June 19, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Profesa amejichafua, atashindwa tu

Spread the love

 

WAPO wanaomshauri Profesa Ibrahim Lipumba ajiunge na CCM (Chama Cha Mapinduzi), na sababu anayotajiwa kwa ushauri huo, inatajwa kuwa ndiko atatumika ipasavyo. Sawa, inaweza kuwa ndiko atatumika au kutumiwa, anaandika Jabir Idrissa.

Mchambuzi mmoja anasema Prof. Lipumba atatumika vizuri huko CCM kwa sababu tayari amewasaidia kwa “kuwafanyia kazi nzuri ya kuhakikisha Edward Lowassa haupati urais ng’o.”

Ushauri huu siuamini na simtakii profesa huyu mahiri wa uchumi ari na utashi wa kuamua kuingia chama hicho ambacho kadiri siku ziendavyo, naona kinazidi kuthibitisha kinaishi kwa kuhitaji sana msaada wa vyombo vya dola.

Kwanza sidhani kama ni kweli Prof. Lipumba alitumika kumzuia Lowassa kupata urais wakati wa uchaguzi mkuu uliopita. Lowassa alifanya kampeni nzuri kuliko mgombea mwingine yeyote wa wadhifa huo katika wale walioingia kugombea.

Lowassa, waziri mkuu aliyeshika nafasi hiyo kipindi kifupi zaidi katika jamhuri hii – Novemba 2005 hadi Februari 2007 – alizichangamsha siasa za Tanzania zaidi kuliko mwanasiasa mwingine yeyote tangu kipindi kile.

Na kwa ufundi wa timu ya kampeni iliyomsimamia, ikiongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) chini ya mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), alirudisha heshima yake kisiasa na kimtizamo.

Heshima ya Lowassa anayeichagiza CCM hata viongozi wake kukosa usingizi kikawaida, ilikuwa imefifia kutokana na tuhuma nzito za kuwa fisadi miongoni mwa makada wa CCM waliotajwa na chama hicho kama magamba.

Ukweli huo ulimpaisha akaeleweka zaidi alivyo kiuongozi, bali pia alivyo na mahaba makubwa kwa nchi na watu wake. Hizo zikawa hazina zilizomhakikishia uungwaji mkono na hatimaye milioni nyingi za kura.

Walipoona wingi wa kura zake, wasimamizi wa ulinzi na usalama waliokuwa katika hekaheka zisizo mfano, wakapata kiwewe. Kwa shinikizo nzito, wakalazimika kutumia ufundi waliofunzwa kubadilisha mazingira walimokuwa. Hawakujali kuumiza vijana na kutunga uongo katika kudhibiti hali, ilimradi waridhishe wakubwa zao.

Vitendo vilivyofanyika hadharani, ikiwemo kuvamia ofisi ya kupokelea matokeo ya kura za urais za mgombea wa UKAWA, vilisaidia kufungua zaidi macho ya wafuatiliaji siasa na wakajua ni upi utakuwa mwisho wa Lowassa katika matumaini yake ya kuunyaka uongozi wa taifa, chini ya kaulimbiu aliyoichagua ya “Lowassa mabadiliko, mabadiliko Lowassa.”

Mimi naona Prof. Lipumba analazimika kwanza kukubali ukweli kuwa kwa alipofikia sasa, maji ya shingoni kwake kubakia CUF. Namuonea huruma maana amejenga hofu moyoni mwake pamoja na kujitia ujasiri wa kung’ang’ania jengo la Ofisi Kuu ya CUF Buguruni.

Msukosuko aliojipa kwa sababu anazozijua, umemgeuka kuwa msomi aliyejichafua kwa kiwango cha kutisha mbele ya umma wa CUF na Watanzania.

Anavyoshikilia kuwa angali mwenyekiti, tena halali, ndivyo anavyoongeza kasi ya kujipotezea heshima kidogo aliyobaki nayo.

Kwa hakika profesa wa uchumi amegeuka mbumbumbu. Angeangalia sababu zinazosukuma wachora katuni kumfikiria kila wakati. Ona anavyochorwa karikacha hii na ile zikimuelezea kwa namna za ovyo.

