July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Tibaijuka aponzwa na urais 2015

Prof. Anna Tibaijuka

Spread the love

SPIKA wa Bunge la Jamhuri, Anne Makinda, hakumnyima nafasi ya kujieleza bungeni, Prof. Anna Tibaijuka, kwa bahati mbaya. Alikusudia ili kumuangamiza kisiasa. Sarafina Lidwino anaripoti.

Anne Makinda, Spika wa Bunge, hawezi kukwepa tuhuma na shutuma kuwa alipanga kumuangamiza kisiasa, Prof. Anna Tibaijuka, ili kupunguza ushindani katika mradi wake wa kusaka urais mwaka kesho.

Taarifa kutoka bungeni mjini Dodoma zinasema, Prof. Tibaijuka alifanya jitahada kubwa kutaka kutaka kujieleza bungeni juu ya madai hayo, lakini viongozi wa Bunge walimnyima haki hiyo.

Shinikizo la kumzuia Prof. Tibaijuka kujieleza bungeni, lilipewa nguvu na mwanamke mwenzake – Anne Makinda – ambaye anamwona mwanasiasa huyo anayejitambulisha kuwa mwanaharakati wa maendeleo, kama tishio katika “…harakati zake za kuwania urais.”

Makinda ni miongoni mwa wanawake waliotangaza kimya kimya, kujitosa katika mbio za urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka kesho, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Wengine waliotangaza “kimya kimya” kujitosa katika kinyang’anyiro hicho, ni Prof. Tibaijuka na Dk. Asha –Rose Migiro.

Prof. Tibaijuka, ambaye alikuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, alituhumiwa bungeni kupokea kiasi cha Sh. 1.6 bilioni kutoka kwa James Rugemalira, mmoja wa wanahisa katika kampuni ya kufua umeme ya IPTL.

Rais Kikwete, alitangaza kumfukuza kazi mbunge huyo wa Muleba Kusini (CCM), katika mkutano wake na walioitwa, “Wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jublee.

Alidai kuwa Prof. Tibaijuka amefutwa kazi kwa “tuhuma za ukosefu wa maadili.”

Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema, katika kupigania haki yake ya kujieleza, Prof. Tibaijuka, alimuandikia barua Spika akiomba kupewa nafasi ya kujibu tuhuma zilizoibuliwa dhidi yake kuwa amepokea fedha kutoka kwa Rugemalira.

Akiandika kwa Spika Anne Makinda, tarehe 28 Novemba 2014, Prof. Tibaijuka alisema, “Pamoja na kuomba kuchangia kupitia Mhe. Jenista Mhagama – katibu wa wabunge wa CCM – hadi sasa hakuna uhakika kama nitapewa nafasi hiyo kabla ya hoja kufungwa.”

 

TIBAIJUKA

Barua kutoka kwa Prof. Tibaijuka kwenda kwa Makinda, ilikuwa na kichwa cha maneno, “Muda wa kujitetea mbele ya Bunge kufuatana na kutajwa kwa (majina) katika taarifa ya PAC – Issue ya Escrow.”

Prof. Tibaijuka anaandika katika barua hiyo, “Ninaleta maombi rasmi kwako kwamba nijulishwe kama ombi langu hilo litakubaliwa ili nisilazimike kuomba openly from the floor” – kuomba waziwazi ndani ya ukumbi.

Katika kile ambacho mbunge mmoja ameita mkakati wa kumzima Prof. Tibaijuka, Spika Makinda alijibu barua hiyo kwa kusema, “…suala hili ni kubwa sana. Maelezo yako hapa bungeni hayataweza kukupatia haki ambayo unastahili.”

Alisema, “Ushauri wangu jiandae vizuri kusudi vyombo vitakavyoshughulikia suala hilo vikikutaka uweze kujieleza uwe umejiandaa vizuri. Hivyo hatuwezi kukupa muda humu bungeni ili ujitetee.”

Barua ya Makinda ambayo ilimjibu Prof. Tibaijuka, iliandikwa 28 Novemba 2014 na ina Kumb. Na. CBC.155/188/02/16.

Hata hivyo, Prof. Tibaijuka hakukubaliana na maelekezo ya Spika Makinda. Akiandika kwa spika, siku hiyohiyo, Prof. Tibaijuka alisema, “Asante kwa kujibu barua yangu. Ninakusihi sana unipe muda kuchangia kama unanitakia kheri katika maisha yangu. Dunia inasubiri kauli yangu.”

Makinda alijibu andishi hilo, muda mfupi baadaye kwa kusema, “Mh. Prof. Tibaijuka, bunge hili haliwezi kukusaidia. Naomba ukubali kujiandaa kwa hatua nyingine. Maana wataibua hata yale ambayo hayapo humu. Naomba unisikilize.”

Kabla ripoti ya Bunge kuwasilishwa bungeni, hakuna chombo chochote cha Bunge wala ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyomhoji Prof. Tibaijuka.

error: Content is protected !!