January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Tibaijuka atema cheche

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka (kulia) akiwa na James Rugamalira na mkewe

Spread the love

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka, amedai kuna njama zinazolenga kumchafu kisiasa kwa kumhusisha na ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Escrow, MwanaHALISI Online linaripoti.

Amesema, hajawahi kuhusika kwa njia yoyote ile, kuruhusu au kunyamazia ukwapuaji wa Sh. 321 zilizohifadhiwa katika Akaunti ya Escrow, ndani ya Benki Kuu (BoT).

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Alhamisi, Prof. Tibaijuka alisema, “Wapo watu wasionitakia mema. Hao ndiyo wanaeneza taarifa kuwa nilihusika na ukwapuaji wa fedha katika akaunti ya Escrow.”

Prof. Tibaijuka amekiri kupokea kiasi cha Sh. 1.6 bilioni, kutoka kwa James Rugemalira, mmoja wa wanahisa wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Hata hivyo, Prof. Tibaijuka amekana kuwa fedha hizo hazikuwa zake binafsi, bali alizipokea kama msaada kwa ajili ya shule ya Barbro Johansson,iliyoko Kimara, jijini Dar es Salaam.

Taarifa zinasema, Rugemalira amepata zaidi ya Sh. 75.8 bilioni kutokana na kilichoitwa, “mauzo ya hisa zake” kwa kampuni ya Pan-African Power Limited (PAP) inayodaiwa kununua kampuni ya IPTL.

Kampuni ya IPTL ni ubia wa makampuni mawili – VIP Engineering and Marketing Ltd ya Rugemalira na kampuni ya Mechmar Corporation ya Malaysia (MECHMAR).

 

 

 

Alisema Rugemalira hakuwa mtu wa kwanza kuchangia maendeleo ya shule yake. Aliwataja wengine waliochangia kuwa ni pamoja na Reginald Mengi na serikali ya Sweden ambayo ilichangia zaidi ya Sh. 8 bilioni.

“…nilikuwa mtu wa kwanza kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, tena bila kushinikizwa na chombo au mamlaka yoyote, kuhusu mchango niliyopewa na Rugemalira,” alisema Prof. Tibaijuka.

Akizungumzia iwapo anaweza kujiuzulu ili kulinda hadhi yake, Prof. Tibaijuka alisema, “Nijiuzulu kwa sababu gani? Kwa sababu nimepata mchango wa shule? Mimi sijiuzulu, nikijiuzulu sitaiendea haki dhana ya uwajibikaji. Kujiuzulu sio fasheni, lazima kuwe na sababu.”

Amesema, “Iwapo itathibitishwa fedha nilizopokea kutoka kwa Rugemalira ni haramu, basi nitazirudisha kwa sababu taasisi yangu haikai na fedha haramu.”

Prof. Tibaijuka alishangazwa na kitendo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutomhoji kuhusiana na sakata hilo ili aweze kulitolea maelezo yake, licha ya kamati hiyo kukiri kwamba haikuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu umiliki, uhalali na uharamu wa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ya Tegeta na watu waliogawiwa.

Alisema kuna mkanganyiko katika maazimio ya Bunge, ambapo katika azimio la pili imeelezwa kuwa wahusika wote wachunguzwe na vyombo husika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa miujibu wa sheria za nchi, lakini katika azimio la tatu bunge hilo hilo limeazimia kuwa wahusika, wakiwemo mawaziri wawajibike.

“Kwa kuwa ukizingatia hayo, uamuzi wa Bunge katika azimio lake la tatu ‘kuishauri Mamlaka ya Uteuzi pamoja na mambo mengine kumuwajibisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi unakuwa, kwa ufahamu na maoni yangu jambo la kushangaza kwa sababu ni suala ambalo halimuhusu na hana dhamana nalo.”

Alifafanua kwamba jambo hilo linakiuka kanuni ya msingi ya haki ya asili ambayo ni kutomhukumu mtu yeyote wakati uchunguzi wa jambo unaendelea na bila kumsikiliza.

https://soundcloud.com/mwanahalisinionline/tibaijuka-agoma

“Si dalili ya kuheshimu msingi wa utawala bora na utoaji wa haki. Kwa hiyo azimio la pili la Bunge linaloitaka Mamlaka ya Uteuzi kuniwajibisha halinitendei haki kabisa na linanionea waziwazi kwa sababu wazijuazo walioshiriki katika maamuzi hayo na kuyaleta mbele ya Bunge usiku yapitishwe,” aliongeza.

Aliongeza kuwa katika taarifa ya Ukaguzi Maalum kuhusiana na miamala iliyofanyika katika akaunti ya Escrow ya Tegeta, pamoja na umiliki wa Kampuni ya IPTL hakuna sehemu ambapo jina lake linatajwa na kuonekana kushiriki katika suala hilo.

error: Content is protected !!