May 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Safari afurahia Kiswahili kutumika mahakamani, atahadharisha

Spread the love

 

PROF.  Abdallah Safari, wakili wa Mahakama Kuu nchini Tanzania na gwiji wa sheria za jinai katika Afrika Mashariki anasema, ni uamuzi sahihi kwa Mahakama nchini kutumia lugha ya Kiswahili. Anaripoti Yusuph Katimba, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, mjadala wa kutumia Kiswahili kuendeshea kesi mahakamani; na au kuandika hukumu, haukuanza leo. Anasema, ulianza tokea wakati wa utawala wa Rais Benjamin William Mkapa, “lakini baadhi ya watu waliupuuza.”

“Huu mjadala ulianza zamani sana, mimi binafsi niliandika hadi kitabu kinachoitwa, ‘Mashtaka ya Jinai na Utetezi,’” anaeleza Prof Safari na kuongeza, “katika ukurasa wa wa 94 nazungumzia lugha ya Mahakama, kwamba kulikuwa na matatizo ya kutumia Kingereza mahakamani.”

Amesema, hata sheria za kimataifa zinataka Mahakama ziendeshe shughuli zake kwa lugha zinazoeleweka, akieleza kuwa lugha inayoeleweka, ni lugha ya kitaifa.

Prof. Safari ametoa kauli hiyo, siku moja baada ya Rais John Magufuli, kuagiza wizara ya Katiba na Sheria, kuanza mchakato wa kutumia Kiswahili mahakamani.

Rais Magufuli alitoa maelekezo hayo, wakati akimuapisha Jaji Zepharine Galeba, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma na kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Jaji Galeba amepandishwa hadhi hiyo, kutokana na uamuzi wake wa kutumia lugha ya Kiswahili katika kuandika hukumu ya moja ya kesi mahuhuri katika eneo la Kanda ya Ziwa Victoria.

Kesi ambayo Jaji Galeba aliandika hukumu kwa Kiswahili, inatajwa kuwa ni Na. 23/2020, iliyofunguliwa na kampuni ya mgodi wa madini wa North Mara dhidi ya Gerald Nzumbi.

Hata hivyo, Prof. Safari amesema, ili utekelezaji wa agizo la utumiaji wa Kiswahili kwenye Mahakama liweze kutekelezwa, ni sharti kutafsiriwe sheria zote muhimu pamoja na kuandaliwa kanuni za sheria za Kiswahili.

Anasema, “…wakati Kenya wanatambua kwenye Katiba yao, kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa, Katiba ya Tanzania, haijatambua kama Kiswahili ni lugha ya taifa, wala hakuna sheria yoyote inayotambua hivyo.

“Kilichopo Tanzania, ni mazoea tu; kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa, hivyo ni sharti kufanyie mabadiliko ya sheria nyingine, ili kuruhusu hilo kutendeka.”

Aidha, Prof. Safari anaeleza kuwa pamoja na sheria zote za kimataifa kuekeleza mahakama kufanya shughuli zake kwa lugha inayoeleweka, na kwa Tanzania Kiswahili ndio lugha ya taifa, lakini hakuna kokote ambako sheria ya Tanzania zinasema, “Kiswahili ndio lugha ya taifa.”

Anasema, haya aliyaeleza miaka mitano iliyopita, wakati wa kongamano lililoshirikisha vyombo vya habari karibu vyote duniani, lakini hakuna aliyemsikiliza.

Prof. Safari anaonya pia kuwa ni vema, kazi ya kutafsiri sheria, ikafanywa na watu wanaojua vema lugha ya Kiswahili na wenye mapenzi na lugha hiyo.

Anasema, “kuna kazi kubwa mbele katika kutafsiri sheria hizo; na sheria za msingi lazima zianze kutafsiriwa sasa, vinginevyo kutasababisha mkanganyiko kwa majaji.”

