Wednesday , 6 December 2023
Home Gazeti Makala & Uchambuzi RA Mengi: Tasnia ya habari itakukumbuka
Makala & Uchambuzi

RA Mengi: Tasnia ya habari itakukumbuka

Spread the love

NI matarajio yangu kuwa siku historia ya vyombo vya habari katika Tanzania katika robo karne itakayopita itakapoandikwa, basiwaandishi wa historia hiyo watampa nafasi pekee na maalum Reginald Abraham Mengi (RAM), Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia Alhamisi, wiki hii, kule Dubai, Mashariki ya Kati. Anaandika Salva Rweyemamu … (endelea).

Nianze na jambo ambalo pengine siyo muhimu. Lakini ni vizuri lieleweka kwa sababu litasaidia kuweka msingi wa ninayotaka kuyasema kuhusu Marehemu Mengi. Nia yangu ni kukwepa mtego wa kuongozwa na unafiki, kama ilivyo desturi ya tulio wengi katika nchi yetu, wakati mtu anapofariki.

Uhusiano wangu na Mzee Mengi ulitawaliwa na vipindi vifupi vya urafiki, lakini zaidi na vipindi virefu vya mivutano, na mpaka anaaga dunia, nilikuwa sijawasiliana naye kwa kipindi kirefu, kwa sababu mara ya mwisho uhusiano wetu ulikuwa mbaya.

Nilikutana na Mzee Mengi, ana kwa ana, kwa mara ya kwanza, mwaka 1991, kwenye hafla moja kwenye iliyokuwa Hoteli ya Forodhani (sasa Makahama ya Rufani) mjini Dar Es Salaam. Nilikuwa nimejerea nchini kutoka masomoni Uingereza, na katikati ya tafrija hiyo, alinijia mwenyewe, na akajitambulisha, ingawa dhahiri nilikuwa namfahamu. Wakati huo, alikuwa tayari ameanzisha IPP. Lakini kubwa zaidi wakati huo, alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers (TSN).

Baada ya kujitambulisha, alinieleza kuwa alikuwa amesikia habari zangu kutoka kwa baadhi ya Watanzania niliokuwa nao Uingereza. Hili halikunishangaza, kwa sababu wanafunzi wengi walinijua vzuri kwa sababu nilikuwa Mwenyekiti wao wa Chama cha Wanafunzi wa Tanzania katika Uingereza na Ireland. Piaalinialika nipate muda nimtembelee ofisini kwake katika Jengo la IPS, katikati ya Jiji la Dar Es Salaam.

Ofisini kwake, aliniambia mambo kadhaa. Kwanza, kuwaalikuwa na nia ya kuanzisha magazeti. Pili, aliniambia kuwa mimi nilikuwa mtu wa kwanza kuambiwa habari hizo, akiomba mazungumzo yetu yabakie siri kwa muda. Tatu, akaniomba niwe mhaririri wa kwanza wa magazeti hayo. Nne, akaniomba nimwandilia, kwa mhutasari kabisa, namna ya kufanikisha azma yake hiyo. Tano na mwisho, akaniomba nianze “kutazamatazama” watu ambao wangefaa kushiriki katika Mradi huo kama yeye alivyokuwa anauita.

Kazi hiyo niliifanya vizuri nadhani, na vilifuatia vikao vingine vingi tu baina ya Mzee Mengi, tukimwita “Mwenyekiti” na baadhi ya watu ambao niliwapendekeza kwake na yeye akawakubali. Sitawataja kwa sasa kwa sababu hapa siyo mahala pake na hasa kwa sababu wote walikuwa ni waajiwa ama wa Serikali (Maelezo) ama kwenye magazeti ya wakati huo ya Chama cha CCM na Serikali.Wale ambao Mwenyezi Mungu amewajalia kubakia hai, wanajijua wenyewe.

La msingi ni kwamba, hatimaye, sikufanikiwa kuwa mhariri mwanzilishi wa magazeti ya Mzee Mengi, kama tulivyokuwa tumepanga. Sababu za hili nazo tuziache kwa sasa. Zitazungumzwa siku nyingine, mahali pengine na wakati mwafaka. Kubwa la kusema hapa ni kwamba badala ya kuwa mhariri mwanzilishi wa magazeti ya Mzee Mengi, nikawa mmoja wa waanzilishi wa Gazeti la Dimba, gazeti mama la michezo katika Tanzania na chimbuko lakile kilichokuja kujulikana baadaye kama Habari Corporation na magazeti yake.

