Monday , 22 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Prof. Lipumba aomba ‘talaka rejea’ CUF
Habari za SiasaTangulizi

Prof. Lipumba aomba ‘talaka rejea’ CUF

Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

CHAMA cha Wananchi (CUF) kinaelekea kugota. Hofu na mashaka vimeanza kummeza Prof. Ibrahim Lipumba ambapo sasa anahitaji suluhu na Maalim Seif Shariff Hamad, anaandika Faki Sosi.

Prof. Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, ameonesha hofu ya chama hicho kufutiwa usajili endapo mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama hicho utakosa suluhu.

Ameeleza kuwa, ni wakati sasa kwake kuingia kwenye suluhu dhidi ya upande wa Maalim Seif, Katibu Mkuu wa chama hicho ili kunusuru chama hicho kisifutwe na Msajili wa Vyama vya Siasa kutokana na mgogoro uliopo kwa sasa.

Amesema hayo mbele ya wanahabari katika Ofisi Kuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 16 ya wanachama wa CUF waliofariki kwenye vurugu za kisiasa zilizotokea tarehe 26/27 Januari, 2001 visiwani Zanzibar.

Prof. Lipumba amesema kuwa, bila kuwepo kwa mazungumzo ya kunusuru chama hicho, kuna hatari ya kufutwa kwenye Daftari la Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Kwenye mkutano wake Prof. Lipumba amesema kuwa, CUF mwaka 2001 kilipoteza wanachama wake wakati wa kupigania haki na sasa kutokana na mgogoro uliopo, ni vema suluhu ikapatikana ili kuendelea kuwa na amani ndani ya chama hicho.

“Katiba yetu inahamasisha amani…” amesema Prof. Lipumba na kuongeza kwamba “ni vema maadhimisho hayo yakatumika kama njia ya mazungumzo ili kumaliza sintofahamu iliyopo ndani ya chama CUF.”

Bila kumung’unya maneno Prof. Lipumba amesema kuwa, mgogoro uliopo ndani ya chama hicho unamuumiza na kwamba, kwake ni bora kukaa meza moja na Maalim Seif ili kutuliza machafuko yaliyopo kwa sasa.

Na kwamba, muungano uliopo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unalenga kuhimiza maendeleo ya amani, utulivu na usalama.

“…ili chama chetu kiweze kudumu yatupasa tufanye kazi pamoja, utengano uliopo utakiumiza chama kwa kuwa kinaweza kufungwa kwa sababu za sheria ya vyama vya siasa.

“Sheria hii haikihitaji chama kiwepo Zanzibar bali Tanzania nzima ambapo ndio muungano wetu.”

Amedai kuwa, mgogoro ndani ya chama hicho haumuumizi pekee yake bali viongozi wa dini ambao wamekuwa wakimfuata na kumshauri kukaa meza moja na Maalim Seif ili kuweka mambo sasa.

“Maalim Seif usiogope, hii ni ofisi yako njoo tufahamishane yanayoendelea na kujenga chama chetu.

“Naumia na hiki kinachoendelea, nataka tufanye kazi pamoja. Mimi nakutambua kama Katibu Mkuu wangu,” amesema Prof. Lipumba.

Mgogoro ndani ya CUF uliibuka mara baada ya Prof. Lipumba kutangaza kujiuzulu baada ya kumwandikia barua Maalim Seif ya kung’atuka na baadaye kudai ameandika barua ya kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu uenyekiti wa chama hicho.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

NMB yadhamini Mkutano Mkuu ALAT, kufunguliwa na Samia

Spread the loveBENKI ya NMB, imekabidhi hundi yenye thamani ya Sh. 120...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mipango na uwekezaji kutumia bilioni 121.3, mradi wa Bagamoyo wapewa kipaumbele

Spread the loveWIZARA ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, imeliomba Bunge...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mbunge ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the loveMBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze kasi...

ElimuHabari za Siasa

MbungeCCM ataka kasi uzalishaji walimu ipunguzwe akidai hakuna ajira

Spread the love  MBUNGE wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi, ameishauri Serikali ipunguze...

error: Content is protected !!