Mchoraji mmoja katika gazeti la Kingereza Ijumaa iliyopita, alimchora aliyeonekana ni profesa akiwa amevaa shuka au seruni au taulo au kaptura; tumbo wazi, kinywani ameshika msuaki na mikononi (wa kushoto) ameshika kopo na (kulia) ndoo.

Karikacha inamuonesha mtu amevaa ndara miguuni na miwani ipo vizuri inapovaliwa. Mkato wa nywele ni wa ujana; sijui ni panki au wanaitaje wenyewe. Mtu yupo chumbani, hapana, ni ofisini ambako amekugeuza chumba cha kulala. Vipi, amefukuzwa na mama?

Alama za chumba zinazoonekana ni godoro ambalo ni kama limewekwa sakafuni huku likiwa limebeba mto. Juu ya meza inaonekana kompyuta, simu ya mezani, karatasi chache, kikombe na bendera yenye nembo ya CUF.

Mtu anaonekana kama vile anachapa kazi kwelikweli kwa kuwa kikapu cha kutupia taka ofisini, kimejaa uchafu hadi karatasi nyingine kukutwa chini zimeanguka.

Yu kwenye chumba ambacho mlango wake umefungwa kwa ndani; lakini umesheheni vitasa na kuwekewa chuma maalum cha kuuzuia kufunguliwa kwa ndani. Profesa amejifungia!

Kwa hivyo, leo anashuhudiwa profesa aliyekuwa tishio kwa utawala, amejifungia katika chumba kilicho varuvaru. Katika uhalisia, inaonekana tangu aliposimamishwa uanachama na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) la chama hicho Agosti 28 mjini Zanzibar, ameamua kuhama kwa muda nyumbani kwake, na kuhamia Buguruni.

Sasa huyu ndo Profesa Lipumba wa leo. Akiwa hapo, na kikundi kinachozidi kupungua, anatamba akisimamia msimamo wa kisanii wa Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji Francis Mutungi, kumthibitisha ndiye kiongozi.

Jaji Mutungi ambaye analalamikiwa na wajuzi wa sheria na wakuu wa upinzani, alifanya hivyo baada ya kufanya uchambuzi wa malalamiko yake na taarifa zilizo zilizowasilishwa na uongozi wa CUF, usiomtambua baada ya kumsimamisha.

Lakini pia jaji amesahau kuwa bado tovutini mwa msajili hadi juzi tu akitambulika Wakili Twaha Taslima kuwa kiongozi halali baada ya Prof. Lipumba kujiuzulu mwenyewe kwa barua ya 5 Agosti 2015. Wakili Taslima aliteuliwa baadaye kuongoza kamati ya muda ya kufanya kazi ya mwenyekiti na makamu wake.

Hatua inayosomeka kwamba profesa amevuliwa uanachama ilikuja kwa kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Uongozi cha 27 Septemba 2016, baada ya kutofika kujitetea dhidi ya tuhuma kuwa amedharau wito wa kufika mbele kujieleza ni kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kufuatia shitaka la kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya chama iliopo Buguruni, jijini Dar es Salaam tarehe 24 Septemba, 2016.

Ushauri mzuri kwa Profesa angechagua njia ya mahakama kuitafuta haki. Kule angesikilizwa anachokiamini, kikapimwa na ukasikilizwa utetezi wa CUF, na akasubiri hatima yake. Ameamua kuamini serikali ileile iliyofurahia kuvunjwa kwake mkono 2005 na kubebwa juujuu na vijana Januari 2015 Mtoni kwa Azizi Ali.

Namsema Prof. Lipumba kwa sababu fujo zake naziona kama zinavyoonekana na wengi zimelenga kudhoofisha nguvu za CUF kupigania haki ya Wazanzibari walioichagua 25 Oktoba 2015 Zanzibar.

Isitoshe, kujenga kwake uswahiba na walewale waliomdhalilisha huko nyuma alipokuwa imara kitini, kunaazimia kuangamiza harakati za mabadiliko nchi nzima. Natabiri atashindwa baada ya muda si mrefu, lakini kuua nguvu ya upinzani ndio mwelekeo wa kampeni yake iliyojaa dalili za kufadhiliwa na watawala.

 

error: Content is protected !!