Uamuzi wangu wa kutokujinga na himaya ya Mzee Mengi, pamoja na imani kubwa aliyokuwa amenionyesha, haukumfurahisha Mzee. Alikasirika. Hata hivyo, uhusiano wetu ulikuja kurudia hali yake nzuri baadaye wakati nikiwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), tawi la Tanzania, na baadaye kwenye Kanda ya Kusini Mwa Afrika.

Uhusiano huo ulikua zaidi wakati nilipokuwa mjumbe wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), chama ambacho Mzee Mengi alikiongoza tokea kuanzishwa kwake hadi umauti ulipomfika. Baadaye, wakati wa msiba wa mwananguBrian, Mzee Mengi alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kabisa kunifariji kwa kila hali na alishiriki kikamilifu katika mazishi.

Uhusiano wangu na Mzee Mengi uliharibika tena mwaka 1996, wakati gazeti la Mtanzania ambalo nilikuwa Mhariri Mtendaji wake,lilipoandika habari za kuwa alikuwa mdaiwa mkuu na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Huo ulikuwa wakati wa misukosuko mikubwa ya kubinafsishwa kwa Benki hiyo. Na wala hakuficha hasira zake kuhusu kuandikwa kwa habari hiyo. Alitufungulia kesi ya madai, akitaka kulipwa mabilioni ya fedha, kwa kuvunjiwa heshima na hadhi.

Hatukuishia hapo. Uhusiano wangu na Mzee Mengi ulivurugika mno wakati nilipotumikia katika nafasi ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu. Kwa sababu ambazo, binafsi sikupata kuzijua vizuri ingawa naamini zilikuwa za uongo, uhusiano wangu na Mzee Mengi ulifikia kiasi cha yeye kukataa kunipa mkono wakati wa hafla moja ya kitaifa pale Ikulu.

Na kwa maneno ya kuambiwa tu, alifikia mahali pa kunipigia simu siku moja, na kunishutumu kwa kuwa kizabizabina, ambaye nilikuwa nasambaza maneno ya kumsema yeye kwa watu. Lakini baya zaidi, akanishutumu kuwa nilikuwa kwenye mpango wa kutaka kumwuua. Kwa nini sikupata kujua. Sijui kwa sababu siamini hata kama binafsi nina hata uwezo wa kumwua inzi wacha mtu maarufu katika jamii kama Mzee Mengi.

Mpaka anaaga dunia hatujapata nafasi ya kuzungumza, ana kwa ana, kuhusu shutuma hizo dhidi yangu, ukiondoa hatua yangu ya kujiunga naye katika ibada ya kumwaga mke wake wa zamani, Marehemu Mercy Mengi.

Lakini hata kama uhusiano wetu ulikuwa wa kupanda na kushuka milima kwa miaka yote 28 tuliyojuana, bado kwangu mimi, na naamini kwa mamilioni ya Watanzania na hasa Waafrika wa nchi hii, Mzee Reginald Abraham Mengi alikuwa mtu muhimu sana. Ameonyesha njia na kufungua milango kwa mamilioni ya watu,hasa katika eneo la uthubutu wa Waafrika kufanya biashara.

Aidha, uhusiano huo haukupata kubadilisha maoni na msimamo wangu kuhusu mchango wake mkubwa, tena mkubwamno, pengine kuliko wa Mtanzania mwingine yoyote, katika maendeleo ya tasni ya habari katika nchi yetu, kwa hakika katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki.

Kwa maoni yangu, siamini kama kuna mtu mwingine amechangia zaidi tasnia hii kama alivyofanya Mzee Mengi. Siyokama mwandishi wa habari, kwa sababu hakuwa mwandishi wa habari. Bali kama mfanyabiashara na mchumi halisi wa vyombo vya habari. Alikuwa na uthutubu wa ajabu sana, dhamira na maono ya kuhusudiwa katika eneo hili.

