September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Pwani wamvaa Rais Magufuli

Spread the love

CHAMA Cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Pwani kimemtaka Rais John Magufuli kuendesha nchi kwa kufuta misingi ya sheria na Katiba, anaandika Faki Sosi. 

Kauli hiyo imetolewa na Baraka Mwago, Mwenyekiti wa Chedema Mkoa wa Pwani jana katika tamko la chama hicho mkoani humo.

Mwago amesema kuwa, rais anatakiwa kuruhusu viongozi wengine watekeleze kazi zao za kuisimamia na kuishauri serikali yake na si kuwapinga.

Amesema kuwa, siyo jukumu la rais kutoa maagizo na maelekezo kwa kutumia vitisho, uteuzi wake kwa baadhi ya watu au kutoa zawadia mabilioni ya shilingi kwa vyombo kama Mahakama.

“Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika tunamtaka kuacha mara moja kutumia na kutafsiri kanuni za Bunge vibaya kwa maslahi ya chama chake (CCM) na serikali yake.

“Tunamtaka kutoongozwa na mapenzi ya kuilinda CCM na serikali. Atumie Katiba inayotoa mamlaka kwa Bunge kuisimamia serikali” amesema Mwago.

Pia amesema kuwa Jeshi la Polisi  linataka kuacha kutumiwa na CCM kwa maslahi yake ya kisiasa na kwamba, liheshimu taratibu, kanuni na sheria za nchi na watekeleze wajibu wao wa kulinda “Usalama wa raia na mali zao.”

Kuhusu Jeshi la Polisi kuzuilia mikutano ya vyama vya upinzani amesema kuwa, baraza hilo Mkoa wa Pwani limeshitushwa taarifa hiyo.

“Tukiangalia kanuni za jumla za jeshi la polisi namba 403 kifungu cha kwanza inasema anayetaka  kufanya  maandamano  au  mkutano  wa hadhara kwa mujibu wa sheria hii ni kutoa taarifa tu, tena katika kipindi kisichopungua saa arobaini na nane (48).

“Hii inasisitiza. Baraza la uongozi la Mkoa wa Pwani limeshitushwa kusikia msemaji wa jeshi la polisi amekataza mkutano wa hadhara ambao tayari OCD wa Wilaya ya Kahama alikuwa amesharidhia kwa maandishi,” amesema na kuongeza;

“Upo ushahidi mwingi wa Jeshi la Polisi kutumika kisiasa. Mfano hai, ni pale aliyekuwa Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Michael Kamhanda alipoagiza kuzuiwa kwa mkutano wa Chadema katika eneo la Nyororo mkoani Iringa.

“Amri hii iliyotolewa tarehe 2 Septemba 2012, siyo tu ilikuwa kinyume cha sheria, bali ilisababisha mauaji ya mwandishi wa habari, Marehemu Daud Mwangosi.”

Amesema, hata ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, chini ya Jaji Manento ilieleza kuwa Jeshi la Polisi lilitenda kinyume na sheria ya vyama vya Siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11 (a) na (b) na Sheria ya Polisi (Sura 322).

“Jaji Manento alisema, Kamanda Kamuhanda alikiuka sheria hizo Kwa kuingilia kazi za mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za (Chadema) wakati yeye (Kamuhanda) hakuwa kiongozi wa polisi wa eneo husika,” amesema.

error: Content is protected !!