August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Mukandala: Nilishahamisha vitu vyangu ofisini

Prof. Rwekaza Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Spread the love

PROFESA Rwekaza Sympho Mukandala, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema alishakamilisha utaratibu wa kukabidhi ofisi yake kwa mtu mwingine kufuatia muda wake wa uongozi kumalizika mnamo tarehe 04 Desemba mwaka huu, anaandika Charles William.

Prof. Mukandala ameyasema hayo leo tarehe 05 Desemba kufuatia Rais John Magufuli kwa kushauriana na Dk. Jakaya Kikwete, ambaye ndiye Mkuu wa Chuo hicho kuamua kumuongeza muda wa mwaka mmoja katika nafasi hiyo ya juu zaidi katika uendeshaji wa kila siku wa chuo.

Akizungumza katika mahojiano maalum na MwanaHALISI Online jioni ya leo, Prof. Mukandala amesema, “Nimeupokea kwa mikono miwili na kwa faraja kubwa uamuzi wa Rais Magufuli na Dk. Kikwete ingawa tayari nilikuwa nimeshajiandaa kustaafu na nilikuwa nimeshawaaga watumishi wa UDSM.

Prof. Mukandala ambaye amekuwa Makamu Mkuu wa UDSM tangu mwaka 2006 ikiwa ni miaka 10 sasa amesema, alishaondoa vitu vyake binafsi ofisini tayari kwa kumpisha mteule mpya katika nafasi hiyo na pia alishawaomba wakuu wa Ndaki, Shule na Taasisi za chuo hicho wamsaidie kuandaa nyaraka za makabidhino.

“Nilishafanya maandalizi ya kumsimika mrithi wa nafasi yangu ndiyo maana hata wakati wa mahafali ya mwaka huu niliaga, hata hivyo nipo tayari kuendelea kuitumikia nafasi hii. Nitaendelea kuhakikisha chuo kinatoa wahitimu walio bora ndani na nje ya nchi,” amesema.

Akieleza sababu za kuongezewa kipindi cha mwaka mmoja, amesema kuna miradi mbalimbali ya chuo inayotakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja ambayo anatakiwa kuisimia.

“Ipo miradi mikubwa ya chuo ikiwemo ujenzi wa mabweni ya wanafunzi, ujenzi wa maktaba ya kisasa na mingineyo ambayo natakiwa kuisimamia katika kipindi hiki, tunamshukuru rais kwa kuunga mkono jitihada zetu za kuboresha miundombinu ya chuo,” amesema Prof. Mukandala.

Prof. Mukandala amekiri kuwa kipindi cha uongozi wake wa awamu ya kwanza (2006-2011) kilikuwa kigumu zaidi kutokana na migomo mikubwa na ya mara kwa mara ya wanafunzi na hivyo kusababisha hata chuo kufungwa mara kadhaa na hivyo kuathiri shughuli za kitaaluma.

“Ni kweli, miaka yangu mitano ya kwanza ilikuwa ya changamoto kubwa, migomo ya mara kwa mara ya wanafunzi ilikuwa ikitokea huku mingi ikisababishwa na tatizo la mikopo hata hivyo katika awamu ya pili nilijitahidi sana kutengeneza mfumo imara wa utatuzi wa migogoro hiyo.

“Tukatengeneza mfumo hapa chuoni pawe na idara maalum inayoshughulikia mikopo, mfumo ambao baadaye uliigwa na vyuo vingine, tukawa bega kwa bega na wanafunzi katika madai yao ikiwemo ya kuongezewa fedha za kujikimu na idadi ya wanufaikaji na hatimaye hali ikawa shwari kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Prof. Mukandala kwa sasa menejimenti ya chuo inayo utayari wa kusikilizana na wanafunzi huku wanafunzi wachache wasumbufu, wanaohatarisha amani ya chuo na wasiokubali maridhiano wala kuonywa wakithibitiwa kwa kusimamishwa au kufukuzwa.

“Miaka ya nyuma ilikuwa ikitokea vurugu chuo kinafungwa na wanafunzi wanarudi nyumbani, kipindi cha pili tukaamua tuanze kudhibiti wachache tu ambao wanachochea vurugu badala ya kuadhibu wanafunzi wote,” amesema.

Prof. Mukandala alizaliwa tarehe 30 Septemba mwaka 1953, huku akipata elimu yake ya juu UDSM, alipata Shahada ya Sanaa katika mahusiano ya kimataifa na utawala (1973 – 1976), kisha Shahada ya uzamili katika maendeleo ya utawala katika chuo hicho (1977) huku mwaka 1988 akipata shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Carlifornia, Marekani ambapo pia alitunukiwa tuzo ya Peter Odegard kama mwanafunzi wa kipekee zaidi wa shahada ya uzamivu katika chuo hicho.

error: Content is protected !!