January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Mwandosya, Wassira wachukua fomu kwa tambo

Mawaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Profesa Mark Mwandosya (kulia) na Waziri wa Kilimo na Ushirika, Steven Wasira (kushoto) wakiteta na Kiongozi wa Upinzani Bugeni, Freeman Mbowe

Spread the love

MAWAZIRI wawili katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete- Stephen Wassira (Kilimo, Chakula na Ushirika) na Prof. Mark Mwandosya (Ofisi ya Rais-Kazi Maalum), wamekuwa makada wa mwanzo kuchukua fomu za kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu. Anaandika Dany Tibason … (endelea) .

Kama ambavyo wamejinadi wakati wakitangaza nia, makada hao kwa nyakati tofauti baada ya kukabidhiwa fomu hizo katika ofisi za Makao Makuu ya CCM- Dodoma, walizungumza na waandishi wa habari ambapo Prof. Mark Mwandosya ameahidi kukomesha vitendo vya rushwa huku Wassira akiahidi kufufua uchumi wa viwanda na kilimo ili kuondokana na jembe la mkono. 

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Prof. Mwandosya ambaye aliambatana na mkewe Lucy, amesema mbali na kukomesha vitendo vya rushwa na ufisadi, pia amejinadi kuwa atahakikisha anaufanya uchumi wa Tanzania kuwa sawa na Bara la Ulaya.

Amesema kuwa, amelazimika kuomba ridhaa ya Watanzania kwa ajili ya kuliongoza Taifa ambalo kwa sasa linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwa ni kutokana na umasikini ambao umekithiri.

Prof. Mwandosya amesema katika vipaumbele vyake ni lazima kuwa na uchumi ambao utamwezesha kila mtanzania kuona anafaidi rasilimali za nchi.

“Tumeuona uchumi wa Ulaya, Asia na Marekani ulivyo mkubwa na sasa Afrika kuna uwezekano mkubwa katika kipindi cha miaka 2025 au 2050 tukawa na uchumi kama wa nchi hizo na tukaongoza kwa uchumi katika Bara la Afrika.

“Katika kuinua uchumi natamani ifikapo kwaka 2025 au 2050 tukawa na uchumi imara katika dunia ya sasa kutokana na kuwa na rasilimali nyingi ambazo nchi inazo kama vile mafuta, gesi, mbuga na hifadhi pamoja na vyanzo vingine vya mapato ya ndani,”amesema.

Ameongeza kuwa “tukiimarisha uchumi ni wazi kuwa tutaondokana na suala la kuomba misaada kutoka katika mataifa mengine jambo ambalo linaweza kusababisha kuwepo kwa misaada yenye masharti magumu”.

Mbali na hilo, amedai kuchukizwa na sera za watangaza nia kuchafuana na kusemana huku wakiendelea kukisema vibaya chama chao pamoja na serikali.

 Wassira

Baada ya kukabidhiwa fomu yake, Wassira amewaeleza waandishi wa habari kuwa, anaamini ikiwa ataingia Ikulu na vipaumbele vyake, atahakikisha anafufua uchumi wa viwanda na kilimo ili kuondokana na jembe la mkono na badala yake kulima kilimo cha kisasa.

Amesema kuwa, katika hatua nyingine ya kukuza uchumi, atawekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea kilimo cha mvua ambacho wakati mwingine kinaweza kusababisha kutokuwepo kwa chakula cha kutosha.

Kwa mujibu wa Wassira, iwapo kilimo cha umwagiliaji kitapewa kipaumbele, ni wazi kuwa kitapatikana chakula cha kutosha na kingine kwa ajili ya kuuza kwa nchi nyingine za nje na kupata fedha ya kigeni.

Amesema “nikiingia madarakani ni lazima nijue viashiria vya umasikini, kutatua matatizo ya ajira hususani kwa vijana kwa kuwawezesha kujiunga katika vikundi mbalimbali ili kuwawezesha kupata mitaji na kuweza kuzalisha ajira wao badala ya kusubiri kuajiriwa”.

Wassira ameeleza kushangazwa na jamii ambayo imekuwa na tabia ya kuwashangilia na kuwashabikia watu ambao wamekuwa wakifanya ufisadi na kuonekana kuwa watu hao ni hodari zaidi.

error: Content is protected !!