December 8, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba akacha uzinduzi wa ACT-Tanzania

Kiongozi Mkuu wa ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akipongezwa na wanachama wake katika mkutano wa mkuu wa chama hicho

Kiongozi Mkuu wa ACT-Tanzania, Zitto Kabwe akipongezwa na wanachama wake katika mkutano wa mkuu wa chama hicho

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba, amekacha uzinduzi wa chama kipya cha ACT- Tanzania, anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kutoka kwa watu waliokaribu na kiongozi huyo zinasema, Prof. Lipumba amekacha kuhudhuria uzinduzi wa ACT kwa kile kilichoitwa, “hofu ya kuchafuka.”

“Prof. Lipumba hakuhudhuria mkutano huo kwa sababu ya mahusiano yake na Chadema, ambacho ni moja ya vyama vinavyounda UKAWA,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa CUF.

Chama cha ACT, kinaundwa kwa asilimia kubwa na waliokuwa viongozi na wanachama kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Prof. Lipumba alikuwa miongoni mwa wasomi wa ndani na nje ya nchi walioalikwa kutoa mada katika uzinduzi wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaa, leo 29 Machi 2015.

Mbali na Prof. Lipumba, wengine ambao wamekacha uzinduzi wa ACT-Tanzania, ni  Samia Nkrumah, Kiongozi wa Chama cha CPP cha Ghana na mtoto wa Rais wa kwanza wa Ghana, Osagyefo Kwame Nkrumah.

Katika orodha hiyo, walitajwa kuwamo pia, Ababu Namwamba-Katibu Mkuu wa Chama cha ODM cha Kenya; Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Kenya; mabalozi wa nchi mbalimbali walioko nchini; kiongozi wa vyama rafiki vya Ujerumani, Die Linke na Umoja wa vyama vya mrengo wa kushoto Progressive Alliance.

Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, hatua ya Prof. Lipumba kutohudhuria uzinduzi wa mkutano huo, unaashiria kutokubaliana na uadilifu wa waanzilishi wa ACT.

Aidha, hatua ya Prof. Lipumba kususia uzinduzi wa ACT, yaweza kuwa imesukumwa na kutaka kuimarisha umoja ndani ya UKAWA.

ACT kimezindua ilani yake ya uchaguzi, kutangaza viongozi; na kudai kuwa kitarejesha Azimio la Arusha, ambalo lilikufa kabla ya muasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akiwa bado yuko ulimwenguni.

error: Content is protected !!