January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

PSPF kuwakopesha wanachama wake viwanja

Spread the love

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu ameipongeza PSPF kwa kushirikiana na Kampuni ya Kupima na Kupangilia Miji (PIL) na Benki ya Posta Tanzania kwa kutoa huduma ya mikopo ya viwanja katika maeneo yaliyopimwa. Anaandika Hamisi Mguta … (endelea)

Waziri Suluhu aliyasema hayo katika uzinduzi wa huduma hiyo kwa ushirikiano wa PSPF, PIL na Benki ya Posta, iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt jijini Dar es Salaam.

Akitoa shukrani kwa PSPF, Suluhu amesema ushirika huo utakuwa na faida kubwa kwa wanachama wa mfuko huo kwa kuweka akiba na kuendesha familia zao wakiwa na makazi yao ya kudumu.

Waziri Suluhu ameimwagia sifa kampuni ya PIL kwa kuwa wabunifu wa hali ya juu ya kuchukua maeneo yaliyowazi kihalali na kufanyia vipimo kwa bei nafuu.

Hata hivyo amesisitiza kuwa mradi huo utawaondoa wananchi kwenye migogoro ya ardhi na itasaidia serikali kuyafanya maisha ya Mtanzania kuwa bora.

Aidha amewataka wananchi na wanachama wa PSPF kujiunga na huduma hiyo kupata viwanja halali vilivyopimwa na shirika la PIL ili kuepusha migogoro ya ardhi.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka PSPF, Gabriel Silaya amesema watashirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma ya mikopo ya kuanzia maisha, elimu na miradi mbalimbali.

Silaya amesema wanachama wasiopungua 350,000 ni walimu hivyo huduma hiyo mpya itawanufaisha kwa kuwapatia mikopo kupitia Benki ya Posta ili kununua viwanja.

Naye Mtendaji Mkuu wa PIL, Abdulahim Zahran amesema wana imani ya kuwahudumia watanzania kwa kila jitihada kuhakikisha mteja anapata kiwanja kilichopimwa ambacho kitamuwezesha kupata mkopo kutoka Benki ya Posta.

Zahran ametaja maeneo yaliyofanyiwa vipimo ni Kigamboni, Kibaha, Mlandizi, Tanga na Zanzibar.

error: Content is protected !!