PROFESA Shadrack Mwakalila, Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere ameitaka serikali kuwapeleka viongozi wake kusomea mafunzo ya maadili na uongozi katika chuo hicho ili kupata uelewa wa jinsi ya kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, muasisi wa Taifa la Tanzania, anaandika Aisha Amran.
Prof. Mwakalila ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku mbili tu kuelekea katika kongamano maalum la maadhimisho ya miaka 17 ya kumuenzi Mwalimu Nyerere ambalo litafanyika Ijumaa ya tarehe 14 Oktoba, mwaka huu.
“Miiko ya uongozi ambayo imefafanuliwa kwenye Azimio la Arusha mwaka 1967 imekuwa na mabadiliko makubwa katika miaka ya 90 katika ngazi ya kisiasa, kiuchumi pamoja na sera zake, hali iliyopelekea viongozi wengi kutumia vibaya fursa hiyo na kupelekea mmomonyoko wa maadili kwa uongozi na jamii kwa ujumla ,” amesema.
Mwakalila amesema watu wengi wanadhani Azimio la Arusha na kila jambo ambalo lipo kwenye Azimio hilo limekufa, lakini ukweli ni kuwa misingi hiyo bado inasihi mpaka leo na inaweza kuliokoa taifa katika mmomonyoko wa kimaadili unaoendeleza kujitokeza.
“Misingi ya Azimio la Arusha iko vizuri hata baba wa Taifa alisema kuwa katika hilo hakuna kasoro lakini wengine walitafsiri vibaya kutokana na viongozi kutumia vibaya fursa walizokuwa wakipata,” amesema Mwakalila.
Aidha amesema kuwa chuo hicho kitafanya kongamano la kumuenzi Mwalimu Nyerere katika ukumbi wa Utamaduni ulipo chuoni hapo na kwamba viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi mbalimbali watahudhuria ili kujifunza namna ya kuziishi falsafa za Baba wa Taifa na misingi imara ya maadili ya kazi na utawala.
More Stories
Askofu Kilaini alaani Klabu ya Simba kutumia msalaba kwa dhihaka
NMB kunufaisha sekta ya kilimo Tanzania
Dk. Mwinyi: Utafiti ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa