July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba: Waziri fedha anarejesha kodi ya kichwa kinyemela

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi- CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, ni moja ya bajeti mbovu ambazo amewahi kuzipitia. Anaripoti Mwandishi wetu … (endelea).

Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo leo tarehe 19 Juni, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa uchambuzi wa CUF kuhusu bajeti hiyo kwa waandishi wa habari.

Amesema kitendo cha Dk. Mwigulu kupendekeza wale wote wenye namba ya utambulisho wa Taifa (NIDA) wapatiwe namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) na itumike kwenye miamala yote inayofanyika katika ununuzi na mauzo yanayofanyika ndani ya nchi, ni kurejesha kodi ya kichwa kinyemela.

“Kuunganisha Kitambulisho cha Nida na masuala ya kodi, Waziri (Dk. Mwigulu) anaanzisha kodi ya kichwa kinyemela… lilishatuletea matatizo, waliondoe kabla ya watu kwenda mtaani kulipinga jambo hili,” amesema.

Amesema pendekezo hilo la Dk. Mwigulu linaweza kukwamisha zoezi la Watanzania kujisali kupata kitambulisho cha NIDA.

Amesema vitambulisho hivyo vitumike kama nyenzo ya maendeleo kama vile kukopa kupata misaada.

Amesema pamoja na Dk. Mwigulu kurudia mara nyingi kumtaja na kumsifia Rais Samia, hotuba ya Bajeti haiendelezi msimamo wa Rais wa kuboresha mazingira ya kuimarisha sekta binafsi, kuwa na sera zinazotabirika na kuendeleza siasa za maridhiano.

Amesema kwa muda mrefu bajeti kuu za serikali ya Tanzania hakuna ziada kwenye bajeti ya kawaida.

“Kwa kawaida unahitaji mapato yanayokusanywa na Serikali yakidhi kugharamia matumizi ya kawaida na ibakie ziada utakayoleka kwenye bajeti ya maendeleo,” amesema.

Kutokana na hali hiyo amesema ni muhimu serikali ikaachia yale yanayoweza kutekelezwa na sekta binafsi yatekelezwe na sekta hizo kwa kuwa serikali haina fedha.

error: Content is protected !!