June 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Ndulu: Uchumi wa Tanzania unazidi kukua

Prof. Benno Ndullu

Spread the love

WAKATI wachambuzi wa masuala ya masuala ya kisiasa na kiuchumi wakielezea kuporomoka kwa uchumi na kuongezeka kwa ugumu wa maisha hapa nchini, Profesa Benno Ndulu, Gavana wa Benki Kuu amesema hali ya ukuaji wa uchumi ni ya kuridhisha, anaandika Pendo Omary.

Prof. Ndulu amesema, takwimu kutoka Ofisi ya Taifa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2016, ukuaji wa Pato la Taifa unakadiliwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.7 kipindi kama hicho mwaka 2015.

Amezitaja shughuli zilizochangia ukuaji wa uchumi kwa kiasi kikubwa kuwa ni; kilimo, biashara, uchukuzi, sekta ya fedha na mawasiliano huku akieleza kuwa shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kasi katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni sekta ya fedha (asilimia 13.5), mawasiliano (asilimia 13.4) na utawala wa umma (asilimia 10.2).

“Uzalishaji wa umeme nchini katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016 umeongezeka kwa asilimia 14.5 kufikia kWh milioni 3,454.2 ikilinganishwa na kWh milioni 3,016.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2015,” amesema Prof. Ndulu.

Aidha amesema uzalishaji wa saruji katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 umeongezeka kwa asilimia 7 na kufikia tani elfu 725.4 ikilinganishwa na tani elfu 680.1. Hali hiyo imechangiwa na ongezeko la uzalishaji wa kampuni ya Dangote ambayo yenye uwezo wa kuzalisha tani 3 Milioni.

Kuhusu mfumuko wa bei, amesema “katika miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016 umeshuka hadi kufikia asilimia 5.5 mwezi Juni 2016 na asilimia 4.9 mwezi Agosti 2016 kutoka asilimia 6.8 Desemba 2015.

“Wastani wa mfumuko wa bei usiojumuisha bei za vyakula na nishati ambao ni kiashiria sahihi zaidi cha utekelezaji wa sera ya fedha, umeendelea kubaki katika viwango vya chini wastani wa asilimia 2.8,” amesema Prof. Ndulu.

Amesema ongezeko la fedha taslimu, ambacho ni kipimo cha ukwasi kwenye uchumi limeendelea kubakia ndani ya malengo katika kipindi chote cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2016.

“Mikopo mingi kwa sekta binafsi ilielekezwa kwenye shughuli za biashara kwa wastani wa asilimia 19.0, uzalishaji wa viwandani wastani wa asilimia 10.6, uchukuzi na mawasiliano wastani wa asilimia 7.9 na shughuli za kilimo asilimia 7.8,” ameeleza Prof. Ndulu.

Pia amefafanua kuwa katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya mwaka 2016 Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati ya Sh. 2,180 hadi 2,190 kwa dola moja ya Marekani akisema kufikia mwezi Juni 2016, kulikuwa na jumla ya benki na taasisi za fedha zinazosimamiwa na Benki Kuu zipatazo 65 zenye matawi 739 nchini.

Kiwango cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekwa kilikuwa asilimia 17.7 kikilinganishwa na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria cha asilimia 12.0.

Akizungumzia deni la taifa, Prof. Ndulu amesema deni la taifa limeendelea kuongezeka na kufikia dola za Kimarekani 20,851 Milioni mwisho wa mwezi Juni 2016 kutoka dola za Kimarekani 19,861 Milioni mwezi Desemba 2015.

“Asilimia 83.4 ya deni la nje ni deni la serikali na tasisi za umma. Pamoja na ongezeko hilo, takwimu zinaonyesha kuwa deni letu bado ni stahimilivu. Kwa mfano, deni la nje kwa thamani ya sasa ni karibu asilimia 20 ya pato la taifa, ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50 ya pato la taifa.

Deni la ndani liliongezeka kufikia Sh. 10,038.4 bilioni mwishoni mwa mwezi Juni 2016 na kukopa Sh. 8,597.0 Bilioni mwezi Desemba 2015. Ongezeko hilo lilitokana na serikali kukopa kupitia dhamana na hati fungani kwa ajili ya kugharamia bajeti ya serikali kwa mwaka 2015/2016, ikilinganishwa na kupungua kwa misaada na mikopo kutoka nje,” amefafanua Prof. Ndulu.

 

error: Content is protected !!