Friday , 29 March 2024
Home Gazeti Habari Prof. Ndulu, gavana atakayekumbukwa kwa mengi
HabariTangulizi

Prof. Ndulu, gavana atakayekumbukwa kwa mengi

Spread the love

 

ALIYEKUWA Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndullu (71), amefariki dunia. Prof. Ndullu, alizaliwa tarehe 23 Januari 1950. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Prof. Ndulu alichukua hatamu za uogozi wa BoT, kutoka kwa Dk. Daud Balali, tarehe 8 Januari 2008, baada ya Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, “kuridhia gavana huyo kujiuzulu.”

Dk. Balali, alijiuzulu ugavana, kufuatia hatua ya benki hiyo ya umma, kujitumbukiza katika kashifa za ufisadi, ikiwamo ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi kutoka Akaunti ya Fedha za kigeni (EPA) na majengo yake pacha.

Aliyekuwa Gavana wa BOT, Marehemu Dk. Daud Balali

Kashfa hiyo iliyotikisa nchi, wahusika walitajwa kutumia vivuli vya siasa kupitisha nyaraka bila kufanyiwa uhakiki.

Ilimalizika kwa baadhi yao kufikishwa mahakamani na wengine ambao hawakutajwa kusamehewa na Rais Kikwete wakidaiwa kurejesha fedha walizoiba.

Katika kipindi hicho, yalipofanyika mabadiliko ndani ya baraza la mawaziri aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakia Maghji hakurudi.

Alipofika BoT, Prof. Ndulu, alifanya kazi kubwa ya kusimamia ukuaji wa uchumi, kuzuia mfumuko wa bei na kupunguza nakisi ya fedha za kigeni, katika kipindi ambacho taifa lilianza ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu.

Kwa mfano, mfumuko wa bei ulishuka kutoka asilimia 7 kwa mwaka, hadi kufikia asilimia moja, Desemba mwaka 2011.

Rais Mstaafu Jakaya Kikwete

Hata hivyo, nuru ya Prof. Ndulu, ndani ya BoT na kwa umma, ilianza kufifia pale benki hiyo, iliporuhusu; na au kunyamazia ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow.

Katika sakata hilo, kiasi cha Sh. 321 bilioni, zilikwapuliwa ndani ya BoT, kati ya Septemba na Novemba mwaka 2013.

Mabilioni ya shilingi yalilimbikizwa na Tanesco, katika akaunti hiyo, baada ya kuibuka mgogoro juu ya malipo ya gharama ya uwekazaji wa mitambo na gharama za kuweka mitambo (Capacity Charge), kati ya IPTL na shirika la umeme la taifa (TANESCO).

Kampuni ya IPTL – Independent Power Tanzania Limited – ilikuwa inamilikiwa na makampuni mawili – MECHMAR ya Malaysia na VIP Engineering and Marketing Limited.

VIP ilikuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa katika kampuni ya kigeni ya IPTL na MECHMAR inamiliki asimilia 70 ya hisa.
Kampuni hayo mawili, kupitia IPTL walijifunga katika mkataba na serikali wa miaka 20 wa kuzalisha megawati 100 za “umeme wa dharura” na kisha kuuza umeme huo kwa TANESCO.

Mabilioni hayo ya shilingi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika akaunti ya Escrow yalichotwa kwa msaada mkubwa wa viongozi wakuu wa serikali na kile kilichoitwa, “amri ya mahakama.”

Katika ripoti ya uchunguzi maalumu wa mabilioni hayo ya fedha na ripoti kuwasilishwa kwenye mkutano wa Bunge wa 16/17, maazimio yaliyofikiwa 29 Novemba mwaka 2014, ulisababisha mawaziri, mwanasheria mkuu wa serikali, Fredrick Werema na wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge kujiudhuru nyadhifa zao.

Frederick Werema, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mawaziri waliong’oka kutokana na sakata hilo ni, Profesa Anna Tibaijuka aliyekuwa waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi na Profesa Sospeter Muhongo wa nishati na madini.

