Wednesday , 27 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Lipumba kupata pigo jingine la mwaka  
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba kupata pigo jingine la mwaka  

Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

WABUNGE karibu wote wa Chama cha Wananchi (CUF), kutokea Unguja na Pemba,  wanatarajiwa kutangaza kuondoka kwenye chama hicho, muda wowote kutoka sasa. Anaripoti Yusuph Katimba … (endelea).

Taarifa zilizofikia MwanaHALISI ONLINE kutoka Dodoma, Dar es Salaam, Unguja na Pemba zinasema, hatua ya wabunge hao kutaka kuikimbia CUF, inatokana na kutokubaliana na uongozi wa Prof. Ibrahim Lipumba na shinikizo kutoka kwa wapiga kura wao.

Mtoa taarifa wetu ambaye ni mmoja wa viongozi waandamizi ndani ya chama hicho na ambaye hakupenda kutajwa jina lake, amethibitishia mwandishi wa habari hizi, taarifa za kuondoka kwa wabunge hao.

Amesema, “ni kweli baadhi ya wabunge wetu, hasa kutoka Unguja na Pemba, wamepanga kuondoka kabla ya kumaliza kipindi chao cha ubunge.

Anataja sababu ya kuondoka kwao ni kushinikizwa na wapigakura ambao wengi wao, ni wafuasi wa aliyekuwa katibu mkuu wao, Maalim Seif Sharif Hamad.

Anasema, “CUF bado kuna shida. Kuna watu hawajui siasa. Wanachowaza wao, ni kupambana na kila anayewapinga. Hii siyo sahihi. Hawa wabunge ni watu muhimu sana kwa uhai wa chama na mustakabali wake.”

Alipoulizwa kutokana na hali hiyo, wao kama chama, wanatarajia kuchukua hatua gani ili kukabiliana na “hama hama hiyo,” haraka kiongozi huyo aliishia kusema, “kwa kweli, bado tuna kazi kubwa.”

Kupatikana kwa taarifa hizi kumekuja siku moja baada ya katibu mkuu mpya wa chama hicho, Khalifa Sulemani Khalifa, kuwataka wabunge wote kuripoti kwa Prof. Lipumba na kuomba radhi.

Kwa mujibu wa Khalifa, wabunge ambao watashindwa kuitikia wito huo, wajiandae kufukuzwa ndani ya chama hicho. Alisema, “hatuko tayari kulea wabunge ambao siyo watiifu kwetu.”

Chama cha CUF, kimeingia katika mgogoro mkubwa wa uongozi, kufuatia Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kumrejesha madarakani kwa nguvu, Prof. Ibrahim Lipumba.

Mbali na kumrejesha Lipumba CUF, Jaji Mutungi alimbariki Magdalena Sakaya, kushika nafasi ya kaimu katibu mkuu, wakati Maalim Seif bado alikuwa akiendelea kuhudumu kwenye wadhifa wake wa ukatibu mkuu.

Naye mbunge mmoja wa CUF kutoka Pemba, alipoulizwa juu ya kuwapo kwa taarifa za baadhi ya wabunge kutaka kujiuzulu, yeye akiwamo, haraka alisema, “…wewe kaka subiri. Sisi hatuwezi kufanya kazi na Lipumba.”

Alipoelezwa kuwa haoni kuwa hatua yao hiyo, itasababisha kurudiwa kwa uchaguzi, jambo ambalo litaingiza nchi kwenye matumizi makubwa ya fedha za umma na kusababisha majimbo hayo kuongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinyume na matakwa ya wapiga kura wao, haraka alisema, “hayo mengine ni yako.”

Anasema, “chaguzi ndogo nyingi zimefanyika na mamilioni ya fedha yametumika, lakini hakuna aliyeonekana kuonea huruma fedha hizo. Kibaya zaidi, baadhi ya chaguzi zimefanyika baada ya serikali yenyewe, kushiriki katika ununuzi wa wabunge wa upinzani.”

Aliongeza, “…hao wapiga kura unaowataja, ndio wanaotutaka kuondoka CUF. Lipumba anatumiwa na serikali, sisi hatutaki kuwa sehemu ya uchafu huo.”

Mwenyekiti wa wabunge wa CUF, Sulemani Bungara, maarufu kwa jina la Bwege, hakupatikana kueleza iwapo anazifahamu taarifa hizo; na au naye ni mmoja wa wanaotarajiwa kujiondoa.

Hata hivyo, Bwege amewahi kunukuliwa akisema, yeye ataendelea kuwa mwanachama wa CUF, “labda hao wanaojiiita wenye chama,” waamue kumfukuza.

Akichambua athari za kuondoka kwa wabunge hao, mtoa taarifa huyo ambaye amepata kuwa kiongozi wa juu wa CUF, wakati Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa katibu mkuu wa chama hicho anasema, “ni kweli hawa wabunge walikuwa kwenye timu ya Maalim.

“Lakini sisi tunawahitaji kwa ajili ya kuendelea kupata ruzuku. Kuwafukuza au kujiuzulu wao wenyewe, kutasababisha kupungua kwa ruzuku ya chama.”

Anasema, “hivyo kwa vyovyote vile, kunahitajika kutumika busara kubwa ya kuwazuia kuondoka. Lakini baadhi ya viongozi wetu, wanataka kutumia nguvu, badala ya ushawishi wa hoja. Tukiendelea hivi, wabunge wote wataondoka.”

Chama cha CUF kina wabunge 22 wa majimbo Unguja na Pemba; kunatarajiwa kuwa wabunge takribani 20 wanaweza kuondoka ili kuungana na Maalim Seif katika kile wanachokiita, “mapambano ya kudai haki.”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

error: Content is protected !!