May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Profesa Tibaijuka: Rais Samia iangalie Kagera kwa jicho la huruma

Anna Tibaijuka, aliyekuwa Mbunge wa Muleba Kusini

Spread the love

 

MWAKA 1961 tulipopata Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), Kagera ulikuwa mkoa wa pili kwa maendeleo baada ya Kilimanjaro. Hivi sasa wakati ikiwa ni miaka 60 baada ya uhuru, Kagera ni mkoa wa mwisho Tanzania Bara kwa maendeleo. Mwandishi Maalum…(endelea)

Ambapo taarifa rasmi za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) (Consolidated Zonal Economic Performance Report) inaorodhesha pato la Taifa kwa kila mkoa na kwa kila mwananchi au kichwa kwa Tanzania Bara.

Wa kwanza ni Dar es Salaam shilingi milioni 4,678,751. Mwisho namba 25 ni Kagera ambayo ni Sh. milioni 1,168,661.

Kwa asilimia kipato cha mwananchi Mkoa wa Kagera ni asilimia 44 tu ya kipato cha Taifa. Na asilimia 25 au robo ya kipato cha wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.

Ukilinganisha na makao makuu Dodoma pato lake ni Sh. milioni 1,759,347 wakati Kagera ina asilimia 66 au theluthi mbili.

Hali ni tete. Kaya maskini nyingi hata mlo ni wa kubahatisha katika hali ya kawaida. Ukiingiza na mambo ya ukame inakuwa zahama kubwa.

Kimsingi ni kwamba tukubali mkoa ‘slowly but surely’ umefilisika. Tunahitaji kufanya tathmini ya kina kuona tunajikwamua vipi. Nini kazi ya Serikali? Nini jukumu la WanaKagera. Na kipi Rais wetu
Mama Samia atuwekee nguvu? Mambo yalipofikia tunahitaji mbinu zote na mikakati mipya kubadilisha hali hii isiyopendeza.

Rais Samia Suluhu Hassan

Aidha, lazima kumwangalia adui umaskini machoni na kupambana naye. Tukikata tamaa au kulaumu hatutafanikiwa.

Kinachohitajika ni utambuzi na uelewa wa pamoja wa sababu za kufilisika kiasi hiki ili kurekebisha mambo. Tunaweza kujikwamua si kuanguka. Jambo la muhimu ni kwamba lazima tujipange. Kila mtu kwa nafasi yake.

Mwalimu Baba wa Taifa, Julius Kambarage alisema. “It can be done. Play your part.” Inawezekana timiza wajibu wako.

Ninawapongeza waheshimiwa Rais Samia, na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa kwa kupanga safu ya uongozi upya.

Tumeshuhudia maboresho makubwa. Ninawapongeza mawaziri na makatibu wakuu na manaibu wote walioaminiwa na kupewa majukumu ya kuongoza sekta mbalimbali. Ninaomba nao waangalie hii hali tete ya Mkoa wa Kagera. Twafaaa… Tunahitaji msaada.

Mkoa wa Kagera kwa sasa umeachwa na wenzetu wa Kigoma ambao wapo nafasi ya 24, pato lao likiwa ni Sh. milioni 1,479,389; Singida ipo nafasi ya 23 ikiwa na pato la Sh. milioni 1,622,891 sina budi kuwasemea pia. Kwa ujumla wetu: Twafaa. Kazi Iendelee katika mwaka huu wa Otagwisa Mukono.

Mwandishi wa makala haya, Prof. Anna Tibaijuka amewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na pia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati wa Serikali ya awamu ya nne iliyokuwa inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

error: Content is protected !!