Hakuiona tasnia ya habari kama eneo la kuchoma na kupoteza fedha zake, kama kama walivyo wafanya biashara wengine. Bali aliiona tasni kama dimba mwafaka la kuwahabarisha, kuwaelimisha na kuwaburudisha Watanzania na wana-Afrika Mashariki.

Kwetu sisi wakati huo tukiwa Habari Corporation, Mzee Mengi kupitia magazeti yake ya IPP alikuwa mshindani mkubwa.Mshindani, kwa maana ya magazeti tu, siyo vinginevyo, kwa kutilia maanani kuwa sisi hatukuwa na vyombo vingine vya habari na yeye alikuwa na raslimali nyingi zaidi kifedha na kibiashara. Lakini alikuwa ni mshindani hodari ambaye mchango wake ni lazima tuuenzi. Sura ya tasnia ya habari ya Tanzania ya sasa ni matokeo ya mchango wake mkubwa. Tasnia isingekuwa kama ilivyo sasa bila mchango mkubwa wa Mzee Mengi. Huo ndio ukweli usiopingika – tupende, tusipende.

Nataka kusema jambo ambalo linaweza kuwa lenye utata. Lakini nitalisema, wacha lizae utata. Kama iko siku historia ya vyombo vya habari katika Tanzania, ikiandikwa kwa haki na wanahistoria wanaojali ukweli, itaonyesha kuwa katika miaka 30 iliyopita ya kuchipuka upya kwa vyombo vya habari binafsi, na kuchanua kwa uhuru wa habari katika Tanzania, makundi matatu yalitoa mchango wa aina pekee katika hali hiyo na katika kukua kwa tasnia ya habari.

Kundi la kwanza ni la IPP likisukubwa na dhamira na utashi pamoja na raslimali kubwa za Mzee Mengi, Habari Corporation ikisukubwa na uthubutu na kiwango cha juu kabisa cha weledi na taaluma, na Business Times ikiongozwa na ubunifu mkubwa wa Marehemu Richard Nyaulawa na Rashid Mbughuni ambao kwa pamoja walianzisha gazeti la kwanza la kila siku la Kiswahili la Majira katika kipindi cha baada ya kurudishwa kwa uhuru wa kujieleza na vyama vingi katika Tanzania.

Yapo makundi mengine mwili muhimu yaliyochangia na yanaendelea kuchangia, kwa kiasi kikubwa, maendeleo ya tasnia katika kipindi hicho. Kuna Kampuni ya Mwananchi Communications ya Dar Es Salaam na kuna Sahara Communications ya Mwanza. Haya yamechangia kwa namna ya pekee pia. Lakini historia yao ni tofauti kidogo na makundi yale matatu yaliyotajwa hapo juu.

Mzee Mengi alikuwa Mtanzania wa kwanza kuwawezesha watu wengi kupata matangazo mbadala ya redio wakati alipoanzisha Radio One na ikaanza kutoa matangazo ya ushindani, kwa mara ya kwanza, na redio za Serikali za Redio Tanzania na Sauti ya Tanzania, Zanzibar ambazo baadaye zikuja kubadili majina na kuitwa Tanzania Broadcasting Corporation (TBC) na Zanzibar Broadcasting Corporation (ZBC). Redio nyingine binafsi nchini zilifuata nyayo tu za Mzee Mengi na Radio One.

Sikatai, kuwa kabla ya Redio One, ilikuwepo redio ndogo binafsi ya Sauti ya Injili, ikitangaza kutoka pale Moshi, lakini hii ilikuwa redio iliyowafikia watu wachache kwa sababu ya maudhi yake ya dini na ya madhehebu ya Kilutheri, na hata mipaka ya mapokeo yake. Lakini kwa maana ya broadcasting, yaani kutupa wavu mpana zaidi wa matangazo yanayorushwa na mawimbi kufikia watu wengi kwa wakati mmoja bila mtu yoyote kupoteza ubora na maudhi ya matangazo yenyewe, mbali ya Serikali, Mzee Mengi alikuwa kinara katika nchi hii. Wengine wote wanaotamba leo walifuata nyayo zake kama nilivyoeleza hapo juu.

