April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Profesa Ndalichako atoa maagizo Chuo cha Ualimu Mpwapwa

Spread the love

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameuagiza uongozi wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa jijini Dodoma, kuhakikisha miundombinu ya chuo hicho inalindwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mpwapwa … (endelea).

Hayo ameyasema jana Ijumaa tarehe 19 Juni 2020 alipokagua maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika chuo hicho ambao umegharimu zaidi ya  Sh. 2.8 bilioni.

Akizungumza na wakufunzi, walimu na wanafunzi wa chuo hicho, Profesa Ndalichako alisema, Serikali imeamua kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu ya Taasisi za Elimu ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa elimu kwa Watanzania.

Alitaja miundombinu inayojengwa ni jengo moja la ghorofa kwa ajili ya Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bweni la ghorofa moja la walimu tarajali wa kike, bwalo la chakula na nyumba mbili za watumishi ambazo nyumba moja ina uwezo wa kuchukua familia tatu. 

“Serikali imeamua kwa dhati kuboresha miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ndio maana inawekeza katika eneo hili.”

“Sasa ni jukumu lenu kusimamia na kuhakikisha miundombinu inatunzwa ili iweze kutumika kwa muda mrefu,” alisema Waziri Ndalichako.

Naye Kaimu Katibu Tawala, Said Mwaliego akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Jabili Shekimweri, aliishukuru Wizara kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa chuo hicho. 

Aliiomba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kusimamia mradi huo kwa karibu ili ukamilike kwa wakati. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ualimu Mpwapwa, Gerald Richard aliishukuru wizara kwa kukipatia fedha za ukarabati chuo hicho kwani miundombinu yake ilikuwa imechakaa kutokana na kuwa cha muda mrefu.

Alisema ujenzi wa miundombinu unaoendelea utaongeza nafasi za udahili wa wanachuo wengi zaidi.

error: Content is protected !!