Wednesday , 27 September 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Mradi wa Lipumba kumng’oa Maalim Seif wakumbana na vigingi
Habari za Siasa

Mradi wa Lipumba kumng’oa Maalim Seif wakumbana na vigingi

Spread the love
MKAKATI wa mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), “aliyechongwa” na msajili wa vyama vya siasa, Prof. Ibrahimu Lipumba, kutaka kuwaondoa wafuasi wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamadi, sasa umeiva. Anaripoti Faki Sosi…(endelea).

Taarifa kutoka kwa wafuasi wa Prof. Lipumba zinasema, mkakati huo unataka “kuwafyeka mbali,” wafuasi wa Maalim Seif, ili kurahisha kazi ya kumuondoa kiongozi huyo. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mkakati wa kumuondoa Maalim Seif, unasukwa kupitia “chaguzi feki,” zinazoendelea katika baadhi ya wilaya nchini.

Habari zinasema, miongoni mwa wilaya zilizopangwa kutumika ili kufanikisha mkakati wa kumng’oa Maalim Seif, ni pamoja na zile zilizopo jijini Dar es Salaam.

Tayari katika mkoa huo, wilayani Kinondoni ambako kulikuwa ngome kuu ya Maalim Seif,

kumeanza kusambaratishwa kwa kuwaengua wafuasi wake wote na kuingiza watu wanaomuunga mkono Prof. Lipumba.

“Hapa Kinondoni, tumeshaondoa vimelea vyote vya Maalim Seif. Katika wilaya hii, nguzo yake kuu, ilikuwa Juma Nkumbi, ambaye alikuwa mwenyekiti wa wilaya na mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa (BKT). Sisi tumefanya uchaguzi na kumuweka Rajabu Salim,” ananukuliwa Yusuph Bungilo, akieleza baadhi ya wafuasi wake.

Bungilo ambaye anajulikana kuwa mfuasi wa karibu wa Prof. Lipumba anasema, “uchaguzi katika wilaya ya Kinondoni, ulifanyika tarehe 24 Novemba.”

Anadai kuwa yeye ndiye aliyekuwa amepewa jukumu na viongozi wake kusimamia uchaguzi huo.

Mgogoro ndani ya CUF umepandikizwa ili kukifanya chama hicho kuacha madai yake ya msingi ya kuporwa ushindi wake iliyoupata kwenye uchaguzi mkuu wa rais na wawakilishi, Visiwani.

Katika uchaguzi huo wa tarehe 25 Oktoba 2015, Maalim Seif ambaye alikuwa ndiye mgombea urais wa chama hicho, anadai kuwa ndiye mshindi halali.

Anasema, matokeo ya uchaguzi huo yalifutwa kwa makusudi na Jecha Salim Jecha ili kumnufaisha aliyekuwa mshindani wake mkuu, mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Alli Mohammed Shein.

Maalim Seif anasema, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ametumia madaraka yake vibaya kwa kukubali kutumiwa na CCM kupandikizia mgogoro chama chake.

Vyanzo vya taarifa vinaeleza kuwa Prof. Lipumba amejipanga kufanya uchaguzi wa ndani kwenye mikoa yote nchini ili kuuondoa uongozi unamuunga mkono Maalim Seif.

Hata hivyo, mkurugenzi wa mipango na uchaguzi halali wa chama hicho, Shaweji Mketo, ameeleza kuwa “CUF taasisi,” haitambui chaguzi zinazoendeshwa na Prof. Lipumba na wafuasi wake.

“Sisi hatutambui uchaguzi wowote ndani ya chama na hao waliochaguana hatuwatambui. Chama chetu kinaendeshwa na katiba na kanuni zake. Hatuwezi kuwatambua wahuni waliojipachika vyeo,” ameeleza.

Amasema, kama uchaguzi huo umefanyika, basi utakuwa umefanywa kinyume na kanuni na katiba ya chama hicho.

“Kanuni zetu zipo wazi kuwa chaguzi zote ndani ya chama zinaiitishwa na Baraza Kuu.

Baraza halijakutana kuidhinisha uchaguzi. Mimi  ndiye mkurugenzi wa uchaguzi. Sifahamu chochote kuhusu hicho kinachoitwa, uchaguzi.”

Amesema matendo maovu ya Prof. Lipumba na wafuasi wake, yanatokana na  mafanikio makubwa ambayo chama hicho iliyapata kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Anasema, “CUF ilipata wabunge na madiwani wengi na kwa mamara ya kwanza iliongoza  halmashauri na manispaa. Haya siyo mafanikio madogo. Prof. Lipumba amekubali kutumika ili kutusambaratisha. Hatutakubali.”

Mketo amewatoa hofu wafuasi wa chama hicho kuwa CUF iko imara na wanatarajia muda si mrefu taasisi hiyo itarudi mikononi mwao kupitia kesi zilizofunguliwa mahakamani.

Naye naibu mkurugenzi wa habari na Mawasiliano, Mbarala Maharagande amesema, uchaguzi huo hatambuliwi na masuala yote ya kesi na uchaguzi yapo mahakamani.

Mgogoro ndani ya CUF umeibuka kufuatia Jaji Mutungi, “kuridhia” kinyume cha taratibu, Prof. Lipumba kutengua barua yake ya kujiuzulu wadhifa wake. 

Prof. Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa CUF, tarehe 6 Agosti 2015. Akarejeshwa kwenye nafasi yake na Jaji Mutungi, tarehe 13 Juni 2016.

Prof. Lipumba  aliondoka ndani ya CUF katikati ya kipindi cha kampeni kwa madai kuwa haungi mkono makubaliano yaliyofikiwa na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ya kukakaribishwa Edwad Lowasa, kuwa mgombea wao wa urais.

Lowassa, waziri mkuu mstaafu wa Jamhuri, alijiengua CCM kati kati ya mwaka 2015. Alitangaza kujiunga na Chadema siku tatu baada ya kuenguliwa katika mbio za urais.

Wiki moja baadaye akafanywa kuwa mgombea urais wa Ukawa, ambako alitoa upinzani kwa Rais John Magufuli.

Ukawa unaundwa na vyama vya National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), CUF, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Nation League for Democracy (NRD).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga: Usambazaji umeme vijijini mwisho Desemba 2023

Spread the love  NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo mwezi...

Habari za Siasa

Mgongano wa kimasilahi wamhamisha Chande TTTCL

Spread the love  ALIYEKUWA Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),...

Habari za SiasaTangulizi

Mgawo wa umeme: Rais Samia ampa miezi sita bosi mpya TANESCO

Spread the love  RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amempa miezi sita Mkurugenzi...

Habari za Siasa

Rais Samia avunja bodi ya REA

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amemteua Balozi Jacob Kingu, kuwa...

error: Content is protected !!