January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Muhongo aja kisayansi, aikana Escrow

Spread the love

PROFESA Sospeter Muhongo-Waziri wa Nishati na Madini aliyejiuzulu kwa kashfa ya uchotwaji wa mabilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow, ametangaza nia ya kuomba uteuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili agombee urais Oktoba mwaka huu, akijivunia uwezo wake na taaluma ya sayansi kwamba utaivusha nchini na kuipeleka kwenye uchumi wa kisasa. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Prof, Muhongo (61), ambaye ni mtaalamu wa miamba anayetambulika kimataifa, pia ameendelea kujitetea kwamba hakuchukua hata senti moja ya Escrow, hivyo hana sababu ya kujisafisha kwani hakuna popote alipotajwa katika ripoti.

“Angalieni kwenye ripoti sikutajwa, wala katika orodha ya majina ya waliopata mgawo kupitia mabenki ya Mkombozi na Stanibc, mimi simo, huwezi kujua labda aliyenisingizia alitaka kunizuia nisigombee urais. Mimi ndiye ninayefaa kuwa rais ajaye…sasa nanyie wananchi naomba muwasukume wanaoteua wanipitishe,”ametamba.

Akitangaza kuingia kwenye mchakato huo katika mkutano wake wa ndani mjini Musoma leo mchana, Prof. Muhongo alitumia muda mwingi kuchanganua takwimu za historia ya uchumi wa Tanzania ulipotoka hadi sasa huku akiulinganisha na mataifa mengine makubwa ya India, China na Brazil yaliyokuwa sawa na Tanzanaia.

Amesema hakuna haja ya kulaumiana bali kujipanga kwa kuweka mikakati imara ya kufika huko walikofika mataifa yaliyokuwa sawa na Tanzania kiuchumi miaka ya nyuma.

Prof. Muhongo ametamba kuleta mafanikio makubwa katika wizara ya nishati kwa muda ambao alikuwa  madarakani huku akipiga kijembe kwamba sasa umeme umeanza kukatika hovyo kama zamani wakati tatizo hilo alikwisha lipatia ufumbuzi.

Amesema kuwa, Tanzania na dunia kwa sasa inahubiri maendeleo ya sayansi na teknolojia na hivyo kutamba kwamba, yeye ndiye mwanasayansi pekee nchini na duniani anayeweza kuipeleka Tanzania katika uchumi mkubwa kwa kutumia sayansi.

Ameongeza kuwa kasi kubwa aliyoifanya kwenye wizara ya nishati katika sekta ya gesi na mafuta ni kubwa na kwamba ujenzi wa bomba la gesi ni hatua ya awali ya kupeleka nishati hiyo kwenye viwanda viweze kuzalisha wakati wote.

Lakini Prof. Muhongo amewataka wananchi kutokubali mapato ya gesi na mafuta yewekwe kwenye hazina ya serikali bali Bunge litunge sheria ya kuanzisha mfuko maalum ili fedha hizo ziwekewe utaratibu wa kuwakopesha wananchi ili kuwaepusha na kero ya mikopo ya mabenki yenye riba kubwa.

Ametaja mambo mengine ambayo atayapa kipaumbele kuwa ni vita dhidi ya rushwa kwa vitendo, elimu bora, ajira, huduma ya maji safi na salama, kero alizodai hakuna yeyote wa kuzitatua isipokuwa yeye.

“CCM ikinichagua mimi kuwania urais, nitahakikisha natenga bajeti kwa ajili ya kufanya utafiti wa elimu na vitu vingine vya maendeleo. Hakuna nchi iliyoendelea bila kufanya utafiti,” amesema Muhongo.

Kuhusu migogoro ya ardhi, amesema kinachohitajika ni teknolojia bora ya matumizi ya ardhi iliyopo na kwamba sio semina wa majadiliano.

error: Content is protected !!