July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Mbarawa kufungua kongamano la uchumi wa bluu

Spread the love

 

CHUO cha Bahari (DMI), kimewataka Watanzania kuchangamkia fursa ya mafunzo ya fani ya ubaharia kwa kuwa ina soko kubwa la ajira ndani ya nchi na mataifa mbalimbali duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu….(endelea)

Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Tumaini Gurumo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Kongamano la kwanza la mabaharia la uchumi wa bluu.

Kongamano hilo linalofanyika leo linafunguliwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na kuhudhuriwa na mabalozi wa nchi mbalimbali zenye bahari.

Aidha, Gurumo alisema ubaharia ni fani kama zilivyo fani zingine zenye heshima ambayo husomwa kwa vitendo na nadharia na hatimaye akifaulu anapata cheti na kupanda madaraja kama ilivyo kwa fani ziingine.

Alisema mafunzo yanayotolewa na DMI yana ithibati ya kimataifa na baharia anayefundishwa na chuo hicho anauwezo wa kufanya kazi ndani ya nchi na kwingine kote duniani kwani vyeti vyake vitakuwa vinatambuliwa kimataifa.

Kaimu Mkuu wa Chuo cha Bahari (DMI), Tumaini Gurumo, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa kimataifa kuhusu uchumi wa bluu

“Uhitaji wa mabaharia duniani bado ni mkubwa… wanahitajika wengi kwani nchi nyingi zina meli lakini hazina watenda kazi.

“Ukraine ilikuwa inatoa mabaharia wengi lakini katika kipindi hiki cha vita idadi ya mabaharia imepungua kwani wengi wapo huko nyumbani hivyo nafasi inazidi kuongezeka kwa mabaharia wa kitanzania

“Kuna fursa kubwa kwenye fani ya ubaharia nawaasa vijana, wazazi na walezi waitazame, fani hii, zamani ilionekana kama vile ya kihuni lakini leo hii imekuwa fani yenye uwezo wa kumuingizia mtu kipato kikubwa,” alisema Tumaini

Alisema dhumuni la kongamano hilo la siku mbili ni kupambanua fursa zinazopatikana kwenye uchumi wa bluu na baharini ili zitumiwe vyema na watanzania kwa maeneo ya nchi.

Alisema mpango wa maendeleo wa miaka mitano ulioanza mwaka 2021-2025 umeweka bayana kwamba uchumi wa bluu ni kipaumbele katika shughuli za kuendeleza uchumi wa Tanzania .

Alisema kongamano hilo pia litahudhuria Waziri wa Uchumi wa Bluu na Uvuvi wa Zanzibar ambaye atakuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu.

“Tutasikia Waziri wetu wa uchumi wa bluu anatuambia nini kuhusu fursa zilizopo kwenye uchumi wetu wa bluu hili ni kongamano la kwanza la uchumi wa bluu hivyo sio la kukosa na siku ya kufunga tumepata fursa ya kuwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda,” alisema Tumaini

error: Content is protected !!