PROFESA Ibrahim Lipumba, Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF) amesema, wananchi wakishindwa kuutumia Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020 kuleta mabadiliko, watajuta kuipoteza nafasi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumamosi tarehe 12 Septemba 2020 wakati anazungumza na wanahabari mkoani Morogoro, kuhusu mchakato wa uchaguzi huo.
“Uchaguzi huu ni mgumu sana sababu mgombea wa CCM ameonesha suala la ujenzi wa demokrasia na katiba mpya yenye msingi wa demokrasia sio kipaumbele chake, tukiipoteza nafasi hii tutajuta sababu maendeleo yetu ya demokrasia yatarudi nyuma,” amesema Prof. Lipumba.
Wakati huo huo, Prof. Lipumba amewaomba wananchi kuutumia uchaguzi huo, kuchagua viongozi wenye nia ya kuleta katiba mpya na misingi ya demokrasia.
Mwenyekiti huyo wa CUF amesema, harakati za kudai Katiba mpya na misingi mizuri ya demokrasia sio kazi ya viongozi wa kisiasa peke yake, bali ni jukumu la wananchi kuchagua viongozi watakaoleta mabadiliko.
“Ni muhimu sana katika suala la kupata katiba yenye misingi mizuri ya demokrasia sio suala la viongozi peke yao ni suala la wananchi tuweze kujitokeza tulete mabadiliko, tujitokeze katika uchaguzi huu ili tuweze kupata haki,” amesema Prof. Lipumba.
Leave a comment