May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Raila Odinga: Nimempoteza rafiki, Uingereza yashitushwa na kifo cha JPM

Spread the love

 

WAZIRI mkuu mstaafu wa Kenya na Kiongozi wa Upinzani nchini humo, Raila Odinga ametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani, wakati huu wa msiba wa kuondokewa na rais wake, John Pombe Magufuli. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Raila, mtoto wa aliyekuwa Makamu wa Rais wa kwanza wa taifa hilo, Jaramogi Oginga Odinga, ameeleza kuwa njia pekee ya Tanzania kusonga mbele ni kudumisha umoja na mshikamo, vitu ambavyo ndiyo tunu iliyoachwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema, “katika kipindi hiki cha msiba na ugatuaji wa madaraka ya urais, baada ya Rais Magufuli kufariki dunia, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho ndicho marehemu anatoka, kinapaswa kufuata misingi iliyoasisiwa na Mwalimu ili kudumisha amani katika taifa.

Rais Magufuli alifariki dunia jana Jumatano, majira ya saa 12 jioni, katika hospitali ya Mzena, Makumbusho, jijini Dar es Salaam.

Taarifa za Rais Magufuli kufariki dunia, zilitolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri, Samia Suluhu Hassani.

Magufuli alilazwa katika hospitali hiyo, akipatiwa matibabu baada ya kuugua maradhi ya moyo.

Raia ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Rais Magufuli amesema, mchakato wa kukabidhiana madaraka, unapaswa kutekezwa kwa amani na kwa kuzingatia matakwa ya Katiba.

Amesema, Rais Magufuli atakumbukwa kwa mchango wake wa kulipasha taifa hilo,  katika jumuiya za kimataifa.

“Kwa watu wa Tanzania na CCM cha Mwalimu Julius Nyerere, tunaomboleza pamoja nanyi, katika kusherehekea maisha ya Magufuli hapa duniani. Tunatambua mchango wake katika kuipandisha Tanzania katika ukanda na jumuiya za kimataifa,” ameeleza mwanasiasa huyu nguli katika eneo la Afrika Mashariki.

Amesema, kifo cha Magufuli kimemuachia pigo, kwa kuwa alikuwa rafiki yake wa karibu katika kipindi cha shida na raha.

“Ni huzuni kubwa kwamba nimefahamu kifo cha rafiki yangu, Rais John Magufuli wa Tanzania. Magufuli na familia yake tulikuwa marafiki wa karibu kwa muda mrefu. Alikuwa upande wangu nilipokuwa katika kipindi kigumu na cha maumivu.

“Kwa zaidi ya miaka kadhaa, tulifanya kazi pamoja katika masuala ya miundombinu kwenye maeneo ya Afrika Mashariki. Kwa niaba ya familia yangu na ODM natuma salamu za pole kwa familia ya Rais Magufuli na watu wa Tanzania,” amesema Odinga.

Naye Dk. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar, ameeleza kuwa amepokea taarifa za kifo cha Dk. Magufuli, kwa masikitiko makubwa.

Amesema, “tumempoteza rais. Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi (Amin).”

Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, ameisikitishwa na kifo cha Rais Magufuli. Akiandika katika ukurasa wake wa twitter, Johnson amesema, “nimesikitika kusikia kwamba Rais wa Tanzania, John Magufuli ameaga dunia,   mawazo yangu yako kwa wapendwa wake na watu wa Tanzania.”

Rais wa Somalia, Mohamed Farmaajo ametuma salamu za rambirambi, kufuatia kifo hicho.

Amesema, “kwa niaba yangu na kwa niaba ya serikali ya taifa la Somalia, ningependa kuwasilisha rambirambi zetu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  akumpoteza kiongozi wao, Rais John Magufuli.”

Amesema, “tunalitakia taifa zima na serikali subra na utulivu katika kipindi hiki cha maombolezo.”

error: Content is protected !!