Wabunge waliovuliwa nyadhifa zao ni; Andrew Chenge (Bajeti- Bariadi Magharibi), William Ngeleja (Katika, Sheria na Utawala-Sengerema), Victor Mwambalaswa (Nishati na Madini-Lupa).

Taarifa zinasema, Prof. Benno Ndulu, aliyekuwa gavana wa BoT, alichukua tahadhari zote juu ya fedha hizo, ikiwamo kumjulisha aliyekuwa Waziri wa Fedha, umuhimu wa kumjulisha Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu malipo hayo.

Gavana alikwenda mbali zaidi. Alitaka kupata uhakika kwamba utekelezaji wa uamuzi wa mahakama, pamoja na makubaliano ya kukabidhi fedha, unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Rais na Waziri Mkuu.

Aidha, BoT ilihakikisha mahitaji yote ya msingi kama vile, makubaliano ya kuhamisha fedha, kinga dhidi ya madai au mashitaka baada ya malipo, na suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT), vinapata ufafanuzi, baraka na mwongozo unaostahili.

BoT iliamua kuchukua hatua hizo ili kujinasua na madai mapya ambayo yangeweza kuibuka baada ya fedha kuhamishwa kutoka benki.

Kile ambacho BoT haikukifanya, ni kufanya uhakiki wa uhamishaji wa hisa kutoka Mechmar kwenda PAP; bila PAP kusajili hisa zake nchini; bila PAP kuthibitisha kujisajili Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC); na bila kuwa na hati ya mlipa kodi (TIN).

Mpaka sasa, mgogoro huo bado haujaisha, kufuatia MECHMAR ilikuwa inasisitiza na mpaka sasa, bado inasisitiza, kuwa mtambo wa IPTL uliyopo eneo la Tegeta, Salasala, jijini Dar es Salaam, ni mali ya Benki ya Standard Chartered ya Malaysia.

Benki ya Standard Chartered ilikuwa inadai na mpaka sasa bado inadai kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow, ni mali yake.

Inadai kuwa kampuni ya MECHMAR ya Malasia ilishindwa kurejesha mkopo iliochukua benki na kwamba hilo ni jambo linalosababisha mitambo ya IPTL iliyopo Tegeta Salasala, jijini Dar es Salaam, kuwa mali yake.

Standard Chartered inaeleza kuwa ilikabidhiwa mamlaka ya kumiliki, kusimamia na kuendesha, mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na mahakama, kufuatia MECHMAR kushindwa kulipa mkopo.

Mkataba huo ulipa benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.

Benki ya Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni zinazotokana na mkopo pamoja na riba.

Nje ya madai haya, ambayo kwa kiasi kikubwa yaliyotokana na mashinikizo ya wakubwa zake, Prof. Benno Ndulu, anabaki kuwa mmoja wa magava bora na wachumi mahiri ndani na nje ya Tanzania.

Alikuwa gavana wa BoT, kwa miaka kumi, kuanzia mwaka 2008 hadi Januati 2018 nafasi yake alipoteuliwa Profesa Florens Luoga, ambaye alikuwa mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Florens Luoga

Alfajili ya Jumatatu 22 Februari 2021, Profesa Ndulu, alihitimisha safari yake hapa duniani akiwa Hospitali ya Kairuki, jijini Dar es Salaam, akipatiwa matibabu.

Mwenyezi Mungu amlaze pema, pemoni. Amina

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Zuma akataliwa kugombea urais

Spread the love  TUME Huru ya Uchaguzi Afrika Kusini (IEC) imemwondoa rais...

Habari za SiasaTangulizi

CAG: Wastaafu, wenza wao chanzo NHIF kufilisika

Spread the loveRIPOTI ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu...

Habari za SiasaTangulizi

Vikundi hewa 851 vyalamba bilioni 2.6 mikopo ya halmashauri

Spread the loveVIKUNDI hewa vya wajasirimali wadogo 851 kutoka katika halmashauri 19...

Habari za SiasaTangulizi

Mashirika matano yapata hasara mabilioni ya fedha

Spread the loveMASHIRIKA matano ya Serikali yanayojiendesha kibiashara, yamepata hasara ya mabilioni...

error: Content is protected !!