May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Makubi awapa mtihani wakurugenzi sekta ya afya

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Prof. Abel Makubi

Spread the love

 

WAKURUGENZI wa Hospitali za Rufaa za Mikoa, Kanda Maalumu, Taifa pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, wametakiwa kusimamia vipaumbele vya wizara ya afya katika kuboresha huduma za afya ili kuondoa kero kwa wananchi. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Maagizo hayo yametolewa leo tarehe 27 Januari, 2022 na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Abel Makubi wakati wa kikao kazi cha tathmini ya utoaji wa huduma kwa kipindi cha miezi sita kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamini Mkapa jijini Dodoma.

Amesema taasisi zinaongozwa na sera, vipaumbele za sekta pamoja na dira ya Taifa ya maendeleo hivyo mpango mkakati wa wizara lazima utekelezeke ili kutoa huduma bora na ya viwango kwa watanzania.

“Sasa hivi sekta ya afya ipo katika maboresho makubwa ya miundombinu pamoja na vifaa, hivyo lazima tuunganishe maboresho hayo ili yaoneshe ubora wa huduma pale mgonjwa anapofika aweze kupata huduma zote anazohitaji katika hospitali,” amesema.

Ameongeza tathimini hiyo itawaonesha kwa namna gani wamefanya vizuri na pale ambapo hawakufanya vizuri kwa wananchi wafanye vyema wanapoelekea mwisho wa mwaka wa bajeti ya Serikali.

“Tunategemea wakurugenzi wanaporudi kwenye hospitali zao wakaendelee kuboresha huduma zaidi na kuondoa kero na malalamiko kwa wananchi.

“Wizara haitegemei kusikia kero kutoka kwenye maeneo yao kwamba mama ameshindwa kupata huduma au amekosa dawa hususani kwenye hospitali ya Kanda na Taifa, lazima mwananchi apate dawa,” alisisitiza Prof. Makubi.

Aidha, Katibu Mkuu huyo aliwataka Viongozi wote wa hospitali na taasisi wafanye kazi kwa uadilifu, kujituma kwa bidii.

“Wizara imekuja na mfumo wa kuwapima wakurugenzi, tunataka viongozi waende kwa matokeo kwani hospitali hizo kubwa wanao uwezo wa kununua dawa, tutawapima kufikia malengo tuliyowapatia na kama tumewapa kuongeza dawa kwa asilimia 10 hadi 20 hivyo tunataka kuona hilo linafikiwa,” amesema.

Kwa upande mwingine Prof. Makubi amezitaka taasisi hizo kuunganisha nguvu katika kampeni shirikishi na harakishi ya uhamasishaji wa chanjo dhidi ya UVIKO-19 ili wananchi wahamasike kuchanja zaidi ili kufikia malengo waliyojiwekea ambapo hadi sasa wamefikia asilimia 3.3 ya wananchi wamepata chanjo ya UVIKO-19.

Kuhusu matumizi holela ya dawa za ‘Antibiotics’ Prof. Makubi amesema wamelipokea agizo la Waziri wa afya, Ummy Mwalimu kupitia kwa Mfamasia Mkuu wa Serikali kwamba wanalifanyia kazi.

Amesema wameanza kuliandalia mkakati wa uratibu kuona ni jinsi gani mtu anayehitaji hizo dawa apatiwe kwa kuzingatia miongozo ambayo inasisimia matumizi ya dawa.

Hata hivyo, amewakumbusha wananchi kuacha kutumia dawa kiholela pasipo kuandikiwa na watoa huduma na vile vile kwa wauza dawa wasitoe dawa bila kwa wananchi bila ya kuwa na cheti na kuwataka wafuate miongozo ya dawa.

Katika kikao hicho Katibu Mkuu amewapitisha wakurugenzi katika maeneo ya vipaumbele vya wizara takriban kumi ikiwemo uboreshaji wa huduma za afya, bidhaa za dawa, UVIKO-19, Uongozi, Bima ya afya kwa wote, vifo vya mama na mtoto, Magonjwa ya kuambukiza (NCDs), huduma za kibingwa na bobezi, miundombinu na vifaa, watumishi, tehama na takwimu pamoja na tafiti.

error: Content is protected !!