Saturday , 20 April 2024
Home Kitengo Habari Kimataifa Punguzo la posho lawa moto Kenya
Kimataifa

Punguzo la posho lawa moto Kenya

Uhuru Kenyatta, Rais mteule wa Kenya
Spread the love

MAOFISA wa ngazi ya juu pamoja na wanasiasa wa upinzani nchini Kenya hawajatoa sauti kuhusiana na tamko la Tume ya Mishahara ya serikali kupunguza posho na marupurupu. Lakini mawaziri na wanasiasa wanaomuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta anayetetea wadhifa huo, kupitia uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, wamepongeza, anaandika Catherine Kayombo.

Kama hatua inayoshangaza umma, kwa kuwa haikutarajiwa kimya kizito, mpaka muda huu hakuna kauli yoyote ya kupinga tamko la kupunguza viwango vya posho na marupurupu litakaloanza baada ya uchaguzi.

Badala yake, mawaziri na kwa jumla wanasiasa wa kundi linalomuunga mkono Rais Kenyatta ndio pekee waliosikika wakipongeza uamuzi huo uliotangazwa jana na Mwenyekiti wa Tume ya Mishahara wa Serikali ya Kenya, Sarah Serem.

Tangazo la Serem lilisema kulingana na mpangilio mpya wa ulipaji mishahara, posho na marupurupu kwa maofisa wa serikalini na taasisi zake zitapunguzwa kwa asilimia 35, hatua itatayowezesha kuokolewa takribani Sh. 8 bilioni kwa mwaka.

Miongoni mwa posho zilizofutwa ni malipo ya usafiri wa magari kwa magavana na wabunge na badala yake, mfumo mpya wa marupurupu kwa kuzingatia kanda utafidiwa kutoka kwenye malipo hayo.

Kwa mujibu wa tamko hilo, Rais atalipwa Sh.1.4 milioni za Kenya ambayo ni sawa na Dola 14,000 badala ya Sh.1.65 milioni sawa na Dola 16,500. Mawaziri watalipwa Sh.924,000 za Kenya sawa na Dola 9,240, Spika wa Bunge Sh.1.1 milioni (Dola 11,000) na magavana Sh.924,000 (Dola 9,240).

Serem amesema maafisa wa serikali walikuwa wakitumia vibaya mfumo wa marupurupu wa kukadiriwa kulingana na masafa husika, hivyo punguzo hilo ni njia mojawapo ya kuiwezesha serikali kupeleka fedha zaidi kwenye sekta nyingine ili kukuza uchumi wa nchi.

Leo wanasiasa mbalimbali wa kundi linalomuunga mkono Rais Kenyatta, wameeleza kuridhishwa kwao na tamko la kupunguza matumizi ya serikali kwa njia hiyo ya kukata posho na marupurupu. Wanasema itasaidia kuwanufaisha zaidi wananchi.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Kenyatta, ambaye Machi mwaka huu katika hotuba yake ya mwisho kwa taifa kabla ya uchaguzi mkuu, alisema atatekeleza ahadi hiyo ya miaka minne iliyopita.

Kilio cha kupunguzwa kwa fedha zinazotumika kulipa posho na marupurupu katika sekta ya utumishi wa umma nchini Kenya, kimekuwa cha muda mrefu baada ya kuonekana maisha ya fakhari kubwa wanayoishi.

Viongozi wa dini walipata kushauri serikali kupunguza matumizi hayo kwa asilimia 40 ili fedha zaidi zipelekwe kwenye huduma za jamii na zile zinazochochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Katika pendekezo lao, viongozi wa dini waliokuwa katika mjadala wa uendeshaji mzuri wa serikali, walisema idadi ya viti vya bunge ipunguzwe na kufikia 150, serikali za majimbo ziwe 16, Bunge la Senate liwe la viti 32 na Baraza la Madiwani wa majimbo kuwa na wajumbe 1,050.

“Hatua hii itanusuru fedha nyingi ili zipelekwe kwenye maendeleo ya watu,” lilisema pendekezo la viongozi wa dini huku wakitahadharisha kuwa ni hatari kiwango cha mishahara, posho na marupurupu nchini Kenya kuachiwa kukua.

Waliitaka Tume ya Mishahara na Marupurupu kutumia mamlaka yake ya kikatiba kupunguzia viongozi na maofisa viwango vya posho, na badala yake kuwapatia mapato zaidi watumishi wa kawaida. Walisema walitarajia mabadiliko kwa kuwa somo hilo lilieleweka vema kwa wajumbe wa tume.

Serikali inalipa Sh. 627 bilioni za Kenya kwa mwaka kulipa mishahara na posho. Kiwango hicho ni sawa na asilimia 50 ya mapato yote yanayokusanywa na serikali. Watumishi wa ngazi ya juu serikalini wanafikia 700,000.

“Ni kiwango kikubwa sana. Mapato haya yanalipwa kwa maofisa 700,000 wakiwemo wengi mliopo hapa,” alisema Rais Kenyatta akihutubia taifa kupitia Bunge la Kenya hivi karibuni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Kimataifa

Majaji kuamua hatima ya Zuma leo

Spread the loveMajaji nchini Afrika Kusini leo Jumanne wataamua ikiwa rais wa...

Habari za SiasaKimataifa

Spika Afrika Kusini ajiuzulu kwa tuhuma za rushwa

Spread the loveSpika wa Bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula ametangaza kujiuzulu...

Habari MchanganyikoKimataifa

Tetemeko la ardhi laua 7, lajeruhi 800 Taiwan

Spread the loveWatu wapatao saba wamefariki dunia na wengine zaidi ya 800...

error: Content is protected !!