January 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rais atulie, hajui sheria – Mallya

Spread the love

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unashikilia msimamo wa kuelekeza wananchi kubaki vituoni wakishapiga kura na kumtafadhalisha Rais Jakaya Kikwete asiwatishe kwa sababu hilo ni suala la sheria ambayo “si taaluma yake.” Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mallya amesema wanaendelea kushikilia msimamo huo kwa kuzingatia Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 kupitia kifungu Na. 104.

Mallya amesema kifungu hicho kinakataza watu kuwepo kwenye kituo cha kupiga kura isipokuwa nje ya mita 200 ya kituo husika.

Rais Kikwete akihutubia wananchi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, mjini Dodoma jana, alisema ni marufuku watu kukaa karibu na vituo na kuonya kuwa atakayevunja sheria hatovumiliwa ili kuepusha demokrasia kutekwa nyara.

Tamko la Rais Kikwete limeimarisha agizo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi lililotaka watu waende nyumbani baada ya kupiga kura na agizo likatiliwa nguvu na Jeshi la Polisi lililokataza watu kuwepo kwenye maeneo ya vituo ili kuzuia uchochezi wa vurugu siku ya uchaguzi.

Lakini, katika kuonesha hofu inayojengwa na Serikali na Polisi kuhusu suala la wananchi kuwa macho dhidi ya wizi wa kura, Mallya amesema vitisho vya Rais Kikwete vipuuzwe kwa kuwa “yeye si kazi yake na wala hajui sheria za uchaguzi.”

“Tunaomba wananchi wote wapenda mabadiliko baada ya kupiga kura wasiondoke eneo la tukio. Sawa mawakala wanakazi yao, lakini pia wananchi wanaweza kutoa msaada wa kuripoti vitendo vyote viovu vitakavyofanyika baada ya upigaji kura,” amesema Mallya.

Amesema iwapo kutatokea vurugu nje ya vituo vya uchaguzi, Rais Kikwete atabeba dhamana kwa sababu, “wananchi wanayo haki ya kusimamia kura zao dhidi ya kuibwa kama inavyotokea katika uchaguzi ambapo wagombea wa CCM hutangazwa washindi kwa kura za wizi.”

Akasisitiza kwamba Rais na wakuu wa Polisi watawajibika pakitokea vurugu kwa sababu ya hatua ya wananchi kulinda kura zao.

“Vurugu zikitokea, ni wao pamoja na wasimamizi wa uchaguzi ndio watakaoshitakiwa katika Mahakama za Kimataifa hasa kwa vile waangalizi wa uchaguzi kutoka ndani ya nje wapo wanaona kila kitu,” amesema.

“Rais Kikwete hana haki wala nguvu ya kuingilia kazi za Tume ya Uchaguzi kwani hana uzoefu wa sheria, asitake kuvuruga amani ya wananchi wapenda maendeleo kwa kuwa anamaliza muda wake,” amesema Mallya ambaye alizungumza akiwa ukumbi wa mikutano Millenium Tower, Makumbusho jijini Dar es Salaam.

error: Content is protected !!