June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Propaganda hadi mauaji?

Makamo Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula

Spread the love

PHILIP Mangula- Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, naye amejitumbukiza katika tope la njama za mauaji. Anaandika Christian Mwesiga … (endelea).

Ametajwa na Khalid Kangezi, kuwa ni miongoni mwa waliokuwa wanamtumia kuangamiza maisha ya Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Wengine waliotajwa na Kangezi kuwa wanashirikiana na Mangula kutaka kuangamiza maisha ya kiongozi huyo, ni maofisa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Kagenzi, alikuwa mlinzi wa Dk. Slaa. Ameeleza katika hati yake ya kiapo kuwa Mangula, alimtaka kutekeleza mauaji hayo dhidi ya Dk. Slaa. Mangula hajakana madai hayo.

Ukimya wake huu, unathibitisha kuwa madai haya hajasingiziwa. Anaufahamu kwa undani mpango huu.

Hata hivyo, kitendo cha Mangula kujitumbukiza katika uharamia huu, kinaonyesha kuwapo mahusiano ya mashaka katika nyanja za kisiasa nchini, kati ya CCM na vyama vya upinzani halisi.

Kwa mfano, tangu uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa mwaka 1995 hadi sasa, CCM kimekuwa kikitumia propaganda chafu dhidi ya vyama vingine ili wananchi wasivichague. Propaganda ambazo zinaonesha kuwa CCM kina chuki na vyama vingine vya siasa.

CUF ndicho chama cha kwanza kilichoadhirika na propaganda chafu za CCM. Akiwa katika kampeni katika tarafa ya Ilolanguru (Tabora Kaskazini) Septemba 7, 1995, marehemu Dk. Omari Ali Juma aliwaambia wananchi kuwa wasikichague CUF kwa madai kuwa kilikuwa chama cha watu wa uarabuni.

Fundisho hili lilikuwa ni propaganda chafu na kutokujiweza kisiasa kwani CUF kilikuwa kimesajiliwa kwa mujibu wa taratibu na sheria za kusajili vyama vya siasa. Kwa lugha nyingine kilikuwa kimetimiza taratibu za usajili wa vyama vya siasa. 

Pia, siku moja kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kufanyika, CUF kilituhumiwa na aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Omari Mahita kuwa chama hiki kilikuwa kimeingiza nchini majambia ya kuulia watu. Hapa Mahita alikuwa anakisafishia njia CCM kipate ushindi mnono katika uchaguzi huo. Katika hili alifanikiwa.

Cha kushangaza ni kwamba mpaka sasa si Mahita wala viongozi wa CUF waliokamatwa na kupelekwa mahakamani ili kudhibitisha tuhuma hizi za kuingiza majambia.

Hali hii inaonesha pasi shaka kuwa viongozi wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakitumiwa na CCM kuendesha siasa za kipropaganda dhidi ya vyama vingine vya siasa.

Katika hali ya kushangaza makada wa CCM wakati wa kampeni wamekuwa hawatoi mipango na mikakati ya namna watakavyotekeleza nafasi za uongozi wanazoomba badala yake wanajikita katika kutoa matamko ya kichonganishi na kipropaganda ili kuwafanya wananchi wasivichague vyama vya upinzani. 

Mnamo siku ya Jumamosi Desemba 3,  2005, mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM, Jakaya Kikwete aliwaambia wananchi wa kijiji cha Uru/Mingeni, wilaya ya Moshi vijijini kuwa, “mmekipinga CCM na miaka kumi mnatembea kwenye barabara za vumbi, bado haijatosha…msitoke Chadema au TLP, lakini kura zenu ziende kwa mgombea urais, wabunge na madiwani wa CCM”

Tafsiri ya propaganda hii ni kwamba katika maeneo ambayo wananchi wanachagua madiwani na wabunge wa CCM kuna maendeleo lakini maeneo ambayo ni kinyume na viongozi hawa hakuna maendeleo.

Hii siyo sahihi bali alilenga wananchi wavione vyama vya upinzani havifai maana ushahidi unaonesha kuwa hali ni mbaya sana katika halmashauri zinazoongozwa na CCM.

Waziri Mkuu mstaafu Samwel Malecela alinukuliwa na gazeti la Majira toleo la Mei 18, 2009, akiwaambia wapigakura katika uchaguzi mdogo jimboni Busanda kuwa, “Shetani huyo ametokea wapi anayetaka mvipigie kura vyama vya upinzani, wakati mwaka 2005 mlichagua CCM kwa kishindo? Shetani huyo ashindwe kwa jina la Yesu”.

Bila kujali ukweli kuwa wananchi wana haki ya kuchagua kiongozi wanayemtaka, mnamo Oktoba 9, 2013, Mangula alinukuliwa akipingana na maamuzi ya wananchi wa Kawe kwa kudai kuwa, “ni aibu, mimi ni mkazi wa Oysterbay jijini Dar es Salaam na Mdee (Halima) ndiye mbunge wangu sasa siku akisema anataka kuongea na wazee wa jimbo lake mimi nitafanyaje? Siwezi kwenda, nitasingizia naumwa ili nisiende.”

Kauli hii ya Mangula moja kwa moja inaonesha chuki binafsi aliyonayo kwa Watanzania wenzake wanaoamini katika uongozi wa vyama vingine vya siasa. Kwa hali hii Mangula anapotajwa katika mipango ya mauaji hajaonewa.  

Mnamo Juni 29, 2014, Dk. John Magufuli aliwaambia wananchi wa Chato kuwa CCM kitatawala milele kwa sababu wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri ni wana CCM. 

