August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Rafu za CCM zawaliza CUF

Spread the love

RAFU zinazofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zinawaumiza viongozi, wananchi na wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), anaandika Happyness Lidwino.

Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu wa CUF amekutana na waandishi wa habari leo katika Ofisi Kuu ya chama hicho, Buguruni, jijini Dar es Salaam ambapo amesema, CCM na washirika wake wanatesa wananchi hususan wafuasi wa chama hicho.

Amesema, serikali kupitia Jeshi la Polisi limekuwa likikamata wafuasi wake pamoja na viongozi huku wengine wakiwajeruhi kwa kipigo kutokana na kusimamia kauli ya kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliotangazwa na ZEC kufanyika tarehe Machi 20 mwaka huu visiwani humo.

“Zaidi ya wafuasi 60 na viongozi wetu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kudaiwa kufanya fujo, ofisi za CUF zikichomwa moto na mali za chama zinaharibiwa vibaya na mzombi,” amesema na kuongeza;

“Kundi hilo la mazombi limekuwa likiwavamia viongozi wa CUF na kuwapiga, licha ya matukio hayo kuripotiwa polisi, wamekuwa wakikanusha kwamba kundi hilo halipo.”

Kwa mujibu wa Sakaya, hadi sasa viongozi waliokamatwa ni pamoja na, Eddy Liamy mwanamikakati ya ushindi CUF; Nassoro Mazrui, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar; Mahomoud Mahinda, Katibu Mtendaji JUVICUF; Abeid Hamis Bakari, Mkuu wa Idara ya Habari na Uenezi na Hamad Masoud, Mkurugenzi wa Habari CUF.

Amesema, kutokana na hali hiyo, kuna kila aina ya uvunjifu wa haki za binadamu visiwani humo na kwamba, polisi wamekuwa wakivamia ofisi za chama hicho wakiwa na silaha nzito pia vifaru vya kijeshi na kuwatishia wananchi kwa kisingizio cha kulinda amani.

‘’Hiyo yote ni mipango ya CCM ya kutaka kuwanyanyasa wananchi hata wasiokuwa wafuasi Zanzibar hakuna vita, CUF tulijitoa kwa amani, hakuna mwanachama aliyeandamana lakini tunashangazwa na vifaa vya vita vinavyoletwa.

“Tulitegemea baada ya sisi kujitoa, CCM ingefurahi ili ijitangaze ushindi kwa amani kwani ndicho wanachoking’ang’ania. Sasa wanahitaji nini kutoka kwa wananchi?

“CUF wapop kimya lakini kila tukio wanasingiziwa wao licha ya CCM kuonekana wazi kuanzisha fujo,’’ amesema Sakaya.

Sakaya amesema, kinachoendelea Zanzibar hivi sasa ni jitihada za CCM kwa kushirikiana na serikali kuwalazimisha wananchi kushiriki uchaguzi haramu.

Pia amesema, CUF wanashangazwa na hatua ya Rais John Magufuli kuruhusu vifaa vya kivita kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibari kwa ajili ya kujiandaa na vita wakati alisema hatoshiriki kwa chochote na uchaguzi huo.

“Kinachofanywa na Magufuli ni kama maandalizi ya vita kana kwamba wanajua kitakachoenda kutokea. Ingekuwa nyema muda huu asimamie suala la usalama na kudhibiti maovu yanyoendelea Zanzibari,’’ amesema Sakaya.

Ameeleza masikitiko yake kuhusu kauli ya Charles Kitwanga, Waziri wa Mambo ya Ndani wakati akinzungumza na vyombo vya habari ambapo alisema Zanzibar hakuna watu wanaopigwa.

“Ni hatari sana kwa waziri kupotosha umma kwa kusema uongo hadharani na kuficha ukweli kwa kile kinachoendelea Zanzibar. Ina maana waziri hasomi hata magazeti au hata kusikiliza radio au kuangalia TV hadi asione kinachoendelea huko?. Kauli yake inawapa viburi wanaofanya maovu Zanzibar,” amesema.

error: Content is protected !!