May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof Shivji awabana wagombea urais TLS kuhusu sheria kandamizi

Spread the love

 

MHADHIRI Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji, amewahoji wagombea urais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), kwa nini walikuwa kimya wakati sheria kandamizi zinapitishwa bungeni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Wagombea hao ni, Rais wa TLS anayemaliza muda wake, Profesa Edward Hoseah. Jeremiah Mtobesya na Harold Sungusia.

Prof. Shiviji ameuliza swali hilo leo Jumatano, tarehe 27 Aprili 2022, jijini Dar es Salaam, katika mdahalo wa wagombea urais wa TLS, katika uchaguzi mkuu wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa Mei, mwaka huu.

Mwanazuoni huyo amewahoji , endapo watapata ridhaa hiyo, watachukua hatua gani kuhakikisha sheria hizo zinafutwa au zinarekebishwa.

“Katika miaka mitano iliyopita nchi hii imeona sheria mbaya sana zimepitishwa, TLS ilikuwa kimya, hata mmoja wenu hakuzungumzia akichaguliwa kuwa Rais atafanya nini kuona sheria hizo zinafutwa au zinarekebishwa,” amesema Prof. Shivji.

Akijibu swali hilo, Mtobesya amesema endapo akichaguliwa atatumia mpango kazi wa TLS kutatua changamoto hiyo.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Issa Shivji

“Naomba nirudi kwenye mpango kazi, sababu ni ya utendaji kazi. Ukiusoma unaelekeza kazi nyingi ambazo zinalenga kwenye masuala ya TLS iwe relevance kwa wanachama wake, jamii na mamlaka. Moja ya kazi ni kuangalia sheria kandamizi zilizotungwa, nikiingia nitatekeleza na kushughulikia,” amesema Mtobesya.

Naye Prof. Hoseah amejibu swali hilo akisema “Profesa mimi nakupa changamoto sababu wewe una kero na haya mambo kwa nini huji tuongee? Ungepiga tu simu Edward mbona hii kitu hajasema unakaa kimya? Prof. Shivji njoo ufanye kazi.”

“Nikichaguliwa kuwa Rais nitashughulikia hili, lakini naomba tukutumie vizuri wewe ni baba yetu,” amesema Prof. Hoseah.

Kwa upande wake Sungusia, amesema endapo akipata nafasi hiyo, atatumia kamati za TLS kushughulikia masuala makubwa yanayohusu taifa.

“Profesa umeuliza swali kuhusu ushawishi wa kijamii na majukumu ya TLS kwenye mambo makubwa yenye maslahi mapana ya kitaifa na kusaidia wananchi. Nafahamu TLS ina kamati ambazo ziko maalumu kwa lengo la kuwahudumia wananchi,” amesema Sungusia.

error: Content is protected !!