September 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba atumbua tena CUF

Spread the love

MGOGORO ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) bado unafukuta ambapo leo Prof. Ibrahim Lipumba, amegomea mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho ulioitishwa kesho visiwani Zanzibar, anaandika Pendo Omary.

Anasema, taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari kuhusu kufanyika kwa mkutano huo hazitambua kwa kuwa, mamlaka zinazohusika kuitisha kikao hicho hazijakidhi matakwa.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam kupitia taarifa iliyoandaliwa na Magdalena Sakaya, Naibu Katibu Mkuu Bara aliyesimamishwa na chama hicho amesema, matakwa ya katiba hayakuzingatiwa.

“Wajibu wa Kamati ya Utendaji ya Taifa utakuwa kuandaa.. agenda za Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na kutayarisha na kuhifadhi mihtusari ya vikao vyote vya Mkutano Mkuu wa Taifa, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na vya kamati ya utendaji ya taifa yenyewe na kuwasilisha taarifa ya yatokanayo kutokana na utekelezaji wa maamuzi ya kikao kilichohusika kilichopita,” Prof. Lipumba amenukuu katiba ya chama hicho ibara ya 85(5).

Prof. Lipumba amesema, Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa chama hicho yupo nje ya nchi na kwamba, kutokana na Katiba ya CUF;

“Mimi ndiye mwenye mamlaka ya Katibu Mkuu kwa sababu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara kikatiba ndiye msimamizi namba moja wa Katibu Mkuu,” amesema.

Amesema, Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la 2014 kifungu cha 95 (3) kinaeleza “Naibu Katibu Mkuu atakayemfuata Katibu Mkuu kwa madaraka ni yule aliyetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anaotoka Katibu Mkuu,” na kwamba, Katibu Mkuu anatoka Zanzibar na yeye anatoka Bara.

Hata hivyo Prof. amesisitiza kuwa, Sakaya hana taarifa ya kikao hicho cha kamati tendaji kilichofanyika Zanzibar.

Pamoja na kuwepo kwa sintofahamu kutokana na uamuzi wa Jaji Mutungi kumtambua Prof. Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho, (Lipumba) amepongeza kurejeshwa kwake.

Prof. Lipumba, mwenyekiti wa chama hicho aliyesimamishwa na CUF mwezi uliopita, alirejea kwenye nafasi hiyo kwa kauli ya Jaji Mutungu, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Kurejea kwake pia kumesimamiwa na vyombo vya dola huku vurugu na uharibifu wa mali ukiripotiwa kutokea kwenye Ofisi Kuu ya chama hicho Buguruni jijini Dar es Salaam juzi.

Prof. Lipumba ameeleza kushangazwa na hatua ya Jaji Mutungi kukosolewa na baadhi ya wanasheria na majaji mashuhuri kuwa, hakuna sheria inayompa furasa jaji huyo kuchukua hatua aliyoichukua.

 

error: Content is protected !!