Maghufuli alitoa kauli hii wakati wafuasi na viongozi wa vyama vya upinzani wakiwa wanalalamikia wakuu wa wilaya na wakurugenzi kuwa wanatumiwa na CCM kuiba kura na kutangaza wagombea wasiostahili.

Kauli hii inatosha kuwajuvya wananchi kuwa utawala wa CCM hautokani na kura wanazopiga bali unatokana na viongozi hawa wanaotajwa.

Uthibitisho wa kauli hii ya Magufuli umeonekana wazi wazi katika chaguzi za Serikali za Mitaa ambapo katika baadhi ya maeneo wakurugenzi waliwaapisha makada wa CCM waliokuwa wameshindwa katika uchaguzi.

Chuo cha siasa cha Kigamboni kilikuwa kikiwandaa makada wa siasa za mfumo wa chama kimoja ili watumike kuwaadaa wananchi. Mafunzo waliyoyapata pale Kigamboni leo hii yanawafanya wapwaye katika siasa za mfumo wa vyama vingi.

Kupwaya huku kunawafanya baadhi ya makada waone ujio wa anguko la chama chao. Kwa kawaida chama kinachoendekeza propaganda mfu za kisiasa hakiwezi kuwa salama mbele ya wapigakura wenye kila aina ya tabu za kiuchumi na kijamii.

Mtu wa kwanza kubaini kupwaya kwa CCM ni Mwalimu Nyerere. Akiwa katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza mnamo Oktoba 3, 1995 wakati akiwahutubia wananchi alisema, “tuna watu wa ajabu ndani ya CCM ambao hawafanani na CCM”.

Mwaka huu chama kinaingia katika uchaguzi mkuu kikiwa na watu wa maajabu. Mpango wake wa kujivua gamba ulioasisiwa na Mwenyekiti wa Taifa Jakaya Kikwete mjini Dodoma mnamo Februari 5, 2011, umeshindwa kukisafisha chama.

Baadhi ya makada waandamizi wa chama hiki waliopewa siku 90 kujivua gamba kabla ya kuvuliwa hilo gamba ni: mbunge wa Monduli Edward Lowassa, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na aliyekuwa mbunge wa Igunga Rostam Aziz. Aziz alijivua gamba lakini Lowassa na Chenge waligoma na chama hakikuchukua hatua. 

Akiongelea mpango wa chama chake kujivua gamba Katibu Mwenezi Taifa, Nape Nnauye akiwa katika kipindi cha Kipimajoto mnamo Januari 13, 2012, alisema, “wenzetu Chadema walitoa orodha ya watu 11 lakini ndani ya CCM wapo zaidi ya hao kwa sababu tunaanzia ngazi ya tawi, tunapanda hadi taifani, hii ni kwa sababu tumedhamiria kukirejesha chama kwenye msingi wake”.

Orodha ya watu 11 ni makada na viongozi waandamizi wa serikali waliotajwa mwaka 2007 na Dk. Willbroad Slaa katika viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam kuwa ni mafisadi. Watu hao ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete na Edward Lowassa.

Kwa mara nyingine Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha ‘Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania (1994)’ anaandika kuwa ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliomfanya akapendekeza uanzishaji wa siasa za mfumo wa vyama vingi. Maana yake ni kwamba mwalimu hakuwa adui wa vyama vya upinzani alijua wazi kuwa kutoka katika vyama hivi ndipo wananchi wanaweza kupata chama kinachofaa kuratibu maisha yao ya kiuchumi na kijamii.

Kada wa CCM na waziri wa zamani katika serikali ya awamu ya pili na ya tatu Mateo Qares anaona kuwa chama hiki hakina tena sifa ya kutoa kiongozi. Gazeti la Mwananchi katika toleo la Novemba 24, 2014, linamnukuu akisema kuwa kiongozi jasiri kabisa atakayefanya uamuzi mgumu dhidi ya mfumo uliovurugika hayupo CCM.

Naye Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Jakaya Kikwete mnamo Novemba 11, 2012 akiwa katika mkutano wa ndani wa chama mjini Dodoma aliwaambia makada wenzake kuwa, “chanzo cha kutofautiana kwetu ni chaguzi zetu na kutafuta ukuu wa dola. Robo tatu ya migawanyiko na migogoro ndani ya CCM inahusiana na vyeo”.

Maslahi binafsi yanawasukuma makada wengi wa CCM kuona kuwa vyama vingine vya siasa havifai kuliongoza taifa letu. Lakini mahubiri yote ya kipropganda yanayohubiriwa na makada hawa kwa nia ya kudumaza maendeleo ya kisiasa ya vyama hivi yanavunja katiba ya nchi yetu.

Ibara ya 3 (1) ya katiba ya nchi yetu toleo la 1977 inasema kuwa Jamhuri ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Kwa mujibu wa ibara hii ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa. Kuwa mgombea kupitia tiketi ya chama chochote cha siasa. Kuchaguliwa na kuchagua mgombea kutoka chama chochote cha siasa.

Maisha ya Watanzania yanazidi kuwa magumu. Propaganda za CCM wananchi wameishazichoka wanataka mabadiliko. Katika hitaji hili kumeibuka siasa mpya ambazo ni mikakati ya kuuana kwa sumu. Bila kuchukua taadhari mapema siasa za propaganda polepole zinageuka kuwa za mauaji hivyo nchi yetu si salama tena.

0756267870/ 0652845836 au chrismwesiga@gmail.com

error: Content is protected !!