August 18, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Mbarawa amtisha mkandarasi

Prof. Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Spread the love

PROFESA Makame Mbarawa, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ameitaka kampuni ya Beinjing Construction and Engineering Group (BCEG) ya China, inayofanya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza na jengo la kuongozea ndege kukamilisha kazi hiyo ndani ya miezi minane, anaandika Moses Mseti.

Kauli hiyo inakuja baada ya serikali kuilipa kampuni hiyo deni la Sh. 7.6 bilioni kwaajili ya upanuzi wa uwanja na ujenzi wa jengo hilo huku Prof. Mbarawa akidai kuwa mkandarasi huyo aliidanganya Serikali kuwa inadaiwa Sh. 18 bilioni.

“Baada ya kuchunguza tumebaini deni tunalodaiwa ni Sh. 7.6 bilioni ambalo lilipwa jana, sasa kama mkandarasi atashindwa kukamilisha ujenzi huu atachukuliwa hatua kama ifikapo Agousti mwakani atakuwa hajakamilisha na tutamtaka atulipe faini,” amesema Prof. Mbarawa.

Prof. Mbarawa yupo Mwanza katika ziara ya kikazi ambapo amesema kufuatia kusimama kwa ujenzi huo serikali haitomlipa fidia mkandarasi huyo kwani alipeleka baadhi ya vielelezo vilivyokuwa vya uongo na hivyo gharama za kutoendelea kwa ujenzi alizisabisha yeye mwenyewe.

“Niwahakikishie wananchi kuwa serikali inafanya jitihada kubwa katika ujenzi wa viwanja vya ndege hapa nchini kwa lengo la kuimarisha usafiri wa anga ili kuchochea ukuaji wa uchumi,” amesema.

Ameitaja mikoa ambayo viwanja hivyo vinajengwa kuwa ni pamoja na Mbeya, Shinyanga, Kigoma, Sumbawanga, Tabora, Songea, Mara na Iringa.

Ester Madale, meneja wa uwanja wa Mwanza amesema kuwa katika uwanja huo wamejitokeza ndege hai wanaohatarisha usalama wa ndege za anga na usalama wa raia na kudai kuwa hutumia Sh. 50 milioni kwa mwaka kwa ajili ya kuwalipa wafanyakazi wanaowafukuza ndege hai.

error: Content is protected !!