August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Profesa Lipumba ‘out’ CUF

Spread the love

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), limechukua uamuzi wa kumfukuza uanachama wa chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba, leo Jumanne tarehe 27 Septemba, 2016 katika kikao cha dharura kilichofanyika Makao Makuu ya CUF, mjini Zanzibar, anaandika Charles William.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wajumbe 43 kati ya wajumbe 53 wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa, ambapo sambamba na kumfukuza uanachama Prof. Lipumba lakini pia kimejadili ajenda zingine mbili ikiwemo mvutano uliopo baina yao na Jaji Francis Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa hapa nchini.

“Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za chama,” imeeleza taarifa ya CUF iliyotolewa jioni ya leo.

Aidha taarifa hiyo imedokeza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa baada ya baraza hilo kuridhika na mashtaka dhidi ya Prof. Lipumba kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, Dar es Salaam, tarehe 24 Septemba, 2016 mwaka huu.

“Baraza kuu limetumia uwezo wake, kwa mujibu wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba,” imeeleza taarifa hiyo.

Pia baraza hilo limejadili msimamo na mwongozo wa Msajili wa Vyama vya Siasa alioutoa kupitia barua yake ya tarehe 23/09/2016, ukimtambua Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF na kufikia maazimio ya kuukataa mwongozo huo wa msajili.

“Sheria ya Vyama vya Siasa Na. 5 ya mwaka 1992, Sura ya 258 haimpi msajili mamlaka wala uwezo wa kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya chama, kwa kulitambua hilo ndiyo maana Jaji Mutungi ameshindwa kutaja kifungu cha sheria hiyo kinachompa uwezo huo.

Baraza Kuu la Uongozi la CUF limerejea uamuzi wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo alitoa uamuzi akisema;

“Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa au maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”

Kufuatia uamuzi huo, CUF imemuagiza Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa chama hicho, kumjibu kwa maandishi Jaji Mutungi akimueleza juu ya maamuzi ya baraza hilo kuutupilia mbali ushauri na msimamo wa msajili, kwani kikatiba ndilo lenye madaraka ya kusimamia uendeshaji wa chama.

Kuhusu Prof. Lipumba kupewa nafasi ya kujieleza au la, Baraza Kuu la Uongozi la CUF limeridhika kwamba kamati ya utendaji chama hicho ilimfikishia Prof. Ibrahim Lipumba, barua ya wito, tarehe 24 Septemba, 2016 ambayo pia ilikuwa na maelezo ya tuhuma lakini msomi huyo amepuuza wito huo.

Itakumbukwa kuwa, siku ya jana Jumatatu Prof. Lipumba alinukuliwa na  vyombo vya habari akieleza kutotambua kuitishwa kwa baraza hilo la CUF huku Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu-Bara wa chama hicho naye akiungana naye kutokitambua kikao hicho.

Tarehe 28 Agosti mwaka huu Baraza Kuu la Uongozi la CUF taifa lilifikia uamuzi wa kuwasimamisha uanachama watu 11 akiwemo Prof. Lipumba na wabunge Magdalena Sakaya wa Jimbo la Kaliua na Maftah Nachuma wa Jimbo la Mtwara Mjini.

error: Content is protected !!