MBUNGE wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, ameipongeza Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha kiasi cha Sh. 4.75 bilioni, kwa ajili ya usambazaji maji katika kata mbili zilizokuwa zimeachwa katika mradi wa Maji ya Boma la Mugango-Kiabakari-Butiama. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mara … (endelea).
Pongezi hizo zimetolewa na tarehe 6 Aprili 2023 na Prof. Muhongo, kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi yake ya Jimbo la Musoma Vijijini.
“Tunaanza kwa kutoa shukrani nyingi sana kwa Serikali yetu inayoongozwa vizuri na Rais wetu, Dk. Samia. Kata mbili zilizokuwa zimeachwa kwenye mradi wa Sh. 71.5 bilioni wa maji sasa zimepatiwa fedha za kujengewa miundombinu ya usambazaji wa maji kwenye kata hizo , hii ni zawadi ya Pasaka,” imesema taarifa hiyo.
Kupitia taarifa hiyo, Prof. Muhongo amesema wananchi waishio kwenye chanzo cha maji katika Kata ya Mugango na Tegeruka, watapata maji kupitia bomba hilo.
“Mkandarasi wa mradi huu wa kata mbili ameshapatikana na taratibu zote zimekamilika, kifuatacho ni utiaji saini, hafla itakayofanyika kijijini Mayani, Kata ya Tegeruka, tarehe 12 Aprili 2023. Viongozi mbalimbali wa chama na Serikali watakuwepo,” imesema taarifa hiyo.
Leave a comment