Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Safari: Ndugai anatumia Katiba ipi?
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Safari: Ndugai anatumia Katiba ipi?

Spread the love

 

PROFSA Abdallah Safari, mmoja wa wananasheria mahiri nchini Tanzania, amesema, hatua ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuendelea kuwakingia kifua wabunge 19, waliofukuzwa uanachama wa Chama Kikuu cha Upinzania nchini humo-Chadema, ni uvunjifu wa wazi wa Katiba na sheria za nchi. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

“Duniani kote, ukishatiwa hatiani, unatakiwa kutumikia adhabu uliyopewa mpaka rufaa yako isikilizwe na ushinde.”

“Hiyo ni kwenye kesi ya madai au jinai. Ndiyo sheria na kanuni zinavyoelekeza,” amesema Prof. Safari, katika mahojiano yake na gazeti la Raia Mwema, hivi karibuni.

Amesema, “tayari kuna utaratibu, tokea wakati wa TANU (Tanganyika African Union), hadi sasa, kwamba mtu akifukuzwa uanachama wa chama cha siasa, anapoteza ubunge. Ndivyo alivyopoteza Kasella Bantu na wengine, akiwamo juzi Sophia Simba.”

Amesema, Katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya 67 (1) (b), inaelekeza kuwa mtu anayepaswa kuwa mbunge, ni sharti awe ni mwanachama wa cha siasa na aliyependekezwa na chama chake.

Aidha, sheria ya uchaguzi, inavitaka vyama vya siasa, vinavyoshiriki uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, kuwasilisha kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), orodha ya majina ya wanachama wake, wanaopendekezwa kuwa wabunge wa viti maalum.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinyume na maelezo yaliyotolewa na NEC, hakijawahi kuwasilisha orodha ya wabunge wa viti maalum.

Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika, amesisitiza mara kadhaa, chama hicho hakijapeleka orodha ya majina hayo NEC, wala kujaza fomu Na. 8 (d) zinazopaswa kujazwa kwa wanawake walioteuliwa kuwa wabunge wa viti maalum.

Hayo yanajitokeza, kipindi ambacho Spika Ndugai amekuwa akisema, hawezi kuwafukuza wabunge hao akiwemo Halima Mdee kwa kuwa barua aliyotumiwa na Mnyika, haijakidhi vigezo.

Alisema, “katibu yoyote anayeniandikia barua yenye mgogoro, usiniandikie kipeperushi tu. Aandike barua, aambatanishe na katiba yake, aniambatanishie na muhtasari wa hicho kikao, yawezekana huyo katibu mkuu amendika tu huko.”

Spika Ndugai amesema, hawezi kuwaondoa bungeni wabunge hao kwa kuwa suala lao, wamelipeleka Baraza Kuu la taifa (BKT), na kudai hawezi kuwafukuza wabunge bungeni, wakati hawajasikilizwa na chama chao.

Alisema, “Katiba yao, ina mambo ndani yake, wamechukua hatua za ndani ya Katiba yao, kwa katiba yao kuna Baraza Kuu, hilo Baraza Kuu limekutana, limefanya uamuzi wa mwisho? Vipo vyama, vimejaa mfumo dume. Wapo watu wanakaa wanafukuza watu 19 kwa mpigo tena wanawake, kwa barua tu tena kipeperushi!”

Kiongozi huyo wa Bunge alisema, “tabia ya kuonea wanawake lazima iishe katika nchi hii, kwa kupambana na baadhi ya vyama kama hiki cha ajabu ajabu. Nani asiyejua hawa mabinti waliovyopambana?”

Akijibu madai hayo, Prof. Safari amesema, “hata Spika mstaafu, Pius Msekwa, ambaye ni mtu anayehishimiwa sana katika maaspika waliopo, ameshalitolea jambo hili Fatwa (maamuzi yasiyopingika). Kwamba hawa kina Mdee, siyo wabunge kwa mujibu wa Katiba. Spika Ndugai aache kupotosha.”

Amesema, “Spika Ndugai, hana uhalali wa kuwabakiza bungeni Mdee na wenzake, kwa kuwa huwezi kuwa mbunge, bila kupitia chama cha siasa.

“Kama wenzake waliopita, walifanya maamuzi ya aina hii, kuanzia TANU hadi CCM, kwa nini iwe tofauti sasa. Kwani Ndugai anatumia katiba gani? Siyo hii ambayo imekuwa ikitumika siku zote?”

