October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Profesa Lumumba aunguruma Chato, ahoji demokrasia

Prof. Patrick Lumumba

Spread the love

 

MCHAMBUZI maarufu wa masuala ya kisiasa na kihistoria katika ukanda wa Afrika Mashariki, Profesa Patrick Lumumba amewataka Watanzania kujihoji kuwa demokrasia ni nini hasa ikizingatiwa kwamba nchi nyingi za kiafrika zimepata uhuru lakini bado kuna ukoloni mamboleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea)

Pia amewataka Watanzania kuzingatia na kuyaenzi maono ya wanaharakati, wapigania uhuru wa nchi za Afrika ambao walisisitiza umuhimu wa nchi za Bara za Afrika kuungana kiuchumi na kisiasa.

Profesa Lumumba ambaye ni Mkuu wa Shule Kuu ya Sheria nchini Kenya ametoa wito huo leo tarehe 13 Oktoba 2021 wakati akichangia mada kwa njia ya kidijitali kutoka nchini Kenya katika Kongamano la Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Mwalimu Nyerere lililofanyika huko Chato mkoani Geita.

Profesa Lumumba alianza kuelezea kwa kina kuhusu historia ya Bara la Afrika kwamba katika kikao cha nchi za Bara la Ulaya kilichofanyika mwaka 1884 hadi 1885 Berlin nchini Ujeruman, kililenga kubuni na kugawa nchi Afrika kwa misingi ya kiuchumi.

“Lengo la nchi hizi iwe ni Ujerumani, Ubelgiji, Uingereza au Ufaransa, lilikuwa ni kuhakikisha wana fursa ya kumiliki maliasili katika nchi mbalimbali za Kiafrika.

“Nchi hizi zilibuniwa hususani kuhakikisha nchi za Afrika zimetawaliwa kimabavu na rasilimali zao zimenyakuliwa,” amesema.

Amesema baada ya nchi hizi za kiafrika kutawaliwa kwa njia ambazo hazikulandana na demokrasia, wanaharakati mbalimbali wa Afrika walijitoa mhanga kurejesha uhuru.

“Akiwamo Mwalimu Nyerere na wengine, walivalia njuga suala la haki ya waafrika kujitawala na hadhi zao zimerejeshwa, kulikuwa na wanaharaati wengi katika Afrika.

“Historia inaeleza kuwa wakati wakishiriki kwenye vita dhidi ya ukoloni, nchi nyingi zilizokuwa zinatawala hazikuwa na lengo la kuruhusu nchi za kiafrika zijitawale, kwa mfano wareno walikuwa na vita dhidi ya Kenya, Msumbiji, Angola, Guinea Bissau na nyingine ambapo watu wengi walipoteza maisha na hatimaye wakoloni walisalimu amri,” amesema.

Aidha, Prof Lumumba amesema Mwanasiasa shupavu wa Ghana, Kwame Nkuruma alisema mkoloni atawapa mamlaka kwa njia za kinyemela na atahakikisha ameifadhi kile ambacho alichokuwa amekishika.

“Akasema njia watakazotumia ni kuwa na sera ya ukoloni mamboleo, na sasa tuko katika hali ya ukoloni mamboleo.

“Tukiangazia suala la uhuru, lazima tujiulize tuna uhuru wa kisiasa, kwa kuwa tunachagua viongozi wetu? tuna wimbo wa taifa? Bendera?, kauli mbiu? na vitu ambavyo vinatueleza kana kwamba sisi ni mataifa huru?.

Julius Nyerere, Hayati Baba wa Taifa

“Lakini katika nyanja ya uchumi kilichopo ni kwamba bado tunaelekezwa kutoka nchi mbalimbali iwe nchi za Ulaya na China hivi sasa, suala ambalo tunahoji leo ni kwamba je, demokrasia ni nini, tunapozungumzia demokrasia, lazima tujikite katika mantiki fulani, tujiulize nani anaeneza demokrasia,” amesema.

Aidha, amesema nchi za kiafrika katika siku za mwanzoni, viongozi wa enzi ya kwanza akiwamo Mwalimu Nyerere walikutana jijini Addis Ababa nchini Ethiopia tarehe 23- 25 Mei, mwaka 1965 kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa umoja.

“Walikuwa viongozi 32, wote walisisitiza muhimu nchi za kiafrika kuungana kisiasa na kiuchumi ili kujikinga dhidi ya harakati za wakoloni na ukoloni mamboleo ambao ulivuruga nchi zinazotoka katika lindi la ukoloni.

“Mwalimu Nyerere alisema umoja ni muhimu ikiwa sisi waafrika na nchi za kiafrika zitajikinga dhidi ya harakati za wakoloni mamboleo, hatuna budi kujiunga ambako kutatuwezesha kujikidhi kiasiasa, kijamii na kichumi.

“Nkrumah alisema mkoloni habadiliki, anachofanya ni kubadilisha mbinu, hata akibadilika ni kuhakikisha ametudhalilisha na kutunyanyasa kwa hiyo hatuna budi sisi waafrika kutambua kuwa lengo letu litafikiwa kwa kutambua na kujikinga dhidi ya harakati hizo,” amesema.

Lumumba amesema katika maswali yaliyoibuka wakati ule ni kwamba; “Je, tubadilishe mipaka? Lakini wakabaini kuwa wakianza harakati za kubadilisha mipaka kutakuwa na vurugu za ajabu na wakoloni watafurahia kwa sababu vita ya panzi furaha ya kunguru.

“Wakakubaliana kwamba tuhifadhi mipaka hii, ila tuhifadhi kulenga kujiunga na umoja wa nchi huru za Afrika, wakati ule umoja huu ulibuniwa kwani kulikuwa na dhana kuwa hatua maalumu zitachukuliwa kuhakikisha nchi huru za Afrika zitaungana,” amesema.

error: Content is protected !!