Friday , 29 September 2023
Home Kitengo Habari Siasa Prof. Safari: AG anaweza kutenda jinai
SiasaTangulizi

Prof. Safari: AG anaweza kutenda jinai

Spread the love

MBOBEZI wa sheria nchini na Wakili wa Mahakama Kuu, Prof. Abdallah Safari amesema, iwapoDk. Adelardus Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), atagoma kutekeleza hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, atakuwa ametenda jinai. Anaripoti Hamis Mguta….(endelea).

Akizungumzia hukumu hiyo iliyopiga marufuku wakurugenzi wa halmashauri na manispaa kusimamia chaguzi amesema, serikali inayo nafasi ya kukata rufaa lakini si kuzuia hukumu hiyo kutekelezwa.

“AG mimi ninamuheshimu, namkubusha apitie kesi ya rufani No. 44 mwaka 2009, apitie hii kisi ataona kwamba, kukifanyika uchaguzi mwaka 2019, wakurugenzi hawawezi kusimamia.

“Na wakikataa, watakuwa wanafanya vitu viwili kwamba, wanaidharau mahakama au wanakataa kutekeleza amri halali ya mahakama. Haya yote ni makossa ya jinai,” amesema Prof. Safari.

Mwanasheria huyo mbobezi akizungumzana MwanaHALISI ONLINE ofisini kwake leo tarehe 24 Mei 2014 amesema, hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam haiwezi kuzuiwa kutekelezwa kama ambavyo mwanasheria mkuu alivyosema.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Bob Chacha Wangwe, ilitolewa hukumu tarehe 10, Mei 2019 na mahakama hiyo ikieleza kuwa, kifungu cha 7 (1) kinachompa mamlaha mkurugenzi kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kifungu cha 7(1), kinapingana na Katiba ya nchi.

Mahakama hiyo ilieleza kuwa, kifungu hiyo kinakinzana na Katiba ya nchi Ibara za 21(1), (2) na ya 26(1), kuhusiana na ushiriki katika shughuli za uchaguzi na kutii na kufuata Katiba na sheria.

Hukumu hiyo ya kihistoria ilitolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Firmin Matogolo, Dk Atuganile Ngwala na Dk Benhajj Masoud kwenye kesi hiyo ya kikatiba No 17, ya mwaka 2018.

Hata hivyo, Prof. Safari amesema, sio mara ya kwanza watu kuishitaki serikali kuhusu mambo ya uchaguzi baada ya vyama vingi kuruhusiwa mwaka 1992 na kwamba, kesi ya Christopher Mtikila ndio ilikuwa maarufu kuliko kesi zote.

“Mtikila aliishitaki serikali baada ya kukataa kuwepo kwa mgombea binafsi kwa kuwa ilikuwa ikikiuka ibara ya 21 ya Katiba ya nchi. Jaji rugakingira ni miongoni mwa majaji wazuri waliotoa hukumu ile kwamba, kweli inakiuka katiba.

“Hukumu ile aliisifu sana Nyerere (Mwal. Julius Nyerere) katika moja ya hotuba zake alizotoa kwenye sikukuu ya wafanyakazi Mbeya, ilikuwa mwaka 1992 au 93 hivi,” amesema Prof. Safari na kuongeza:

“Lakini AG wa wakati ule hakukata rufaa, walichofanya ni kubadilisha Katiba kwamba, mgombea lazima atokane na chama. Uamuzi huo ulimsikitisha sana Mwalimu Nyerere kwa kuwa ilikuwa kama kuihujumu mahakama,” amesema.

Prof. Safari amesema, pamoja na kubadilisha kipengele hicho, Mtikila alirudi tena kukatia rufaa kipengele hicho akitaka kiondolewe.

“Walisikiliza majaji watatu akiwemo Jaji Bashite Mihayo, ingawa hukumu iliyotolewa na akina Paramagamba Kabudi ambaye aliitwa kuishauri mahakama, waliandika hukumu ambayo iliwashangaza watu wengi sana.

“Pamoja na hukumu hiyo kuonekana kuwa ya ajabu, bado ilitamka kuwa, uamuzi ukishatolewa na mahakama basi ni lazima utekelezwe mara moja. AG asome hukumu hii kama hajaisome,” amesema.

Fatma Karume, Rais Mstaafu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) amesema kuwa, watakutana mahakamani na AG, ni baada ya kueleza dhamira yake ya kukatia rufaa hukumu hiyo.

Akizungumza kwenye kongamano la taasisi ya Change Tanzania leo jijini Arusha Fatma amesema, hukumu ya Mahakama Kuu ina maana kubwa kwa mustakabali wa demokrasia nchini.

Amesema kwamba, hatua ya AG kueleza nia ya kukata rufaa ni shinikizo la kisiasa na kwamba, hukumu hiyo ni ushindi dhidi ya bao la mkono.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za SiasaTangulizi

Chande aliyeng’olewa TANESCO kwenda TTCL apelekwa Posta

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua aliyekuwa, Mkurugenzi Mkuu wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme wang’oa vigogo TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amewahamisha waliokuwa vigogo wa...

Habari MchanganyikoTangulizi

Mgogoro wa ardhi Kiteto: Wakulima wadaiwa kutwanga risasi ng’ombe wa wafugaji Kiteto

Spread the loveMGOGORO kati ya wafugaji na wakulima katika Kijiji cha Lembapuli,...

error: Content is protected !!