October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Rais Dk. Mwinyi atoboa siri ndege za ATCL kupokewa Zanzibar

Spread the love

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Visiwani humo, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uamuzi wa mapokezi ya ndege mbili mpya za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufanyika Zanzibar, ni kielelezo cha juhudi za viongozi katika kuulinda na kuudumisha muungano. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea). 

Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo tarehe 8 Oktoba, 2021 Visiwani Zanzibar wakati akipokea ndege hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Amesema katika ndege zote zilizonunuliwa, zilipokewa jijini Dar es salaam na Mwanza lakini uamuzi wa sasa ni wa kihistoria kwani umelenga kuendeleza juhudi za viongozi wa Taifa katika kuendelea kuulinda fikra, mawazo na falsafa za waaasisi wake.

Amesema ATCL ambayo ilianzishwa mwaka 1977, sasa inamiliki ndege 11 kati ya hizo ni Bombardier Dash 8 Q4100, Bombardier CS300, Boeing 787 dream liner lakini lengo ni kuwezesha shirika hilo kuwa na ndege 16 ifikapo mwaka 2023.

“Haya ni mafanikio makubwa tukizingatia kwamba sekta ya usafiri wa anga, majini na nchi kavu ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa letu.

“Serikali zote mbili zimeahidi kuimarisha miundombinu kuwa ya kisasa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kuboresha kiwanja cha ndege Pemba ili kuwa kisasa,” amesema.

Pia ameuagiza uongozi wa ATCL kuendelea kubuni na kuongeza mikakati imara ya kutumia changamoto zilizotokana na janga la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19 kuwa fursa.

“Pia ili kuhimili ushindani mkubwa wa sekta ya usafiri wa anga, Shirika lifuate miongozo ya usalama na afya ya kimataifa.

“Licha ya idadi ya watanzania kukadiriwa kufikia milioni 60, bado idadi ndogo ya Watanzania wanatumia usafiri wa anga, ni kazi ya ATCL kuwashajihisha watumie usafiri wa ndege kwani kadiri tutakavyotumia bei itashuka na shirika kupata faida,” amesema.

Pamoja na mambo mengine amesema Serikali Zanzibar itaendelea kuibua masoko mapya ya utalii hasa mashariki ya kati na mbali kwani kukiwepo na ndege za safari za moja kwa moja, zitaimarisha sekta hizo.

Pia amesema Serikali Mapinduzi Zanzibar imepokea ombi lililotolewa na ATCL kuhusu uhitaji wa jengo la kupumzikia wateja wao kwenye uwanja cha ndege Amani.

Dk. HUssein Mwinyi, Rais wa Zanzibar

Aidha, Waziri mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mmoja wa viongozi waliohudhuria hafla hiyo amesema malengo ya ujio wa ndege hizo ni kuongeza safari za ndani na nje ili kukuza uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja.

Awali akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Rahma Kassim Ali; Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ndege hizo zimepewa majina ya Zanzibar na Tanzanite baada ya Rais Samia kuagiza ndege moja ipewe jina la Zanzibar.

Mbali na kuishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa maandalizi ya mapokezi ya ndege hizo amesema hiyo ni alama ya mshikamano katika kudumisha muungano wetu.

Amesema hivi karibuni ATCL itaanza kufanya safari za kwenda Pemba.

Aidha, akitoa taarifa kwa viongozi waalikwa na wageni katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema sasa shirika hilo linafanya safari za nje katika vituo vitano lakini hivi karibuni itaanza safari katika vituo cha Bujumbura, Guangzhou, Johannesburg, Lubumbashi, Nairobi na Ndola wakati maandalizi Kinshasa yanaendelea.

Amesema pia itaanza safari za Dar es salaam moja kwa moja kuelekea jiji la Lagos nchini Nigeria ikiwamo Dar es Salaam kuelekea Mumbai nchini India.

Amesema kwa kuwa shirika hilo limefanikiwa kuongezeka umiliki wa soko kutoka asilimia 2.5 hadi asilimia 73, sasa limefanikiwa kuchangia pato la taifa kutokana na kodi Sh bilioni 57.63.

“Tunashukuru Serikali imetuwezesha kuajiri watumishi kutoka 171 hadi 644 kati yao marubani ni 11 hadi 100 ndio maana tumeona ndege hizi zimeletwa Zanzibar na vijana wa Kizanzibar waliozaliwa Pemba Tanzania Bara.

Akitaja sifa za ndege hizo zilizotengenezwa nchini Canada, Mkurugenzi huyo alisema katika ndege hizo mbili kila mojawapo ina uwezo wa kubeba abiria 132.

Pia kila moja ina uwezo wa kuruka kwa saa 6 bila kutua, ina mifumo ya kuwasaidia marubani wakati wa kuruka na kutua na aina ya viti vyake ni vya tofauti ambavyo unaweza kuvibadilisha ukaaji.

“Ndege hizo pia zina mifumo ya burudani ndani yake inayojumuisha burudani kwa ajili ya watoto, sinema, vichekesho na usikilizaji wa muziki wa aina mbalimbali na mitandao ya intaneti,” amesema.

error: Content is protected !!