Prof. Safari anasema, kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, katibu mkuu wa chama ndiye anayepeka majina NEC, na kwamba Mnyika amenukuliwa mara kadhaa akieleza kuwa hajawahi kupeleka majina hayo.

“Hii siyo dhihaka kwa Bunge pekee. Ni dhihaka kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ambayo Ndugai ameapa kuilinda na kuitetea,” ameeleza Prof. Safari, ambaye ni mbobezi kwenye masuala ya kesi za jinai na katiba.

Anasema, Spika Ndugai angekuwa mkweli, angempa nafasi Nape Nnauye, kufafanua alichokieleza. Anasema, Ndugai hakufanya hivyo, kwa kuwa alihofia kuumbuliwa na mbunge huyo wa Mtama.

Kamati Kuu (CC) ya Chadema, iliyokutana jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Novemba 2021, ilipitisha kwa kauli moja, azimio la kuwafuta uanachama wabunge hao 19, wakiongozwa na Halima Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa Bawacha.

Naye aliyekuwa Kamishina wa Bunge, katika Bunge lililopita, Mchungaji Peter Msigwa, amehoji mamlaka ya Ndugai kutaka kuingilia mambo ya ndani ya Chadema na kusema, “jukumu lake, kwa mujibu wa sheria, ni kutekeleza maelekezo ya vyama. Kazi ya kutafsri sheria, hilo ni jukumu la mhimili wa mahakama.”

Amesema, “Ndugai ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema? Nduagi ni mamlaka ya rufaa ya wabunge wanaoadhibiwa na vyama vyao? Kama yote hayo, jibu lake kuwa siyo, anapata wapi uhalali wa kuhoji mamlaka ya Kamati Kuu ya chama chetu na kutaka kupewa muktasari wa vikao?”

Msigwa anasema, “alipopelekewa hayo majina na Mdee na wenzake, wakati tayari katibu mkuu Mnyika, alishasema hatujapeleka majina NEC, mbona hakuuliza muhtasari wa kikao? Hii ni double standard (ndumi la kuwili) ya moja kwa moja na kwa bahati mbaya, inafanywa na kiongozi wa mhimili,” anaeleza kwa uchungu mwanasiasa huyo.

Kwa mujibu wa Msingwa, hamshangai Spika Ndugai kwa kuwa siyo mtu anayeheshimu utawala wa sheria na mwenye kusimamia misingi ya demokarasia nchini.

Anasema, “ni bahati mbaya sana, wabunge wa CCM (Chama Cha Mapinduzi), hawana nguvu ya kufanya maamuzi. Ndugai, hapaswi kuwa kiongozi wa mhimili wa Bunge, hata kwa siku moja. Katiba inaeleza wazi, kwamba mbunge atatokana na chama cha siasa. Anaowaita Ndugai wabunge na kuwaambia wasiwe na wasiwasi, wamefukuzwa na chama wanachodai, kimewapeleka bungeni.”

Anasema, “kuendelea kuwang’ang’ania, ni uvunjifu wa Katiba ya nchi. Nakuambia hivi, hilo tutaendelea kulipigia kelele hata Ndugai akiondoka duniani. Bunge linaongozwa na mtu mbinafsi, asiyetafiti na asiyefuata Katiba ya nchi na sheria zake. Kwa kweli, ni vigumu sana kwa taifa hili, kupata maendeleo, ikiwa mmoja wa mhimili wake, unaongozwa na mtu wa aina hii.”

Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, kundi hilo la wabunge 19, lililopachikwa jina la Covid 19, lilifukuzwa uanachama baada ya kutuhumiwa na kupatikana na makosa mbalimbali yakiwamo usaliti, kughushi nyaraka za chama na uchonganishi.

Mchungaji Peter Msigwa

Makosa mengine, ni kutengeneza migogoro, upendeleo, ubinfasi, kuhujumu chama, kushirikiana na wanaokitakia mabaya chama, udanganyifu na kujipeleka bungeni kujiapisha kuwa wabunge wa viti maalum, kinyume na maelekezo ya chama.

Aidha, Kamati Kuu ya Chadema, iliridhika kuwa viongozi wakuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), wakiongozwa na Mdee na aliyekuwa katibu mkuu wake, Grace Tendega, walikuwa vinara wa mkakati huo wa usaliti.

