MBUNGE wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo, amewataka wazazi watimize wajibu wao wa malezi mazuri kwa wanafunzi wa shule za sekondari, yatakayowawezesha kufaulu mitihani yao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Prof. Muhongo ametoa wito huo kupitia mapendekezo yake aliyotoa juu ya namna ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi baada ya shule za jimbo hilo kufanya vibaya katika mitihani ya kidato cha pili na cha nne.
“Wazazi watimize wajibu wao wa malezi mazuri ya watoto wao na wafuatilie kwa karibu sana mienendo na tabia zao kama kushinda kwenye runinga, kubeti, kamari na kucheza pool table. Wazazi watimize wajibu wao wa kuwanunulia watoto mahitaji ya shule na elimu kwa ujumla,” amesema Prof. Muhongo.
Mbunge huyo wa Musoma Vijijini, amewataka wazazi wanaowapa watoto wao shughuli za kiuchumi wawapo masomoni, waache mara moja kwa kuwa kitendo hicho kinasababisha watoto washindwe kusoma vizuri.
“Sera ya elimu bila malipo iendelee kufafanuliwa na wahusika ili wazazi waasiache kutimiza wajibu wao wa kuchangia upatikanaji wa elimu nzuri kwa watoto wao,” amesema Prof. Muhongo.
Katika hatua nyingine, Prof. Muhongo ameshauri walimu waongezewe mafunzo mara kwa mara, pamoja kuwepo kwa uwiano sawa wa usambazaji walimu katika shule za umma.
Aidha, ameshauri kitengo cha udhibiti ubora kiongezewe uwezo wa kufuatilia shughuli za ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
“Maslahi ya walimu yaboreshwe kwa kiwango kikubwa, yaani wajengewe nyumba za kuishi hasa wanaofundisha vijijini. Mishahara yao iboreshwe na makato yapunguzwe,” amesema Prof. Muhongo.
Leave a comment