Prof. Safari ambaye amewahi kuwa mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Kurasini jijini Dar es Salaam anaeleza kuwa alichoeleza Rais Magufuli kinateleza, lakini sharti juhudi zifanyike katika kuhakikisha sheria kadhaa zinafanyiwa marekebisho.

Amesema, “kwa sheria zilivyo sasa, kuanzia mahakama ya wilaya, lazima kumbukumbu ziwekwe katika lugha ya Kingereza. Mahakama Kuu halikadhalika, Mahakama ya Rufaa ndio usiseme, kwa hiyo, huwezi ukaepuka.  Majaji kwa mujibu wa sheria, lazima waandike rekodi zao kwa Lugha ya Kingereza.”

Ametaka kazi ya kutafsiri sheria kutoka Kiingereza kwenda kwenye Kiswahili, ifanywe na watu wanaojua Kiswahili vizuri sana, na ambao Kiswahili ndio lugha yao ya kwanza.

“Nasisitiza Kiswahili kiwe lugha yao ya kwanza, na wawe na utamaduni wa kutumia Kiswahili. Halafu wafanye kazi na wanasheria ambao wanakipenda Kiswahili na hasa waliokwenda mahakamani. Sizungumzii wanasheria wa Chuo Kikuu. Nazungumzia wanasheria waliokwenda mahakamani na wakaona matumizi yake,” anaeleza.

Anaongeza, “wanasheria wa chuo kikuu sina matatizo nao, lakini tunahitaji watu waliokwenda mahakamani wakaona ugumu wake, sio wale wanaofundisha kwenye vyuo, hao achana nao. Tutafute mawakili au mahakimu ambao wapo kwenye kazi hizo kila siku.”

Akieleza kwa njia ya kufundisha mwanafunzi wake darasani, Prof. Safari amesema, wapo walioandika makala nyingi kuhusu umuhimu wa matumizi ya Kiswahili mahakamani.

Ametolea mfano, Prof. Bataza Rwezaura, aliyekuwa mwalimu wake katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuwa alieleza kwa undani umuhimu wa matumizi ya Kiswahili katika mahakama zetu.

          Soma zaidi:-

Anaongeza, “pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati ule miaka ya 68, University of Collage iliandikwa makala inaitwa, ‘Swahili Legal Terms.’ Hii kazi ilifanywa na Prof. Weston, alikuwa mkuu wa Kitivo cha Sheria, huyu alikuwa Muingereza.

“Katika anga ya kimataifa, Kiswahli kinatumika, Katiba inayoanzisha Mahakama ya ICC (Mahakama ya Uhalifu wa Kijinai) inaitwa, Roma Startout.’ Lakini ilitafsiriwa kutoka Kingereza kwenda lugha nyingine. Wakasema, lazima itafsiriwe katika lugha ya Kiswahili, mimi nikawa mhariri mkuu,” anasimulia.

Prof. Safari anaendelea kueleza kuwa hata kesi maarufu  ya Rajabu Dibagula aliyesema, “Yesu si Mungu” mwaka 2003, kutokana na umuhimu wa hukumu yake baada ya kukata rufaa, Jaji Barnabas Samatta ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, aliagiza hukumu hiyo, itafsiriwe kwa Kiswahili ili isomwe kwa upana wake.”

Prof. Safari anasema, “Jaji Samatta hakuishia hapo. Mara baada ya kutoka hukumu, kwa kuona umhimu wake, akaagiza ifanyiwe tafsiri, na ilivyotolewa hii (ya Kiswahili), Jaji Samata akamuelezea msajili wake aliyenipigia simu mimi, kwamba wapelekewe wale masheikh.”

Amesema, alichokiona Rais Magufuli kuhusu matumizi ya lugha ya Kiswahili mahakamani, umuhimu wake ulionekana miaka mingi mingi iliyopita na Jaji Samatta alishaanza kutekeleza, hata kama halikuwapo kwa mujibu wa sheria.

“Kimsingi anachokisema Magufuli, watu waliishakiona tangu zamani, tatizo lake ni utekelezaji,” ameeleza Prof. Safari.

error: Content is protected !!