RAIS wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Daktari Akinwumi Adesina, amezuru katika kaburi la aliyekuwa Rais wa Tanzania wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, lililoko wilayani Chato, Mkoa wa Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita…(endelea).
Dk. Adesina amelitembelea kaburi hilo jana tarehe 10 Februari 2022, katika ziara yake ya siku moja yenye lengo la kutoa salamu za pole kwa familia ya Hayati Magufuli, ambapo alipokelewa na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Chato, Wilson Shimo.
Rais huyo wa AfDB alisema ziara yake hiyo inatokana na urafiki mkubwa, kati yake na Hayati Magufuli.
“Rais Magufuli alikuwa mfano mzuri kwa viongozi barani Afrika, aliwapenda Watanzania na Waafrika wote, kwa moyo wake wote,” alisema Dk. Adesina.
Dk. Adesina alimshukuru Rais Samia kwa kumruhusu yeye na ujumbe wake kuzuru katika kaburi hilo, huku akisema Tanzania iko kwenye mikono salama chini yake, ambaye anaendeleza mazuri yaliyoachwa na Hayati Magufuli.
Hayati Magufuli aliyeiongoza Tanzania kwa miaka mitano na miezi kadhaa mfululizo (2015 hadi 2021), alifariki dunia tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho jijini Dar es Salaam, alikokuwa anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo.
Mwili wake ulizikwa kijijini kwao Chato mkoani Geita, tarehe 26 Machi mwaka jana.
Leave a comment