December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba ataka kasi ongezeko la watu ipunguzwe, ataja athari zake

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ameishauri Serikali ipunguze kasi ya ongezeko la idadi ya watu, ili kukabiliana na athari zake kiuchumi na kijamii. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Prof. Lipumba ametoa ushauri huo Leo Jumanne, tarehe 1 Novemba 2022, siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kutangaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, akisema ongezeko la watu katika kipindi cha miaka 10 (2012-2022) limefikia asilimia 3.2.

“Rais Samia ametangaza kasi ya ongezeko la idadi ya watu ni 3.2%, sensa ya 2012 ilionyesha kasi hiyo ni 2.7%. ongezeko la 3.2% ni miongoni mwa ongezeko kubwa duniani nchi nyingi za Afrika ziko chini ya 3%. Hii ni changamoto tukiendelea na kasi hii maana yake baada ya miaka 10 tutakuwa na Watanzania milioni 84,” amesema Prof. Lipumba.

Mtaalamu huyo wa masuala ya uchumi, ametaja athari za ongezeko hilo, akisema “maana yake ni kwamba, inapokuwa 3.2% na mwaka huu inakadiriwa uchumi utakuwa kwa 4.9%, wastani wa kipato cha kila mtu mabadiliko yanakuwa ni madogo sana.

“Mnapokuwa na kasi kubwa maana yake kile kinachozalishwa kikigawanywa kwa wananchi wote kila mwananchi anapata kidogo,” amesema Prof. Lipumba.

Mwenyekiti huyo wa CUF, amesema kukiwa na ongezeko la kasi hiyo itabidi kasi ya ongezeko la ajira iongezeke pia, huku akisema idadi ya watu ikiongezeka, watoto ambao wanahitaji msaada wanakuwa wengi kuliko vijana wanaozalisha mali.

Amesema, kukiwa na ongezeko hilo, inabidi Serikali iongeze mikakati ya kuongeza uzalishaji wa chakula kulingana na idadi ya watu, la sivyo wananchi watakumbwa na baa la njaa.

“Ukiwa na ongezeko la watu inabidi ujiandae kuandaa madarasa, la sivyo vijana hawatapata elimu Bora,” amesema Prof. Lipumba.

Mwanasiasa huyo ameshauri Serikali itoe elimu ya kutosha ya uzazi wa mpango kwa wananchi, hasa wanawake ili kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu.

Hata hivyo, Prof. Lipumba ametaja faida za ongezeko la watu, akisema “lakini jambo kubwa ukiwa na ongezeko la kasi hii, kuna athari nzuri kwamba mnapokuwa na idadi kubwa ya vijana mnaweza kupata faida ikiwa vijana watapata kazi na kuwa na ongezeko la uchumi.”

Jana, Rais Samia ametaja ongezeko la watu 16,812,197 sawa na 3.2% ndani ya miaka 10 kutoka watu milioni 44.9 mwaka 2012 hadi watu milioni 61.7 mwaka 2022.

error: Content is protected !!