August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Profesa Lipumba, 10 wakatwa CUF

Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimemsimamisha uanachama aliyekuwa mwenyekiti wake wa taifa, Profesa Ibrahim Lipumba kwa tuhuma za kuwa kinara wa vurugu zilizosababisha mkutano mkuu maalum wa chama hicho kuvunjika., anaandika Aisha Amran.

Pamoja naye katika adhabu hiyo ni viongozi waandamizi wengine 10 akiwemo Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftaha Nachuma na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Abdul Kambaya.

Uamuzi huo umetangazwa rasmi leo na Naibu Katibu Mkuu wa chama Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui wakati akitoa taarifa ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa (BKUT), kilichofanyika mjini Zanzibar jana.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wengine waliochukuliwa hatua hiyo hadi watakapojieleza mbele ya Baraza Kuu hilo, ni Ashura Mustafa, Omar Mhina Masoud, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.

Wakati Ashura ni mjumbe wa Baraza Kuu na mwanamama aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma wa chama, Mnyaa na Kombo, ni viongozi wazoefu waliokuwa wabunge kipindi cha 2010/2015; Mnyaa akiwakilisha jimbo la Mkanyageni na Kombo jimbo la Chake Chake, kisiwani Pemba.

Taarifa ya CUF imesema Profesa Lipumba amechukuliwa kama kiongozi wa vurugu ambazo chama kimesema ni “hujuma za makusudi zilizoandaliwa kwa mashirikiano na maadui wa ndani na nje ya chama kwa nia ya kukihujumu.”

Mkutano mkuu maalum wa CUF ulifanyika 21 Agosti kwenye Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, ukiwa na agenda mbili ikiwemo ya kuchagua mwenyekiti mpya baada ya Prof. Lipumba kujiuzulu kwa hiari 5 Agosti mwaka jana.

“… (vurugu) hazikuwa za bahati mbaya au za kushtukiza bali ni matokeo ya njama na mbinu ovu na chafu ambazo zimekuwa zikipangwa na kutekelezwa chini kwa chini kwa muda mrefu,” imesema taarifa ikieleza namna wajumbe wa Baraza Kuu walivyotoa ushahidi uliowagusa watuhumiwa.

Mazrui ambaye alisoma taarifa mbele ya waandishi wa habari mjini Zanzibar, amesema wajumbe wa Baraza wamesikitishwa na “jinsi baadhi ya viongozi wa walioaminiwa na kupewa nyadhifa za juu walivyogeuka na kuanza kutumiwa na maadui wa nje ya Chama kukihujumu Chama.”

“Baraza Kuu limezingatia kuwa CUF ni chama cha kistaarabu, niChama cha kidemokrasia na ni Chama chenye kutoa matumini ya mabadiliko ya kweli kwa Watanzania walio wengi. Vurugu zilizojitokeza ni aibu na fedheha kwa chama chetu mbele ya macho ya Watanzania na wapenda demokrasia,” amesema.

Mazrui amesema viongozi hao walipewa nafasi mara kadhaa kujirekebisha dhidi ya mwendo wao huo lakini “waliendelea na vurugu na hujuma zao hizo… Baraza Kuu limeona halina njia nyengine ya kukinusuru Chama isipokuwa kuchukua hatua kali na madhubuti kukilinda Chama ambao ni wajibu wake kikatiba.”

Chama hicho kimemfukuza uanachama Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Shashu Lugeye baada ya kutoridhika na maelezo yake ya utetezi mbele ya Baraza hilo, huku likiwapa karipio kali Rukiya Kassim Ahmed na Athumani Henku ambao pia ni wajumbe wa baraza hilo.

Hatua hizo zimeibua Kambaya ambaye wakati anakiri baraza kuu linayo mamlaka ya kikatiba ya kufanya hivyo, anasema hatua hiyo inafanana na kilichofanywa katika kisa cha Firauni (Pharaoh) na Nabii Mussa ambaye alikuwa akimpinga.

“Si jambo geni, hata Firauni aliposhindwa kujibu hoja za Nabii Mussa alitumia jeshi,” ameandika Kambaya katika taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii leo.

Kambaya amesema chama kimetoa adhabu kabla ya kutoa majibu ya hoja za wanachama waliolalamika rasmi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, akiwemo yeye, kufuatia yaliyotokea kwenye mkutano mkuu maalum.

“Nawaomba Wana-CUF msifadhahike na wala msihuzunike waliotufukuza kabla hata ya kutoa majibu ya hoja zetu tulizowasilisha kwa Msajili, bila shaka hawana majibu sahihi ya hoja zetu. Na jambo hili sio geni kwa hapa duniani, Firaun aliposhindwa kuthibitisha kuwa yeye ndie Mungu, alitumia jeshi lake (Baraza Kuu) kutaka kumuangamiza Mussa na wafuasi wake waliokuwa wanaamini katika haki na Mungu wa kweli,” alisema.

 

error: Content is protected !!