Spread the love

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezifariji familia ya rubani Adil Sultan Khamis na Ashraf Abdalla Juma Mabodi kutokana na ajali ya ndege iliyotokea hivi karibuni huko Visiwani Comoro. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Rais Dk. Mwinyi akiwa ameambatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi jana tarehe 6 Machi, 2022 walifika nyumbani kwa familia ya Adi Sultan Khamis huko Mbweni na kuifariji familia hiyo.

Pia ameisihi kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki wakati taarifa sahihi zikitafutwa za raia hao wa Tanzania pamoja na abiria waliokuwemo katika ndege hiyo aina ya Cessna Caravan 5HMZA.

Pia Rais Dk. Mwinyi alifika nyumbani kwa familia ya Rubani Ashraf Abdallah Juma Mabodi huko Chukwani kuifariji na kuisihi kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hichi wakati taarifa sahihi zikitafutwa juu ya tukio hilo.

Baba wa Rubani Asharaf, Dk. Abdallah Juma Mabodi alimueleza Rais Dk.Mwinyi juhudi zinazoendelea kuwatafuta marubani hao pamoja na abiria waliokuwemo katika ndege hiyo.

Aidha, familia hizo zilitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi pamoja na Mama Mariam Mwinyi kwa hatua walizozichukua za kwenda kuwafariji hasa katika kipindi hiki ambacho bado taarifa kamili hazijapatikana juu ya tukio hilo.

Tarehe 27 Februari, 2022 ndege ndogo aina ya Cessna Caravan 5HMZA ikiwa na abiria 14 wakiwemo marubani wa Tanzania wawili ilipotea katika rada kilomita 2.5 kabla ya kutua katika mji wa Fomboni, uliopo kisiwa cha Moheli ikitokea makao makuu ya kisiwa cha Moroni nchini Comoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *