September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba ampopoa Mbowe

Spread the love

HATUA ya Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) – Taifa, kusoma hadharani barua aliyomuandikia Rais John Magufuli, imekebehiwa. Anaripoti Hamis Mguta, Dar es Salaam … (endelea).

Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa CUF – Taifa amekejeli hatua hiyo na kusema, ‘unapoisoma hadharani na pengine haijafika kwa rais, unategemea nini?’

Tarehe 3 Februari 2020 mbele ya wanahabari, Mbowe alisoma barua aliyomwandikia Rais John Magifuli akiainisha mambo kadhaa ikiwemo kufuta uchaguzi wa serikali za mitaa na Tume Huru ya Uchaguzi.

Leo tarehe 1 Februari 2020, Prof. Lipumba amesema, suala hilo linahitaji mbinu za kisiasa katika kumshawishi Rais Magufuli, kukubali maridhiano na vyama vya siasa vya upinzani.

“Unamwandikia barua rais, kabla hajaipata iko mitandao ya kijamii, unategemea nini? Lakini unapohitaji, mundikie na mpe muda. Unakuja kueleza umemuandikia barua, haijafika iko mitandaoni unategemea unayemuandikia ataimpa uzito.

“Hata mimi inawezekana nimeandika barua kuhitaji jambo, lakini siwezi kuiweka mitandao ya kijamii. Kuna namna inahitaji diplomasia ya hali ya juu katika hali hii,” amesema Prof. Lipumba.

Akizungumza kususa uchaguzi, Prof. Lipumba amesema, kwa mazingira yoyote yale, chama chake hakitasusa kushiriki.

Amesema, suala la kutoshiriki uchaguzi huo kutokana na kutokuwepo tume hiyo, haliungi mkono, licha ya kukiri ya kwamba, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haiko huru.

“Mtu anasema bila Tume Huru hatuwezi kuingia kwenye uchaguzi, hilo huwezi kusikia kutoka kwangu sababu najua hata kupigania Uhuru, wazee wetu Tanganyika walipigania Uhuru katika mazingira magumu,” amesema Prof. Lipumba.

Wakati huo huo, Prof. Lipumba amemshauri Rais Magufuli kuanza utekelezaji wa ahadi yake, katika kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru, aliyoitoa mbele ya mabalozi hivi karibuni.

“Kwa kuzingatia kwamba rais ametuhakimishia hilo mbele ya wanadiplomasia, tunashawishika kuamini hilo. CUF tunamuomba kutembea na kauli yake.

“Hilo suala ni mchakati sio jambo la siku moja. Kwanza aondoe zuio la mikutano hili litatoa fursa kwa vyama vyote kufikisha sera na itikadi zao kwa wananchi,” amesema Prof. Lipumba na kuongeza:

“Pili, tunamshauri rais akutane na vyama vya siasa kubalishana mawazo kuhusu mambo muhimu, ikiwemo kuboresha NEC (Tume ya Uchaguzi) ili iwe huru na itende haki. Wadau wakutane waeleze vikwazo gani vinaweza sababisha uchaguzi usiwe huru na haki ili viweze kurekebishwa.”

error: Content is protected !!