Mzee Mengi alikuwa Mtanzania wa kwanza kuanzisha televisheni binafsi nchini, Independent Television (ITV). Kweli, hata katika eneo hili, Tanzania tayari ilikuwa na televisheni, Television Zanzibar (TVZ). Hii nayo ina historia yake muhimu. Ilikuwa televisheni ya kwanza ya rangi kuanzishwa katika Bara la Afrika na mzee mwingine mwenye maoni makali, Mzee Abeid Amaan Karume, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Muasisi wa Muungano wa Tanzania. Lakini hii ilikuwa televisheni ya Serikali. Na isitoshe, matangazo yake yalikuwa hayasambai nchi nzima kiasi cha yalivyokuja kuwa matangazo ya ITV.

Alikuwa ni Mzee Mengi ambaye kwa kupitia ITV aliwawezesha mamilioni ya wapenzi wa michezo wa Tanzania, na hasa wapenzi wa mchezo wa mpira wa miguu, ama soka, kuona kwa urahisi kabisa, matangazo ya mpira bila malipo ya kutisha kama ya vyombo vingine, mradi tu mtu alikuwa na uwezo wa kununua seti ya televisheni, tena wakati huo hakuna vingamuzi na masharti mengine ya sasa. ITV ilikuwa televisheni ya kweli ya umma – free to air- hata kama haikuwa na umiliki wa umma.

Walikuwepo wakati huo watakumbuka jinsi Watanzania walivyoweza, kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, kuona Fainali za Kombe la Soka la Dunia mwaka 1994 moja kwa moja kutoka kule Marekani, majumbani kwao na vyumbani mwao kupitia televisheni ya ITV.

Mzee Mengi alikuwa Mtanzania wa kwanza, na mpaka mauti yanamfikia anabakia Mtanzania pekee, kuwa na uthubutu wa kuanzisha na kumiliki vyombo vya habari nje ya Tanzania, katika masoko magumu kama vile Uganda, na hasa Kenya.

Siasa za kuanzisha chombo cha habari katika nchi yoyote, iliyoendelea ama inayoendelea, ni ngumu. Chombo cha habari ni uwanja (platform) wa kusambaza utamaduni na ni nguvu ya uongozi. Ni tofauti na kuanzisha kampuni ya kuuza matofaliambayo mwekezaji anaweza kuianzisha katika nchi yeyote kwa urahisi kabisa. Kwamba aliweza kupata liseni na vibali vya kufungua redio Uganda, na hasa Kenya, inayolinda sana soko lake kwa kila bidhaa, siyo jambo dogo wala la mchezo, hata kidogo. Ni jambo kubwa sana.

Mzee Mengi hakuwa mwanzilishi katika eneo la magazeti. Wapo wengi waliomtangulia katika historia ya nchi yetu, wawe binafsi ama umma ama hata mashirika ya dini. Lakini himaya yake ya magazeti, ambayo wakati mmoja ilikuwa na magazeti manane, imetoa ajira kwa mamia ya watu, Watanzania na wasiokuwa Watanzania, kuliko kampuni nyingine yoyote ya magazeti na vyombo vingine vya habari hapa nchini. Huo, siyo mchango mdogo, wala wa kubeza. Kwa hakika ni lazima liwe jambo la kutia hofu, kwa hata kufikiria tu, nini kinaweza kutokea kwa himaya hiyo baada ya kifo cha ghafla cha Mzee wetu huyo.

Jambo jingine muhimu ni kwamba uthubutu huo wa Mzee Mengi, kuingia katika umiliki wa vyombo binafsi vya habari uchukuliwe katika mazingira halisi ya wakati huo. Yapo mambo kadhaa, yalikuwa bado ya msingi kabisa – dominant paradigm- wakati anaingia katika tsni ya habari.

Moja, ni kwamba katika miaka hiyo ya mwanzoni mwa 1990, sekta binafsi ilikuwa bado inaonekana adui wa umma na nchi. Kasumba na chuki dhidi ya ubepari, utajiri na miliki binafsi ya mali vilikuwa bado vikali mno miongoni mwa Watanzania wengi, wakiwemo watawala wa Serikali na wanasiasa wengine. Ubepari ulikuwa ni unyama. Na hata leo, miaka 30 baadaye, na juhudi kubwa mno za tawala kadhaa, bado hatuwezi kusema, kwa uhakika,kuwa kasumba hiyo imeisha kabisa. Pengine inaibuka tena leo, kwa kasi zaidi, kuliko wakati mwingine wowote katika miaka 30 iliyopita.

