaguzi mkuu uliopita na kitasaidia kurejesha matumaini ya wananchi, Unguja na Pemba.

Amesema, “…wananchi wa Zanzibar wanapenda amani. Watu wa Zanzibar wanapenda umoja na mshikamano. Kuvutana vutana, mikwaruzo kwaruzo isiyoisha, hawapendi; wameshachoka nayo.”

Amesema, hatua ya Maalim Seif na chama chake cha ACT- Wazalendo, kukubali kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, kutasaidia kuondosha mifarakano hiyo.

Karume ambaye ni mtoto wa aliyekuwa rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume na ambaye ameongoza Zanzibar kutoka mwaka 2000 hadi 2010 amesema, hatua hiyo imemfurahisha sana kwa kuwa itatimiza kile kilichokusudiwa wakati wa kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

           Soma zaidi:-

“Nimefurahi sana kwa kuwa yale yaliyokuwa malengo yetu, wakati tunaanzisha GNU (Serikali ya Umoja wa Kitaifa), mwaka 2010, sasa yameweza kurejea tena,” ameeleza.

Kauli ya Rais mstaafu imekuja miezi miwili tangu Maalim Seif kuapishwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, kama ambavyo Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, inavyoelekeza.

Maalim Seif, ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar, kupitia ACT-Wazalendo, katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 27 na 28 Oktoba 2020, aliapishwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussen Ali Mwinyi, kushika nafasi wadhifa huo, tarehe 8 Desemba 2020.

Katiba ya Zanzibar, inaelekeza kuwapo Makamo wawili wa Rais – Makamo wa kwanza na yule ya pili – na kusema, “Makamo wa Kwanza wa Rais atatokana na chama kilichoshika nafasi ya pili kikiwa na zaidi ya asilimia kumi ya kura zilizopatikana kwenye uchaguzi mkuu wa rais.”

Kwa matokeo yalivyotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilishinda uchaguzi huo na ACT-Wazalendo, kilishika nafasi ya pili.

Anasema, kitendo cha Maalim Seif na chama chake – The Civic United Front (CUF –Chama cha Wananchi) – kususia uchaguzi wa marudio wa Machi 2016 na hivyo kujitoa rasmi kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa, kumerudisha kwa kiasi kikubwa, “maendeleo visiwani.”

Karume ndiye mwasisi wa mwafaka uliofikiwa mwaka 2010, uliokwenda kuandika Katiba mpya ya Zanzibar iliyoruhusu kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU).

Amesema, “kitendo cha kukaa kando, ni unfortunately (bahati mbaya) kwa maendeleo ya nchi yetu.  Kwa sababu waliacha hali ikawa tete sana, hofu ilikuja tena, wengine wakaona tunarudi kulekule. Nafurahi sasa, Maalim Seif kuamua kuingia tena serikalini.”

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, aliamua kususia uchaguzi wa marudio, kuafuatia aliyekuwa Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Jecha Salim Jecha, kuamua kufuta uchaguzi huo pamoja na matokeo yake.

Karume amesema, mwaka 2010 hadi 2015, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla, zilitulia, baada ya upinzani na CCM, kuamua kukaa pamoja na kuunda serikali.

“Alhamdulilah nchi ilitulia, mambo yakaenda… lakini mwaka 2015 hadi 2020, mambo yakawa magumu sana. Wenzetu wapinzani walikataa kuingia serikalini, wakaamua kukaa kando.”

“Walivyokaa kando, wengine wakasema, wako tayari kuendesha serikali. Nadhani kwa hatua hii ya sasa ya Maalim Seif, mambo yatakwenda vizuri,” amesema Rais mstaafu Karume aliyezaliwa tarehe 1 Novemba 1948.

Alipoulizwa kama aliwahi kuongea na Maalim Seif, kabla ya kuamua kujiunga na serikali iliyopo; na au baada ya kufanya uamuzi huo, Rais mstaafu Karume amesema, “Yes I did” (ndio, niliongea naye) na kuongeza, “and I congratulate him,” (na nilimpongeza kwa uamuzi huo.

Karume amesema, Maalim Seif amefanya yote haya, kwa maslahi mapana ya nchi na watu wake.

Amesema, hatua hiyo itawawafanya watu wanaopenda kuiona Zanzibar inakuwa na umoja na mshikamano, kuanza kupata usingizi, huku akipenda kurejea mara kwa mara, kauli ya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, kuhusiana na migogoro na mivutano ya kisiasa Zanzibar.

Akihutubia mkutano wa kwanza wa Bunge, mjini Dodoma, Desemba mwaka 2010, Rais Kikwete alisema, mgogoro wa Zanzibar, unaninyima usingizi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Bunge labaini madudu mfumo ukusanyaji mapato, h’shauri tatu kikaangoni

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali...

Habari za Siasa

Mkuu wa wilaya ya Rungwe azindua vyumba sita vya madarasa vya thamani ya 64 mil

Spread the love  MKUU wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amezindua vyumba...

Habari za Siasa

Mbunge afurahia mabilioni ya Samia kutua jimboni

Spread the love  MBUNGE wa Igunga, Nicholas Ngassa ameishukuru Serikali kwa utekelezaji...

Habari za Siasa

PIC yaishauri Serikali kuanzisha mfuko wa uwekezaji kusaidia mashirika ya umma

Spread the love  KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji...

error: Content is protected !!