July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais Karume ahofia vurugu Z’bar

Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume

Spread the love

RAIS Mstaafu wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume amesisitiza haja ya kulinda na kuendeleza amani iliyopo visiwani humo. Anaandika Mwandishi Wetu … (endelea).

Amesema, suala la amani si jambo la kufanyiwa mzaha bali ni jambo linalohitaji kulichukulia kwa umakini mkubwa ili kuinusuru Zanzibar kutorejea kwenye machafuko.

Dk. Karume ametoa nasaha hizo katika hafla ya futari maalum iliyoandaliwa na kamati ya msikiti wa “Masjid Imani” ulioko Mbweni, nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Amefahamisha kuwa, amani ni rasilimali muhimu ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hivyo haipaswi kufanyiwa mzaha, kwani iwapo amani ikitoweka, inaweza kuigharimu serikali na taifa kwa ujumla.

Akizungumzia kuhusu suala la umoja na mshikanao Dk. Karume amesema, umoja kwa Wazanzibari ni neema iliyotokana na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 na kwamba, lengo la mapinduzi hayo ni kuwaunganisha wananchi.

“Wazanzibari ni wamoja, ni kitu kimoja licha ya kuwa wametoka katika maeneo tofauti ya visiwa vya Unguja na Pemba,” amenasihi Dk. Karume.

Rais huyo Mstaafu wa Zanzibar amesema, umoja wa wazanzibari ni jambo la asili linalopaswa kuenziwa, licha ya kuwepo tofauti ndogo ndogo miongoni mwa wananchi.

Dk. Karume ameelezea kuridhishwa na hali ya amani na utulivu na kuiombea nchi iendelee kudumu katika hali hiyo wakati wote kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015.

Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema, dhamira ya kuendeleza umoja na mshikamano iko pale pale, licha ya kuwepo kasoro ndogo ndogo zilizoanza kujitokeza.

Amesema, kila mmoja ana wajibu wa kuendeleza umoja na kuwaunganisha wananchi, ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inabakia kuwa visiwa vya amani na utulivu.

Maalim Seif amewashauri wananchi kuendeleza utamaduni wa kualikana na kufutari pamoja, ili kuzidisha mapenzi miongoni mwao.

“Utamaduni wa kualikana katika futari ni mila na silka ya Zanzibari, hatuna budi kuzuendeleza silka hizi katika visiwa vyetu”, ameeleza Maalim Seif.

Ameishukuru kamati ya msikiti huo wa “Masjid Imani” kwa kuandaa futari hiyo na kuwakutanisha waislamu kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar, jambo ambalo limeleta faraja kwa waalikwa hao.

error: Content is protected !!