PROFESA Makame Mbarawa, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, amefanya mabadiliko katika Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika mikoa ya Tabora na Bukoba. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).
Taarifa ya mabadiliko hayo imetolewa leo tarehe 15 Julai 2019 na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba, Prof. Mbarawa amemteua Mhandisi Joel Rugemalila aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama, kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira mkoani Tabora.
Kwa upande wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kahama, Prof. Mbarawa amemteua Allen Marwa, aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba, kuwa mkurugenzi wake.
Wakati huo huo, Prof. Mbarawa amemteua aliyekuwa Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba, Mhandisi Clavery Casmir kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo.
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza kuwa, Prof. Mbarawa amefanya uteuzi huo baada ya kubaini changamoto mbalimbali za maji, alizoziona wakati ziara ya kikazi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Kagera.
Aidha, taarifa hiyo imebainisha kwamba hatua hiyo ya Prof. Mbarawa kihamisha viongozi wa mamlaka za maji waliokaa muda mrefu eneo moja la kituo cha kazi, ni endelevu ili kupata matokeo chanya katika sekta ya maji nchini.
Leave a comment