Saturday , 20 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Rais Burkina Faso ahukumiwa maisha kwa kumuua Sankara
Kimataifa

Rais Burkina Faso ahukumiwa maisha kwa kumuua Sankara

Spread the love

RAIS wa zamani wa Burkina Faso, Blaise Compaoré, amehukumiwa leo Jumatano tarehe 6 Aprili, 2022 kifungo cha maisha jela kwa kushiriki katika mauaji ya mtangulizi wake Thomas Sankara. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Sanka aliuawa pamoja na wasaidizi wake 12 katika mapinduzi ya mwaka 1987 yaliyomuweka madarakani Compaore.

Mahakama ya kijeshi ya jijini Ouagadougou pia imehukumu kifungo cha maisha jela Kamanda wa kikosi chake cha ulinzi, Hyacinthe Kafando na Jenerali Gilbert Diendéré aliyekuwa mmoja wa viongozi wa jeshi wakati wa mapinduzi ya mwaka 1987.

Blaise Compaoré, ambaye yuko uhamishoni tangu mwaka 2014 nchini Ivory Coast na Hyacinthe Kafando ambaye yuko mafichoni tangu mwaka 2016, hawakuhudhuria kesi hii iliyoanza miezi sita iliyopita.

Ilichukua miaka kadhaa ya uchunguzi, kesi ambayo walihusishwa mashahidi zaidi ya 110 na kesi hii imesikilizwa kwa miezi 6 ya hadi leo.

Compaore ambaye alikuwa Rais wa taifa hilo kuanzia tarehe 15 Oktoba, 1987 hadi tarehe 31 Oktoba, 2014 ni miongoni mwa washtakiwa 14 wa mauaji hayo.

TUHUMA ZA RAIS COMPAORE

Thomas Sankara

 

Rais Compaore alikuwa mshukiwa muhimu wa mauaji hayo na ndiye alirithi nafasi ya urais baada ya mapinduzi yaliyosababisha kifo cha swahiba wake Rais Sankara.

Kwa mujibu wa nyaraka za jeshi zilizogunduliwa na Shirika la Habari la Ufaransa AFP, Compaore alituhumiwa kwa makosa ya kushiriki mauaji, kuhujumu usalama wa taifa na kuficha maiti ya Sankara.

USWAHIBA WA SANKARA NA COMPAORE

Historia inamtambua Thomas Sankara kama ‘Che guevara ama Fidel Castro’ wa Afrika. Hii ni kutokana na maono yake katika uongozi na fikra zake kudumu mpaka sasa hasa miongoni mwa wafuasi wake.

Lakini pia alikuwa ni kiongozi mashuhuri wa siasa Barani Afrika katika karne ya 20 akifananishwa na Nelson Mandela (Afrika Kusini) na Patrice Lumumba (Congo DRC).

Agosti mwaka 1983, vijana wawili, makapteni wa jeshi na wanamapinduzi, Kapteni Thomas Sankara na Kapteni Blaise Compaore, waliipindua Serikali ya Rais wa wakati huo katika nchi iliyokuwa ikijulikana kama Upper volta. Rais huyu aliitwa Baptiste Ouedraogo.

Vijana hawa wakiwa katika fikra za Karl Max, wakiwa na ndoto nyingi za kuijenga Upper volta, walibadili kabisa historia ya taifa hilo, walibadili jina la nchi na kuitwa Burkina faso, maana yake ‘nchi ya watu waaminifu’.

Mara nyingi Sankara alikuwa anatumia baiskeli kutembelea vijiji kuhimiza maendeleo, wakati pacha wake yaani Compaore wakiwa kama pete na kidole.

Urafiki wa makapteni hawa wa jeshi, ulikuwa mkubwa kiasi kwamba wakati wanausalama walipomwambia Sankara kuwa Compaore ana mpango wa kumpindua na kumuua, aliwajibu kuwa Compaore asingeweza kufanya hivyo, labda mtu mwingine.

Compaore alikutana na Sankara mwaka 1976 katika mafunzo ya kijeshi nchini Morocco na hapo walianza urafiki wao uliokuwa wazi kwa karibu watu wote waliokuwa wakiwafahamu nchini Burkina Fasso na nchi jirani.

Sankara alikuwa akiwaeleza wanausalama wake kuwa, hata kama Compaore angetaka kufanya hayo, hakuna wa kumzuia.

Ni wazi kuwa Kapteni Sankara alikuwa karibu sana na Compaore, kwa kiasi ambacho Compaore alikuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya Sankara.

Kama ilivyotabiriwa na watu wengi wa karibu wa Sankara, Compaore aliongoza mapinduzi yaliyosababisha kifo cha Sankara mwaka 1987, na yeye mwenyewe (Compaore), huku akishuhudia rafiki yake kipenzi Sankara akiuawa, akawa ndiye mrithi wa kiti cha Urais wa iliyokuwa Upper Volta baadaye Burkina Fasso.

THOMAS SANKARA NI NANI?

Sankara alizaliwa tarehe 12 Desemba, 1949 mjini Yoko katika nchi iliyokuwa ikiitwa Upper Volta (Volta ya juu) na kuuawa tarehe 15 Oktoba, 1987 na wanajeshi wenzake wakiongozwa na anayedaiwa kuwa rafiki yake Compaore katika mapigano ya usaliti yaliyotokea Mjini Ouagadougou akiwa katika kikao cha utendaji wa kazi.

Kuna nyakati ambazo Compaore aliwahi kunena kwa kinywa chake katika shirika la kutetea haki za Binadamu duniani kwamba ‘kifo cha Thomas Sankara kilikuwa ni ajali tu’.

Mwaka 1981, Sankara alikuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya kijeshi ya Rais wa wakati huo wa Burkinabe ya zamani (Upper Volta), Dk. Jean Baptiste Major.

Baadaye aliteuliwa kuwa waziri mkuu kwa kipindi cha kuanzia Januari 1983 mpaka Mei alipokamatwa na kutiwa mbaroni na serikali ya Rais Major Jean Baptiste kutokana na msimamo wake juu ya ukombozi kwa watu wote wa Volta ya Juu na kupendelea mapinduzi ya kijamaa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Kimataifa

Majaji kuamua hatima ya Zuma leo

Spread the loveMajaji nchini Afrika Kusini leo Jumanne wataamua ikiwa rais wa...

Habari za SiasaKimataifa

Spika Afrika Kusini ajiuzulu kwa tuhuma za rushwa

Spread the loveSpika wa Bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula ametangaza kujiuzulu...

Habari MchanganyikoKimataifa

Tetemeko la ardhi laua 7, lajeruhi 800 Taiwan

Spread the loveWatu wapatao saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 800...

error: Content is protected !!