Mbali na Mdee na Tendega, wengine waliofukuzwa uanachama wa Chadema, kufuatia tuhuma hizo, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa makamu mwenyekiti (Bara), Hawa Mwaifunga na aliyekuwa katibu mwenezi wa baraza hilo, Agnesta Lambat.

Katika orodha hiyo, wapo pia aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, Asia Mwadin Mohamed; aliyekuwa naibu katibu kuu wa Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine, ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Hatua ya Spika Ndugai kueleza Bunge, kuwa amepokea barua ya Chadema, lakini amegoma kuifanyia kazi kwa vile, ni “kama kipeperushi,” inatofautiana na ile iliyotolewa na naibu wake, Tulia Ackson Mwansasu, alieleza kuwa Bunge halijawahi kupokea barua ya kuwavua unachama Mdee na wenzake.

Dk. Tulia alitoa kauli hiyo, kujibu maelezo ya Kishoa, aliyesema kuwa yeye na wenzake 18, siyo wanachama wa Chadema, na kwamba suala lao wamelipeleka Baraza Kuu kwa hatua zaidi.

Akizungumzia uhalali wa Kamati Kuu ya Chadema, Spika Ndugai alisema, “ni lazima nijiridhishe, hawa wajumbe wa kamati kuu waliokaa ndiyo hawa? Hawa waliotuhumiwa walipata muda wa kusikilizwa? Nafukuzaje watu ambao hawakusikilizwa kokote…”

Tofauti na anavyolivalia njuga suala la Mdee na wenzake 18 kwa maelezo kuwa hawajasikilizwa, Spika Ndugai, aliwondoa bungeni, wabunge nane wa Chama cha Wananchi (CUF), waliodaiwa kufukuzwa uanachama na Prof. Ibrahim Lipumba, katikati ya mgogoro uliokuwa umekikumba chama hicho.

Hata barua ya kuwafuta uanachama wabunge hao, iliandikwa na Prof. Lipumba, huku Spika Ndugai, akikatalia kuwafukuza bungeni, Magdalena Sakaya na Mafftah Nachuma, ambao barua ya kuwafuta uanachama, iliandikwa na Katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad.

Hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa Spika Ndugai, aliomba muhtasari wa vikao vya Lipumba kuwavua uanachama wabunge hao. Wala Spika hakutaka maelezo kutoka kwa wabunge wenyewe, kama afanyavyo kwa Mdee; na au hakusubiri maamuzi ya shauri ambalo wabunge hao walifungua kwenye baraza kuu na mahakamani.

Vilevile, Spika Ndugai, hakuwahi kuomba kupatiwa mihtasari ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM, baada kufukuzwa uanachama kwa aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum na mwenyekiti wake wa Umoja wa Wanawake (CWT), Sophia Simba.

Taarifa iliyotolewa na ofisi yake, tarehe 26 Julai 2017, ilieleza kuwa “Spika Job Ndugai ameridhia kufutwa uanachama kwa wabunge hao na hivyo nafasi zao ziko wazi.”

Prof. Lipumba alitangaza kuwafuta uanachama wabunge wanane na Madiwani wawili kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya kinidhamu, kukihujumu chama, kumkashifu na kumdhalilisha mwenyekiti.

Spika Ndugai alisema, amejiridhisha kuwa wabunge hao wamefutiwa uanachama kulingana na taratibu za chama hicho na hivyo hawana sifa za kuendelea na ubunge.

“Hivyo kwa mamlaka aliyonayo kwa kuzingatia kifungu cha 67(1)(b) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 1977, kikisomwa pamoja na kifungu 37(3) cha Sheria ya Uchaguzi Sura ya 343 kama ilivyojadidiwa mwaka 2015, Spika ametangaza nafasi hizo kuwa wazi na kumuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, aendelee na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa mujibu wa Sheria,” ilieleza taarifa hiyo.

Waliovuliwa ubunge, walikuwa ni Severina Silvanus Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohemed Mwassa, Riziki Shahari Mngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Ally al Kassmy na Halima Ali Mohamed.

Ndugai alifanyia kazi barua zote za CCM na CUF, bila kuhoji maamuzi ya vikao vilivyoamua kuwafutia uanachama wabunge wake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

error: Content is protected !!