Pili, ni kwamba katika miaka hiyo vile vile uhuru wa mambo mengi ulikuwa ni jambo la nadra sana. Siyo kuwa hapakuwepo na uhuru. Kweli ulikuwepo. Jambo kubwa lilikuwa ni nani alikuwa nahaki ya kufurahia na kutumia uhuru huo. Uhuru wa vyombo vya habari na hasa vyombo vya habari binafsi lilikuwa jambo gumu sana na lisilofikirika kwa watu wengi.

Kuandika ama kutangaza mambo kwa uwazi na hasa yaliyowaudhi baadhi ya wenye madaraka, nguvu na mamlaka,lilikuwa jambo lisilifikirika na gumu sana. Na wakati mwingine la hatari. Na hapa, lazima tuseme kuwa uhuru huu siyo dhidi ya watu wa Serikalini tu, ama wenye nguvu ya dola, kwa sababu watu wengi wanauona uhuru wa vyombo vya habari kama mapambano dhidi yaSerikali tu. Kwa hakika, dhana ya uhuru wa habari ni pana zaidi kushirikisha maeneo mengi tu ya madaraka yakiwemo hata wakubwa wenye fedha na matajiri, viongozi wa kibiashara na kidini.Unaandika vipi jambo la kumwuudhi ama hata kumsema shekh maarufu, ama askofu ama kardinali, hata kama kinachoandikwa ni kweli?

Isitoshe, naamini kuwa kwa Mzee Mengi kazi ya kuweka uwiano kati ya kuendesha biashara ya habari, ambayo ni vigumu kuiendesha vizuri bila kuudhi wakubwa, na wakati huo kulinda biashara zake nyingine, haikuwa kazi rahisi. Wapo wengine waliojaribu na wanasuasua sana.  

Kwa Mzee Mengi, haya hayakuwa mazingira rafiki, hata kidogo. Yalikuwa mazingira magumu. Kwamba Mzee Mengi alithubutu kukabiliana nayo, na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, ni jambo la kumuenzi sana. Sisemi alikuwa peke yake katika hili, lakini ni dhahiri kuwa aliongoza akiwa mstari wa mbele kwa kutilia maanani kuwa himaya yake ya habari, mawasiliano na biashara,ilikuwa kubwa kuliko nyingine.

Binafsi, bado sijajaliwa kununua ama kusoma kitabu chake cha “I Can, I Must, I Will. Pengine sasa ni wakati mwafaka zaidi kukinunua na kukisoma. Ni matarajio yangu kuwa katika kitabu hicho atakuwa alipata nafasi ya kuadithia, kwa undani kabisa, safari yake yenye changamoto za kweli kweli ndani ya tasnia ya habari na mawasiliano.

Kama yeye hakubahatika kufanya hivyo, ni matarajio yangu, kama nilivyoanza makala hii, kuwa iko siku mtu mwingine ataelezea kwa undani safari hiyo ya Mzee Mengi. Jaribio langu hili, lilikuwa kumwelezea, kwa ufupi sana, Mzee wetu huyo, Reginald Abraham Mengi kwa uchache sana niliopata kumjua mimi na katika eneo ninalolijua kidogo tu.  Ameondoka duniani kifua mbele, na ni wajibu wetu sisi katika tasni ya habari na mawasiliano, kumuenzi daima. Buriani RAM.  

. Mwandishi wa makala hii, Salva Rweyemamu, ni mwandishi wa habari wa zamani wa magazeti mbali mbali nchini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Tunastawisha ufisadi na kuchukia matunda yake

Spread the loveBUNGE la Jamhuri linaloendelea mjini Dodoma, kwa wiki nzima limetawaliwa...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Wamesahau aliyofanya Magufuli

Spread the loveJUMATATU ya tarehe 16 Oktoba 2023 itabaki kuwa siku ya...

error: Content is protected !!