August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba amsindikiza msaliti mwenzake

Spread the love

PROFESA Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa amehudhuria mazishi ya Ashura Mustafa na kusema “tumepoteza jembe,” anaandika Pendo Omary.

Prof. Lipumba ametoa kauli hiyo leo kwenye msiba wa Ashura Mustafa, aliyekua mwanachama wa CUF na Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi (BKUT) wakati akitoa salamu za rambirambi Mburahati jijini Dar es Salaam.

“Hakika tumepoteza jembe. Ashura alikuwa mtu wa kujituma ndani ya chama na alikuwa rafiki wa kila mtu,” amesema Prof. Lipumba.

Amesema baada ya yeye kuandika barua ya kujiuzulu uongozi Agosti mwaka jana, Ashura alikuwa miongoni mwa wanachama waliokwenda mara kwa mara nyumbani kwake kumshawishi arejee kuongoza chama.

“Alifanya hivyo bila kuchoka kwa kuwa alikuwa akikipenda chama na hata alipokuwa anauguliwa na mtoto wake, nami nilikwenda kumwona,” amesema.

Akizungumza na waombolezaji waliohudhuria mazishi hayo, Prof. Lipumba amesema kuwepo kwa idadi kubwa ya watu waliojitokeza katika mazishi, kunadhihirisha marehemu alikuwa akipendwa.

Miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria mazishi ni Mohamed Habib Mnyaa, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mkanyageni, Mkoa wa Kusini Pemba na waziri kivuli kuhusu masuala ya maliasili katika Bunge la 10.

Kwenye msiba huo, kwa upande wa wanachama wa chama hicho, wengi waliohudhuria ni viongozi walioko upande wa Prof. Lipumba katika kipindi ambacho chama hicho kipo kwenye mgogoro wa uongozi. Ashura amezikwa leo kwenye makaburi ya Kisutu.

Prof. Lipumba na marehemu Ashura walisimamishwa uanachama. Baadaye Prof. Lipumba alifukuzwa na Ashura alikuwa anasubiri kujitetea.

error: Content is protected !!